Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb), amesema kuwa uwepo wa Kituo cha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika eneo la Horohoro, kinachounganisha Tanzania na nchi ya Kenya, kutachochea shughuli za kiuchumi kati ya nchi hizo mbili pamoja na nchi nyingine za jirani.
Waziri Silaa alitoa tamko hilo tarehe 23 Januari, 2025 wakati akikagua mradi wa ufikishaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Mombasa kupitia Kituo cha Horohoro kilichopo wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga. Maunganisho hayo ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano yatawezesha Mkongo wa Taifa kuunganishwa na mikongo ya baharini iliyopo katika pwani ya Mombasa.
“Leo tumekuja hapa kuona kazi kubwa iliyofanyika ya kutengeneza njia mbadala ya Mkongo ambao unaunganisha nchi yetu na nchi ya Kenya kupitia hapa Horohoro kwenda Mombasa, Kenya na kuongeza kuwa kazi ya njia hii inaenda kufanya Mkongo wetu wa Taifa wa Mawasiliano kuwa na njia ya Dar es Salaam ambayo inaunganika na Mikongo ya Mawasiliano ya chini ya Bahari lakini sasa kutakuwa na njia mbadala ya kuunganisha Mkongo wa Taifa na mtandao wake na mikongo saba ya chini ya bahari iliyopo Mombasa,” alisema Waziri Silaa.
Akimkaribisha Mheshimiwa Waziri kukagua kituo hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) CPA Moremi Marwa amesema kuwa Hadi kufikia Disemba 2024 jumla ya Kilomita 13,991 za Mkongo zimejengwa zikiunganisha mikoa yote ya Tanzania Bara, Wilaya 109, pamoja na nchi saba (7) zinazopakana na Tanzania ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi, na Msumbiji.
Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirika hilo Mhandisi Cecil Francis amesema manufaa ya maunganisho ya Mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka Horohoro hadi Mombasa ni pamoja na kuimarika kwa maunganisho ya kikanda, na kuongeza thamani ya mkongo wa taifa wa mawasiliano na hivyo kufungua fursa mpya za biashara na mapato.
Waziri Silaa aliwapongeza Shirika la Mawasiliano la Tanzania (TTCL) kwa kazi kubwa waliyoifanya na watalaamu wa ndani waliyofanya kazi hii na kutangaza kuwa kazi hii imekamilika.
“Kuanzia mwezi wa pili, mkongo utaanza kutumika na tutatengeneza utaratibu mzuri wa kuja kuzindua na wenzetu wa Kenya ili watanzania wafahamu na wananchi wa nchi zote zinazotuzunguka wajue kwamba sasa njia hii ya mkongo kwenda Mombasa imekamilika, aliongeza Waziri Silaa.
“Na wote mnafahamu hawa vijana wetu (Gen-Z), afya ipo katika mawasiliano, habari ipo kwenye mawasiliano, biashara ipo kwenye mawasiliano, elimu ipo kwenye mawasiliano, kilimo kipo kwenye mawasiliano. Sisi kama sekta ya mawasiliano, kazi yetu ni kuhakikisha maeneo haya yanawezeshwa katika huduma hii ili kuhakikisha TEHAMA inachangia ukuaji wa uchumi wa nchi hii,” alisema Waziri Silaa.