• Mwanasheria Mkuu wa Serikali asisitiza kuendelea kusogeza huduma karibu na Wananchi
Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali limekutana na kufanya kikao kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yatakayosaidia kurahisisha utendaji kazi na kutoa huduma bora zaidi za kisheria kwa wananchi.
Kikao hicho kimefanyika Januari 24, 2025 katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani, Pwani kwa kuwashirikisha wajumbe kutoka Divisheni, Vitengo na wajumbe wa TUGHE kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akizungumza wakati wa kikao cha Baraza hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe, Hamza S. Johari, amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi.
“Tumekutana kwenye kikao hiki cha Baraza na kupitia kwa pamoja changamoto zetu hasa suala la mafunzo kwa Mawakili wetu, wapate mafunzo katika kiwango kinachohitajika, na namna tunavyoweza kutumia TEHAMA hususan mfumo wetu wa OAG – MIS katika kuboresha utoaji wa huduma zetu.” amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa ni wazi kuwa mwaka uliopita Ofisi ya Mwanasheri Mkuu wa Serikali wamefanya vizuri katika eneo la utoaji wa huduma za ushauri wa kisheria ikiwemo uanzishwaji wa Kliniki za Ushauri wa Kisheria ambazo zimeendelea kutolewa bure kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kwa mwaka uliopita tumeweza kuanzisha Kliniki za Kisheria tukiwa na lengo la kusogeza huduma za kisheria kwa wananchi katika maeneo yao wanayoishi, na hivi sasa huduma hii tunaendelea kuitoa kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro”. Amesema Mhe. Johari
Kwa upande wake Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Maswi, ameipongeza ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa namna ambavyo wamekuwa wakitekeleza majukumu yao, sambamba na kuitisha kikao cha Baraza la Wafanyakazi kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ofisi hiyo.
Katika hatua nyingine Bw. Maswi ametoa wito kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa mafunzo kuhusu Upekuzi wa Mikataba kwa Mawakili wa Serikali ili kuhakikisha wanaendelea kusimamia vizuri mikataba ya Serikali kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Wito wangu kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni kuendelea kutoa mafunzo ya upekuzi wa Mikataba kwa Mawakili wa Serikali ili kuendelea kuboresha utendaji kazi wa Mawakili na Wanasheria wetu katika kusimamia Mikataba mbalimbali ambayo ina maslahi mapana kwa nchi.” Amesema Bw. Maswi.
Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel Maneno, amesema katika kipindi cha mwaka 2024/2025 Jumla ya mikataba 1,799 ilifanyiwa upekuzi ambapo kati ya hiyo mikataba 1,639 ya manunuzi,120 imehusu fedha,mkataba (1) kuhusu Maliasili na 39 ni ya ushirikiano wa Kimataifa.
Nae Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Zella Rwemanyira Ametoa rai kwa watumishi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuendana na dhana ya Weledi na Ubora.
“Natoa rai kwa Watumishi wenzangu wa Ofisi ya Mwanasheria kuendelea kuchapa kazi kwa bidi ili tuendane na dhana ya Weledi na Ubora.” Amesema Bi. Zella.