Familia ya mtoto aliyeibwa Kibaha yazidi kumlilia Rais Samia

Kibaha. Siku 10 baada ya mtoto wa miezi saba kuibwa na watu wasiojulikana, familia ya mtoto huyo bado ina matumaini kuwa atapatikana salama.

Wakiwa kwenye majonzi, familia hiyo imeendelea kumlilia Rais Samia Suluhu Hassan wakimuomba asaidie kupatikana kwa mtoto huyo. 

Mtoto huyo aitwaye Merisiana Sostenes alichukuliwa  Januari 15, 2025, akiwa nyumbani kwao Kibaha kwa Mfipa Mkoa wa Pwani na inadaiwa kuwa waliomchukua mbali na kuondoka naye, waliiba fedha, simu za mkononi na gari.

Baba wa mtoto huyo, Melkisedeck Sostenes amesema wakati wa tukio saa 12 asubuhi, yeye alikuwa ameenda nje kulisha kuku.

Akizungumza leo Januari 24,2025 wakati wa kupokea faraja kutoka kwa Umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha na Baraza la Wazee wa (CCM ) Mkoa wa Pwani, Sosthenes amesema ana imani na uwezo wa Serikali katika kutatua suala hili.

“Tunamuomba Rais Samia atusaidie, tunaamini anasikia maombi yetu na tunajua ana huruma,” amesema Sostenes baba wa mtoto huyo na kuongeza kuwa kuwa nguvu ya serikali ni kubwa ana amani watatekeleza wajibu wao na kuwapata watuhumiwa hao.

Katika ziara hiyo, Katibu wa UWT Kibaha, Secilia Ndallu amewapa familia hiyo pole na kusema hali hiyo itafikia mwisho kwani aliyeibiwa ni mtoto mchanga ambaye ni malaika asiyekuwa na hatia.

Katibu wa Baraza la Wazee wa (CCM) Mkoa wa Pwani, Abdallah Mdimu, amewatia moyo wazazi wa mtoto huyo akisema Serikali inafanya kazi bila kuchoka kuhakikisha tatizo hilo linapata ufumbuzi.

“Mungu yupo, msiwe na wasiwasi. Serikali inafanya kazi usiku na mchana, naamini ipo siku mtoto atapatikana akiwa salama,” amesema Mdimu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema hatua kali zitachukuliwa watakapowakamata wahusika.

“Tunaendelea na ufuatiliaji wa tukio hili. Tutatoa taarifa uchunguzi utakapokamilika,” amesema Kamanda Morcase.

Related Posts