Dar es Salaam. Ujauzito ni kipindi cha kipekee cha mabadiliko makubwa katika mwili wa mwanamke, kipindi hiki usalama wa mama na mtoto unapaswa kuzingatiwa kwa umakini zaidi ili kulinda afya za wawili hao.
Wakati wanawake wengi hujizatiti kuangalia lishe bora kipindi hiki cha ujauzito na namna ya kujipunguzia majukumu ili kupata muda wa kupumzika, masuala mengine kama matumizi ya bidhaa za urembo husahaulika, na kutozingatiwa.
Moja ya bidhaa hizo za urembo ni kucha za bandia pamoja na rangi za kucha, urembo huu umethibitishwa na madaktari na tafiti mbalimbali kuwa ni kati ya urembo wenye madhara kwa afya ya mjamzito kwa kusababisha matatizo kipindi cha kujifungua, kabla na huleta athari kwa watoto walio tumboni.
Rangi za kucha zinaweza kuwa na kemikali zinazomdhuru mjamzito, hasa akiwa mtumiaji wa muda mrefu na kwa kiasi kikubwa.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika nchini Uingereza mwaka 2020, asilimia 60 ya wajawazito hawafahamu madhara ya baadhi ya kemikali zilizopo kwenye rangi za kucha ambazo huwaathiri wao na watoto walio tumboni. Madhara ya mfumo wa neva pia yanatajwa. Toluene ambayo ni kemikali inayopatikana kwenye rangi ya kucha ni kati ya kemikali zinazoathiri mfumo wa neva wa mjamzito na kusababisha uchovu, kizunguzungu na matatizo ya mwili kama vile maumivu ya kichwa.
Kemikali ya formaldehyde inayopatikana kwenye rangi ya kucha nayo inahusishwa na matatizo ya afya kama saratani na madhara mengine ya mfumo wa hewa. Pia, mjamzito anapovuta hewa yenye kemikali, ana hatari ya kupata matatizo ya kupumua, kama vile pumu na hata ugumu wa kupumua.
Kemikali ya Phthalates, ambayo kazi yake kubwa ni kuhakikisha rangi inakaa kwa muda mrefu, tafiti zimeonyesha kuwa, kemikali hii inasababisha madhara kwenye mfumo wa uzazi na homoni, huku ikiongeza hatari ya kuharibika kwa mimba.
Baadhi ya tafiti za kitaalamu, ukiwamo ule wa Chuo Kikuu cha Yale wa mwaka 2021, uligundua wajawazito wanaotumia rangi za kucha zenye kemikali, wako hatarini kupata matatizo ya uzazi.
Ellen Sain anasema: “Nilipokuwa mjamzito nilipaka rangi ya pinki na kipimo hakikusoma,” anaeleza.
Kadhalika Elizabeth Paul anakiri kupata changamoto pindi alipotakiwa kupimwa kiwango cha hewa kupitia vidole. “Nilitakiwa kupimwa oksijeni nikiwa nimepaka rangi za kucha, ilishindikana, mwisho ikabidi kidole kimoja kifutwe rangi ili kupata majibu ya kipimo wakati wa kujifungua,” anasema Elizabeth.
Mtaalamu wa afya, Paul Masua anasema wakati mjamzito anaenda kujifungua mara nyingi hupimwa kipimo cha oksijeni, hasa akitakiwa kujifungua kwa njia ya upasuaji.
“Kipimo kinachoitwa pulse oximeter, kina kazi ya kupima kiwango cha oksijeni kwenye damu,” anaeleza.
Anasema, kuna rangi ambazo ukipaka kwenye kucha, kipimo hicho husoma tofauti na inavyotakiwa au kutoa majibu ya uwongo tofauti na uhalisia.
“Rangi nyeusi, bluu, kijani na brown ndizo zinazoongoza kwa kuficha kiwango cha oksijeni na kutoa majibu ya uongo,” anasema.
Anasema, hali hiyo husababisha mjamzito kupewa matibabu yasiyo sahihi, kwa kuongezea kiwango cha oksijeni au kuona kiwango kiko sahihi na kumbe mama huyo anahitaji msaada wa haraka wa kuongezea kiwango cha oksijeni mwilini.
Urembo mwingine wenye madhara ni hina, kucha ndefu, uchafu chini ya kidole na kucha bandia zinaweza kukusababishia kipimo kitoe majibu ya uongo.
Masua anasema rangi za kucha ambazo wanawake wengi hupaka zina kemikali ya acrylates ambayo husababishia wanawake wengi kupata mzio kutokana na kemikali hiyo.
Aidha, Dk Masua anasema rangi za kucha zinatengenezwa na aina tatu za kemikali ambazo huipa rangi harufu. Anasema ni busara rangi hizi zipakwe mahali penye hewa ya kutosha.
“Ni vyema mtumiaji wa rangi hizi asome maelekezo yaliyopo kwenye chupa ya rangi na ahakikishe hakuna kemikali hizo,” anasema.
Dk Masua anasema kipimo cha hewa safi kimetengenezwa kujua kiasi cha hewa kilichopo mwilini kwa kupitia mionzi yake ambapo baadhi ya rangi zinapopakwa hushindwa kuruhusu mionzi hiyo kufanya kazi. “Rangi nyekundu, buluu, kijani na kijivu haziruhusu mionzi kupenya na kutoa taarifa sahihi,” anaeleza. Anasema uwepo wa rangi hiyo kwenye kucha mara nyingi huleta majibu ya uwongo kwa kusoma kiwango cha hewa kuwa chini ya 95 kama ilivyo kawaida. “Majibu haya humfanya daktari kushindwa kujua taarifa sahihi za mgonjwa na hata kutoa majibu yasiyo sahihi,” anaeleza.
Kwa mujibu wa tafiti za Centers for Disease Control and Prevention (CDC) na Environmental Protection Agency (EPA) ya mwaka 2000 mpaka 2010, rangi za kucha zinaweza kuathiri mfumo wa homoni kwa mtoto, na kisha kuharibu maendeleo ya ukuaji wa ubongo wake. Katika utafiti huo, vipimo vilionesha uwepo wa kiwango kikubwa cha kemikali ya phthalates, kwenye mkojo wa mjamzito, na baada ya mtoto kuzaliwa pia aligundulika kuwa na matatizo katika tumbo lake la uzazi.
Tafiti hizo ziliweka wazi kuwa kemikali ya phthalates inaweza kuathiri maendeleo ya viungo vya uzazi vya watoto wa kike na watoto wa kiume kwa uchache. Athari nyingine za rangi ya kucha, ni saratani kwa mtoto, baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa baadhi ya kemikali zinazotumika kwenye rangi za kucha, zinaweza kusababisha saratani mbalimbali kwa watoto waliozaliwa kutoka kwa wanawake, waliotumia bidhaa hizo kipindi cha ujauzito.
Kadhalika, tafiti za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2017 na 2018, zinaonyesha uhusiano kati ya matumizi ya rangi za kucha zilizo na kemikali hatarishi, na kuzaliwa kwa watoto wenye matatizo ya kimwili na kiakili.