Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amesema bado hajamalizana na wabunge 19 waliovuliwa uanachama na chama hicho, akisisitiza kuwa suala la kurejeshwa kwao ndani ya chama ni jambo linalohitaji uamuzi wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chadema.
Kamati Kuu ya Chadema iliwavua nyadhifa na uanachama wabunge hao ambao ni Halima Mdee na wenzie 18, Novemba 27, 2020 na Baraza kuu likaubariki uamuzi huo.
Akizungumza leo Ijumaa, Januari 24, 2025, katika mahojiano na kituo cha redio cha Bongo FM nyumbani kwake Dar es Salaam, Lissu amesema chama kimeelekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa wanachama wa namna hiyo.
“Utaratibu wa chama unasema kuwa mwanachama aliyefukuzwa anaweza kurudishwa endapo tu ngazi ya juu zaidi ya ile iliyomfukuza itamruhusu. Hawa walifukuzwa na Baraza Kuu baada ya uamuzi wa Kamati Kuu. Chombo pekee chenye mamlaka ya kuwarejesha ni Mkutano Mkuu wa Taifa.”
Lissu aliongeza kuwa suala hilo haliko mikononi mwake kama mwenyekiti wa chama.
“Wakija kwangu, nitawaambia samahani, waombe Mkutano Mkuu wa Taifa. Mimi nataka tufanye kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu tulizojitungia wenyewe,” amesema Lissu.
“Bado nina shida nao sana”
Akizungumzia zaidi, Lissu amesema anahitaji majibu ya maswali mengi kuhusu jinsi wabunge hao walivyopata nafasi zao bungeni bila ridhaa ya chama.
“Watu hawa waliingiaje bungeni? Fomu zao za kugombea zilitiwa saini na nani? Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, hakuwahi kusaini fomu hizo, na sheria inasema lazima zisainiwe na katibu mkuu, za kwao zilisainiwa na nani?” amehoji Lissu.
Pia ametaka kufahamu nani aliyempa taarifa ya uteuzi mbunge aliyekuwa gerezani, akieleza kuwa hali hiyo bado inaacha maswali mengi yasiyo na majibu.
“Natamani kama wanakuja kutafuta suluhu, waje wakiwa na mioyo iliyo safi na wazi. Wasiwe wanakuja kwa sababu uchaguzi unakaribia, wakitaka wawe tena wabunge” amesisitiza.
Mwenyekiti huyo ameongeza, “ikiwa Mkutano Mkuu wa Taifa utawasamehe na kuwarejesha Halima Mdee na wenzake, kupewa tena nafasi ya viti maalum, itahitajika mabadiliko ya taratibu na kanuni za chama.
“Tunapaswa kuwa na utaratibu wa kikatiba kwamba nafasi ya viti maalum ni miaka mitano tu, nje ya hapo waende majimboni,” amesema Lissu.
Lissu amesisitiza kuwa mabadiliko hayo ni muhimu kwa maendeleo ya chama na kuimarisha uwajibikaji wa viongozi wake.
Hata hivyo, Lissu amesema hajapokea ujumbe wowote wa pongezinkutoka kwa wabunge hao 19 na kwamba hata akiupata atashangaa.
Akizungumzia kuhusu kuteua wajumbe watano wa kamati kuu kati ya nafasi sita alizo nazo na kuacha nafasi moja wazi, Lissu amesema:
“Jambo hili lilileta mjadala mkubwa. Nia yangu ilikuwa kujaza nafasi zote sita mara moja, kwa sababu kamati kuu iliyomaliza muda wake, katika nafasi sita ambazo mwenyekiti anatakiwa kuteua, aliteua mmoja tu. Katiba inasema mwenyekiti anaweza kuteua wajumbe sita, lakini ukiacha nafasi hizo wazi, maana yake ni nini? Kuna ulazima gani wa kuweka kifungu hicho kwenye katiba?
“Nilitaka kujaza nafasi zote mara moja, lakini baada ya ushauri nilipewa maoni tofauti. Unakumbuka, kuna watu walisema huyu hashauriki, huyu mwanaharakati hashauriki. Hata hivyo, nilishauriwa kwamba ni vyema kuacha nafasi moja wazi kwa sababu huwezi kujua huko mbele ya safari nafasi hiyo inaweza kuwa muhimu,” amesema Lissu.
Lissu alishika wadhfa wa kuongoza chama hicho baada ya kupata kura 513 sawa na asilimia 51.5 dhidi ya Mbowe aliyepata kura 482 sawa na asilimia 48.3.