Dabo afichua siri za mastaa kutoka Bongo

KOCHA wa zamani Azam FC, Youssouf Dabo ameeleza sababu za kuwavuta mastaa wa Bongo kwenda katika klabu anayoinoa kwa sasa ya AS Vita ya DR Congo.

Dabo ambaye alitimka Azam mwanzoni mwa msimu huu na katika dirisha hili dogo akiwa katika kikosi hicho amechukua baadhi ya wachezaji wazawa na kuwavuta katika kikosi hicho.

AS Vita imemchukua kiungo wa zamani wa Coastal Union, Denis Modzaka na mshambuliaji wa Mashujaa, Ismail Mgunda.

Akizungumza na Mwanaspoti Dabo, alisema uamuzi wa kuwachukua wachezaji wa Kitanzania kuwapeleka AS Vita, ni kuamini vipaji vyao na juhudi baada ya kuwaona wakati anafanya kazi Azam.

Alisema kuwa asilimia kubwa ya wachezaji aliokuwa anakutana nao kwenye mechi ambao walikuwa wanampa ugumu ni Watanzania ingawa wa kigeni wapo ambao walikuwa bora kushinda Watanzania.

“Wachezaji niliowachukua watakuwa mabalozi wazuri au wabaya, kwa kuonyesha njia ya imani kwa kuwafungulia milango wengine au nao kuwanyima fursa wenzao endapo hawatafanya vibaya. “Wakati nipo Tanzania niliona uwezo wao na nilipopata nafasi ya kuchagua basi niliwakumbuka na kuona kuwa wanaweza kuongeza kitu katika kikosi changu cha sasa,” alisema

Kiungo Modzaka alifunga bao moja msimu uliopita akiwa na Coastal Union, huku Mgunda akiwa na mawili katika duru la kwanza ya Ligi Kuu akiwa Mashujaa.

Related Posts