Dodoma. Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema endapo kilimo kingeheshimika kama ilivyo kwa Mwenge wa Uhuru, umasikini Tanzania ungeondoka.
Mbali na hilo, ameeleza kusikitishwa kwa Kituo cha Mafunzo kwa Wakulima mkoani Iringa (Ward resource center) kugeuzwa nyumba ya kulala wageni.
Bashe ameyasema hayo leo Ijumaa, Januari 25, 2025 wakati wa hafla ya kutia saini makubaliano na wakurugenzi wa halmashauri 19 nchi juu ya usimamizi, uendeshaji na matunzo ya skimu za umwagiliaji.
Makubaliano hayo yamefanywa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Vyama vya Umwagiliaji (NIRC), kupitia mradi wa Mfumo Himilivu ya Chakula Tanzania (TFSRP).
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Bashe amesema inawezekana wakurugenzi nchini hawajawatembelea wakulima kwa kuwa wako katika maandalizi ya kupokea Mwenge wa Uhuru.
“Siku tukiheshimu kilimo cha nchi hii kama tunavyoheshimu Mwenge basi tutaondoa umasikini,” amesema Bashe ambaye pia mbunge wa Nzega.
Pia amesema alikuwa Tanga akakutana na gari la Wizara ya Kilimo ambalo limeondolewa stika na kutumika kwa ajili masuala ya elimu, jambo ambalo amesema hakuku na sababu ya kufanya hivyo.
Amesema Tanzania tatizo sio wakulima bali ni watumishi wa Serikali ambao matatizo yanaanzia kwao, jambo ambalo linamfanya wakati mwingine kudhani wanafurahia matatizo ya sekta hiyo.
“Kwa sababu naamini matatizo yanatuandalia mikutano mingi ya kukutana na tutakuwa tunapata sana vikao vya posho, vikao vya kupembua taarifa na kuchunguza taarifa. Kuna mabadiliko ya tabianchi jamani. Zambia mmewaona na Malawi mwaka jana mmewasikia,” amesema.
“Hebu fikirieni siku ambayo hakuna mvua za kutosha tutakula nini, hakuna mazao, ushuru wenu wa mazao unaanguka. Si ndio jamani, mnaanza kuwakopa na madiwani, vita inaanza kati ya mkurugenzi na madiwani,” ametahadharisha.
Aidha, Bashe amemtaka mkurugenzi wa NIRC kuwaandikia barua wakurugenzi wote kuwaeleza kwenye halmashauri zao kuna miradi gani ambao unatekelezwa na kuwafanya mameneja wao kuripoti kwa wakurugenzi kwa kila mradi wanaofanya.
Amesema sasa hivi ukienda katika vituo vya mafunzo kwa wakulima na wafugaji vilivyoko katika kata unakuta vimefungwa vikiliwa na mchwa.
Amehoji kwa nini wakurugenzi wa halmashauri hawana maofisa kilimo kata ambao watahusika na ukusanyaji wa taarifa za kilimo kama ilivyo kwenye sekta nyingine.
“Unakuta yale majengo yamegeuka kuwa mahakama, mengine ofisi za watendaji. Niwapeni mfano Iringa, hapo nimeenda kutembelea juzi tumekuta jengo limegeuka guest house (nyumba ya kulala wageni),” amesema.
Amesema walipoijenga waliikabidhi kwa halmashauri, ina vyumba 24, ina vitanda na eneo la kilimo, lengo likiwa ni kuwachukua wakulima mahali pengine kwenda kuwafanyia mafunzo katika eneo moja.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mdolwa amesema wamekutana na wakurugenzi wa halmashauri 19, kati ya 23, ambazo wanaenda kufanya nao kazi katika mradi wa P for R ambao fedha zake za utekelezaji zinatoka Benki ya Dunia.
Amesema ni mradi wa miaka mitano ambapo lengo lake ni kurekebisha maeneo ya kilimo ili kuhakikisha skimu za wakulima wadogo wadogo zilizojengwa zamani ama kienyeji zinawekewa mifumo sahihi ziweze kuzalisha.
Mndolwa amesema pia katika mradi huo wa miaka nane, watakwenda kuchimba visima zaidi ya 56 nchi nzima na kuwa wanatarajia magari kwa ajili ya uchimbaji wa visima watayapokea Machi mwaka huu.
Mndolwa amesema mradi huo ambao unatarajiwa kuwanufaisha watu milioni 1.8 na utagharimu Dola za Marekani 300 milioni.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Stephen Katemba amesema kumekuwa na miradi mingi ya kilimo lakini usimamizi wa moja kwa moja umekuwa ukifanyika ndani ya Wizara ya Kilimo.
“Tafsiri yake mimi nikiwa msimamizi wa maendeleo katika halmashauri yangu, naona kweli mradi upo kwenye halmashauri yangu, lakini katika shughuli zangu za kawaida katika upimwaji wangu kwa sasa unaona miradi ya kilimo haijawekwa katika utaratibu wa upimaji,” amesema.
“Tafsiri yake ninapoangalia shughuli zangu wakati wa utekelezaji wake lazima nianze kwanza na vile ninavyopimwa navyo halafu vile vingine nachukulia kama sehemu ya ziada kwa sababu usimamizi wake uko chini ya Wizara ya Kilimo,” amesema.