Baraza la vyama vya mpira wa miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) limetangaza kuwa rais wake Wallace Karia ndio atakuwa mgombea pekee wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) katika uchaguzi mkuu wake utakaofanyika Machi Mwaka huu.
Hiyo ni kufuatia kujiondoa kwa rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (Fufa), Moses Magogo katika kinyang’anyiro hicho.
Taarifa iliyotolewa na Cecafa leo imeeleza kuwa Karia ndio mgombea pekee wa kuwania nafasi ya kuiwakilisha kanda hiyo katika kamati ya utendaji ya Caf.
Lakini pia Cecafa imetangaza kumuunga mkono rais wa shirikisho la mpira wa miguu Djibouti, Souleiman Waberi anayewania nafasi ya ujumbe katika baraza la shirikisho la mpira wa miguu duniani (Fifa).
“Wajumbe wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) wamekubali kumuunga mkono Souleiman Hassan Waberi kwa nafasi ya Baraza la FIFA katika mchezo ujao.
Uchaguzi wa CAF umepangwa kufanyika Machi 2025.
“Wanachama wa CECAFA walifanya azimio la kumuunga mkono Waberi wakati wa Mkutano Mkuu wa Kawaida wa CECAFA uliofanyika Januari 22, 2025 katika Hoteli ya Imperial Plaza huko Juba, Sudan Kusini.
“Wallace Karia, Rais wa CECAFA alisema tangu Kanda hiyo haijawahi kuwa na mwanachama kwenye
Baraza la FIFA, Kanda nzima imeamua kumuunga mkono Waberi ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Soka la Djibouti,” ilisema taarifa hiyo.
Cecafa imefafanua pia kuwa, “katika Bunge hilo Rais wa Shirikisho la Vyama vya Soka Uganda (FUFA), Hassim Moses Magogo alitangaza kwa moyo wa kindugu kwamba hataendelea na kinyang’anyiro chake cha kuwania nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na kumwachia Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania. (TFF), Karia kwa nafasi hiyo.”
Ikiwa atafanikiwa kuingia katika kamati ya utendaji ya Caf, Karia atakuwa Mtanzania wa pili kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Caf kwa kuchaguliwa, wa kwanza akiwa ni Leodgar Tenga.