Mwanza. Baada ya wananchi mikoa ya kanda ya Ziwa na nchi jirani kutumia saa mbili kusubiria kivuko cha Mv Mwanza na MV Misungwi kwenda kati ya Kigongo- Busisi, sasa kuanzia mwezi ujao watatumia dakika tano hadi 15 wakipita katika daraja jipya la JPM kwa kutumia miguu au gari.
Matumaini ya kutumia dakika tano kuvuka katika eneo hilo, yametokana na ujenzi wa daraja la JPM kufikisha asilimia 96.4 za ujenzi wake, ambapo mwezi ujao litaanza kufanya kazi ili kuleta ahueni kwa wananchi wa Misungwi, Sengerema na mikoa mbalimbali ikiwemo ya Kagera na Geita na mataifa jirani.
Ujenzi wa daraja hilo, maarufu Kigongo- Busisi ambalo litakuwa la sita kwa ukubwa barani Afrika ulianza Februari 25, 2020, utaongeza urahisi katika shughuli tofauti hususani za uchukuzi kati ya Mwanza na maeneo mengine yaliounganishwa na jiji hilo la pili kwa ukubwa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Januari 24, 2025 muda mfupi baada ya kukagua mradi huo wenye thamani ya Sh 669 bilioni, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema maendeleo ya ujenzi huo yanakwenda vizuri, akiwapongeza wakandarasi wanaotekeleza mradi huo.
” Ujenzi wa daraja hili umefikia asilimia 96.4 kuelekea mwishoni, hongereni sana, jambo la pili wakati Rais Samia Suluhu Hassan anashika madaraka ujenzi ulikuwa asilimia 25,wakati ukivuka na kivuko nguzo hazikuwa zikionekana leo daraja limesimama.
“Wakati Serikali ililipa Sh150 bilioni,lakini habari njema hadi leo tunavyozungumza mkandarasi ameshalipwa takribani Sh 611 bilioni zimeshatolewa.Daraja hili lina kilomita tatu ndiyo refu katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema Ulega.
Waziri Ulega amesema kukamilika kwa daraja hilo litawezesha Watanzania wanaotumia saa mbili kusubiri kivuko na kuvuka kwenda nga’mbo ya pili, sasa watatumia dakika tano hadi 10.
Kwa mujibu wa Ulega, maelekezo ya Rais Samia ujenzi wa daraja hilo ukamilike Februari mwisho au Machi mwanzoni ili kutoa fursa kwa Watanzania hasa wananchi wa Mwanza na Geita kulitumia.
“Matumaini yetu siyo siku nyingi zijazo tutaanza kulitumia, kwa sababu tupo katika hatua za mwisho za ukamilishaji. Jana wakati nipo njiani nakuja Mwanza Serikali ilitoa Sh 16 bilioni kwa ajili ya mkandarasi kwa ajili ya kumalizia ujenzi huu,” amesema Ulega.
Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Abdulkarim Majuto amesema kwa sasa wapo katika za umaliziaji wa kazi mbalimbali ikiwemo kingo kwa ajili ya usalama kwa waenda kwa miguu na magari.
“Uwekaji wa lami, ujenzi wa barabara katika njia za kuingilia darajani, kimsingi tunakwenda vizuri na tunaishukuru Serikali kwa ushirikiano,” amesema Majuto.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amesema wananchi wa mkoa wanafarijia kwa namna anavyosimamia vyema sekta ya ujenzi kwa kufanya ziara katika mikoa mbalimbali kukagua mienendo ya ujenzi wa barabara.
“Miongoni mwa changamoto kubwa ndani ya mkoa wa Geita ni barabara hii hasa katika eneo la Kigongo- Busisi. Tunaamini kushamiri kwa shughuli za uchumi za mkoa wa Geita utachochewa kwa kiwango kikubwa endapo daraja hili litakamilika.
“Leo tunashuhudia tupo zaidi ya asilimia 96, ndani ya muda mchache wananchi wa Geita, Mwanza wataweza kutembea bila ya kuwa na shida yoyote na wigo wa shughuli za uchumi utaongezeka,” amesema Shigela.
Daraja hilo litakapokamilika, litakuwa refu kuliko yote katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, litakuwa na njia mbili za magari zenye upana wa mita saba kila upande, njia ya waenda kwa miguu yenye upana wa mita 2.5 kila upande, maegesho ya dharura yenye upana wa mita 2.5 kila upande na njia ya waenda kwa miguu yenye upana wa mita 2.5.
Daraja la JPM litakuwa la sita kwa urefu katika Bara la Afrika likiwa na urefu wa kilomita 3, upana wa mita 28.45 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66.
Kwenye daraja hilo lililopewa jina la JPM kama sehemu ya kutambua, kuenzi na kumbukumbu Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli aliyeasisi wazo na kuanza utekelezaji wa mradi huo aliouacha kwa asilimia 25 ya ujenzi, kuna nguzo za msingi 804, vitako vya nguzo za madaraja 65, nguzo 64 na nguzo za mlalo 806.