Athari za gharama kubwa za insulin

Insulin ni dawa muhimu kwa watu wanaoishi na ugonjwa wa kisukari, hasa aina ya kwanza ya kisukari. Kwa mamilioni ya watu duniani kote, insulin ni zaidi ya dawa, ni msaada wa maisha unaowezesha udhibiti wa viwango vya sukari mwilini.

Hata hivyo, gharama kubwa za insulin zimekuwa changamoto kubwa, hasa kwa wagonjwa wenye kipato cha chini na wale wanaoishi katika maeneo ya vijijini. Hali hii inatishia si tu afya ya wagonjwa, bali pia ustawi wa familia na jamii kwa ujumla.

Kwa Tanzania bei ya peni moja ya insulin ni kati ya Sh20,000 mpaka Sh30,000 na kuna wagonjwa wanatumia zaidi ya peni mbili kwa mwezi.

Kwa wagonjwa wanaotumia insulin kila siku, gharama kubwa zinaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya. Wengi hujikuta wakilazimika kupunguza dozi za insulini au hata kuacha kabisa kutumia kwa sababu ya kukosa uwezo wa kifedha.

Na hii kufanya sukari kupanda sana na kusababisha matatizo makubwa kama upofu, matatizo ya figo, magonjwa ya moyo, na hata kupoteza maisha. Pia, gharama hizi zinachangia msongo wa mawazo kwa wagonjwa na familia zao.

Wengine hujikuta wakitumia sehemu kubwa ya mapato yao kwa ajili ya ununuzi wa insulin, hali inayoweza kusababisha ukosefu wa mahitaji mengine muhimu kama chakula, elimu na malazi.

Kwa familia maskini, gharama hizi zinaweza kuwa mzigo usiobebeka na kuwalazimisha kufanya maamuzi magumu kati ya afya na mahitaji mengine ya msingi.

Insulin inasaidia kuboresha maisha ya wagonjwa wa aina ya kwanza ya kisukari na kuna wenye aina ya pili wanaotumia insulin na kuna wale wenye kisukari kipindi cha ujauzito na wanalazimika kutumia insulini kwa kuwapa uwezo wa kuendelea na shughuli zao za kila siku, hivyo kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa watoto na vijana wanaoishi na kisukari, insulin ni chachu ya matumaini na maisha marefu. Kwao, insulin inamaanisha nafasi ya kuishi maisha ya kawaida, kuhudhuria shule na kufikia ndoto zao bila vizuizi vya kiafya.

Serikali zinapaswa kushirikiana na mashirika ya kimataifa, sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kupunguza gharama za uzalishaji na usambazaji wa insulin.

Kampeni kama “Insulin kwa wote,” zinaweza kusaidia kuhamasisha hatua za pamoja katika ngazi ya kimataifa.

Serikali zinaweza kuweka sera za udhibiti wa bei za insulin ili kuhakikisha wagonjwa wanapata dawa kwa gharama nafuu. Hili linaweza kufanikishwa kupitia ruzuku au mipango maalumu ya bima ya afya inayolenga wagonjwa wa kisukari.

Kwa kuhakikisha kuwa insulin inapatikana kwa gharama nafuu kwa kila mgonjwa, inaweza kuokoa maisha na kusaidia wenye kisukari kuishi maisha bora.

Related Posts