AKILI ZA KIJIWENI: Karibu sana kocha Heric wa KenGold

NAKUKARIBISHA kwa moyo mkunjufu kocha wa mpira Vladislav Heric ambaye umepata shavu hapo KenGold FC ambayo inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha, jambo la kwanza na la msingi nakuomba uangalie msimamo wa ligi na uione timu yako mpya ilipo. Ipo mkiani kabisa na ina pointi sita tu ilizopata kwenye mechi 16.

Hadi jamaa wameamua kukufuata na kukubali masharti yako ili wakuajiri maana yake wanaamini wewe utakuwa mwokozi wao dhidi ya janga la kushuka daraja ambalo linawanyemelea hivi sasa.

Hapa kijiweni wamenituma nikuambie mazingira unayofundisha hivi sasa ni tofauti kabisa na kule Afrika Kusini, hivyo jitahidi sana kuendana na mazingira yanayozunguka soka la Tanzania ili mambo yakuendee vizuri.

Huku timu inalazimika kusafiri kilomita nyingi kwa basi kutoka kituo kimoja cha mchezo kwenda kingine huku wachezaji wakipata siku mbili tu za kupumzika na kujiandaa na mechi lakini bado inatakiwa kuingia uwanjani kucheza.

Inabidi ujiandae kukabiliana na mazingira ya namna hiyo vinginevyo ligi haitokuonea huruma na mwishowe, wewe ndio utakuja kuwajibika likitokea la kutokea kwa timu maana matumaini yamekuwa makubwa kwako.

Nakukumbusha pia jitahidi sana kuishi vizuri na wasaidizi na wachezaji wako badala ya kuwabagua au kuwatenga ili wakupiganie ndani ya uwanja timu ipate matokeo mazuri ambayo yataibeba timu na sivii yako wewe mwenyewe.

Ukiwatenga hao jamaa wataanza kampeni za chini chini za kuhakikisha unaondoka na hapo itakuwa ngumu kwako kufanikiwa kwa vile timu itakuwa haipati matokeo mazuri jambo ambalo litaushawishi uongozi ukuweke kando na nafasi yako apewe mwingine.

Vinginevyo karibu Tanzania. Hii ni nchi nzuri ambayo ina watu waungwana na ukifanikiwa kuwapa kile wanachokitegemea utakuwa rafiki yao mkubwa na kwa hakika watakupa ukubwa na fedha nyingi zaidi ya zile unazozipata sasa.

Related Posts