Dk Slaa anavyosota mahabusu | Mwananchi

Dar es Salaam. Hatima ya mvutano kuhusu uhalali wa kesi ya jinai inayomkabili mwanasiasa mkongwe, Dk Wilbroad Slaa itajulikana Jumatatu, Januari 28,2025, Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi wa maombi ya mapitio alilolifungua mahakamani hapo.

Mahakama hiyo imepanga kutoa uamuzi huo Jumatatu baada ya kukamilisha usikilizwaji wa shauri hilo leo Ijumaa, Januari 24, 2025, mbele ya Jaji Anold Kirekino.

Dk Slaa aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anakabiliwa na kesi ya jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar e Salaam, akidaiwa kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii, kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao.

Mgombea huyo wa urais mwaka 2010, alipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa shtaka hilo, Januari 10, akidaiwa kutenda kosa hilo, Januari 9, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, kupitia jopo la mawakili wake amefungua mashauri mawili ya maombi ya Jinai Mahakama Kuu, chini ya hati ya dharura, akihoji uhalali wa shtaka linalomkabili katika Mahakama ya Kisutu.

Mwanasiasa mkongwe, Dk Wilbroad Slaa akiongozwa na askari Magereza kutoka mahakamani baada ya shauri lake la maombi ya mapitio kuhusu uhalali wa kesi inayomkabili katika Mahakama ya Kisutu kusikilizwa leo Januari 24, 2025 katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Katika shauri hilo la maombi ya jinai namba 1688/2025, Dk Slaa anaiomba mahakama iitishe kumbukumbu (mwenendo) wa kesi ya msingi kujiridhisha na usahihi, uhalali utaratibu wa hoja zozote au amri iliyorekodiwa au kutolewa na Mahakama hiyo mwenendo huo.

Shauri hilo aliungwa mkono na kiapo cha binti yake Dk Slaa, Emiliana Wilbroad Slaa, akieleza kuwa upelelezi wa kesi ya msingi unaomkabili mwombaji (Dk Slaa) haujakamilika na kwamba anaendelea kupata hasara ya kukosa uhuru wake kwa kiwango kisichoweza kufidiwa.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, Wakili Peter Madeleka ameieleza mahakama kuwa kesi inayomkabili Dk Slaa ni batili kwa kuwa imefunguliwa kabla ya upelelezi kukamilika, kinyume cha matakwa ya sheria.

Amesema kuwa kifungu cha 131A (1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA) kama ilivyorekebishwa mwaka 2022, kimepiga marufuku mashauri kupelekwa mahakamani kabla ya upelelezi kukamilika, isipokuwa kwa makosa makubwa.

Amebainisha kuwa shtaka linalomkabili mteja wao halimo katika makosa makubwa yaliyotajwa chini ya kifungu kidogo cha (4) cha sheria hiyo.

Wakili Madeleka amedai katika kufungua kesi hiyo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) amekiuka matakwa ya Katiba inayomtaka kufungua mashtaka kwa nia ya kutenda haki na kwamba kinyume chake ni kumkomoa mtu.

Amedai kuwa Mahakama ikiwa chombo cha kutoa haki chini ya Ibara 107A ya Katiba isingetarajiwa mteja wao kuwa mahakamani mpaka sasa na kwamba kesi hiyo kuendelea kuwepo ni maelekezo ya kumtesa.

Wakili Madeleka amedai kuwa hati yoyote ya mashtaka inayoingizwa mahakamani kinyume cha sheria maana yake haibainishi mashtaka na chini ya kifungu cha 129 CPA, hakimu ana mamlaka ya kuikataa.

Mwanasiasa mkongwe, Dk Wilbroad Slaa akitoka kizimbani Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, huku akiwapungua mkono watu waliojitokeza mahamani hapo kusikiliza shauri la maombi yake kuhusu uhalali wa kesi inayomkabili katika Mahakama ya Kisutu.

Hivyo ameiomba Mahakama Kuu ione kwamba kinachoendelea katika kesi hiyo mpaka sasa ni batili na ifute mashtaka na imwachie huru.

Akijibu hoja hizo, kiongozi wa Jopo la mawakili wa Serikali, Nassoro Katuga pamoja na mambo mengine amedai kuwa Mahakama Kuu si mahali sahihi kuwasilisha malalamiko dhidi ya hati ya mashtaka kwa kesi iliyoko Mahakama ya Kisutu.

Amefafanua kuwa kuhoji uhalali wa mashtaka kunagusa mamlaka ya Mahakama kusikiliza kesi husika na kwamba mahakama hiyo ya chini yenyewe ndio ina mamlaka ya kusikiliza na kuamua malalamiko hayo.

“Hivyo, huwezi kulalamikia mamlaka ya mahakama ya chini kwenye mahakama ya juu, kabla ya kupelekea malalamiko hayo mahakama ya chini na kuieleza kuwa haina mamlaka, isipokuwa tu kama kuna amri iliyotolewa na mahakama ya chini,” amedai wakili Katuga na kusisitiza:

“Lakini pia huwezi kuhoji uhalali wa mashtaka kwa njia ya mapitio isipokuwa kama kuna amri iliyotolewa,” amedai.

Hata hivyo Wakili Katuga amedai kuwa hoja hii walishaiibua Mahakama ya Kisutu, kusikilizwa na uamuzi haujatolewa.

Hivyo Wakili Katuga amedai kuwa katika shauri hilo hakuna jambo ambalo linaifanya Mahakama Kuu iitishe mwenendo wa Mahakama ya Kisutu na akaiomba mahakama ilitupilie mbali shauri hilo.

Hata hivyo, Wakili Madeleka amesema wanachokilalamikia ni kuwa wanaamini kuwa mwenendo wa kesi hiyo una kasoro kutokana na kuendelea bila upelelezi kukamilika na kwamba wajibu maombi (mawakili) hawajasema kifungu gani cha sheria ambacho kinaizuia Mahakama kufanya wanachokiomba.

Jaji Kirekiano baada ya kusikiliza hoja zote ameahirisha shauri hilo mpaka Jumatatu kwa ajili ya uamuzi.

Katika kesi msingi, Dk Slaa anatuhumiwa kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa X zamani Twitter, kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Anadaiwa kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X katika akaunti ya Maria Sarungi @MariaSTsehai aliandika ujumbe uliosomeka kuwa:

“Wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung’unya … na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa ni dhahiri atatoa pesa…hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake”

Pia anadaiwa kuwa aliandika katika akaunti maneno yalisomeka kama;   “Samia toka muda mrefu hahangaikii tena maendeleo ya nchi anahangaikia namna ya kurudi Ikulu, na namna yake ya kurudi Ikulu ni kwa njia hizo kama kumsaidia mtu kama Mbowe.”

Related Posts