Marekani. Jaji wa Mahakama ya Wilaya nchini Marekani, John Coughenour amesema amri ya Rais Donald Trump ya kusitisha haki ya uraia wa kuzaliwa kwa wahamiaji nchini humo, ni kinyume na katiba na ametoa agizo la muda la kuizuia utekelezaji wake.
Trump alitaka watoto wanaozaliwa na wahamiaji walioko kinyume cha sheria au kwa viza ya muda wasiunganishwe na uraia wa Marekani, lakini jaji ameona amri hiyo ni kinyume cha Katiba.
Majimbo manne – Washington, Arizona, Illinois na Oregon – yamepinga amri hiyo, yakisema ingeleta madhara makubwa kwa raia wa Marekani.
Kuna ripoti kwamba utawala wa Trump ulikuwa ukipanga kutekeleza amri hiyo kwa kudhibiti nyaraka, kama vile pasipoti, kutoka kwa watu wanaodhaniwa kuwa hawastahili uraia.
Jaji amekubaliana nao, akitoa agizo la kuzuia utekelezaji wa amri hiyo kwa siku 14 hadi kesi hiyo itakaposhughulikiwa zaidi.
Trump alikusudia kubadili sheria ya uraia iliyopo kwenye Marekebisho ya 14 ya Katiba, ambayo ingehitaji mabadiliko ya kisheria au maamuzi ya mahakama kuu.
Marekebisho ya 14, yaliyopitishwa mwaka 1868, yasema kuwa: “Watu wote waliozaliwa Marekani ni raia wa Marekani.”
Mawakili wa serikali wamesema wanapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, na kwamba wanatarajia kesi hiyo kufika mbele ya Mahakama Kuu ya Marekani.
Katika uamuzi wake Jaji Coughenour, ambaye aliteuliwa na Rais wa zamani wa chama cha Republican, Ronald Reagan, amesema amri hiyo ya Trump ni kinyume na katiba.
Trump alisaini amri hiyo Jumatatu, siku ya kwanza ya kurejea kwake madarakani kwa muhula wa pili, akielekeza taasisi za Serikali za Marekani kutotambua uraia wa watoto wanaozaliwa na wazazi ambao si raia wa nchi hiyo au wakazi wa kudumu wa kisheria.
Jaji Coughenour amehoji uwezo wa kisheria wa wanasheria wa utawala wa Trump kuunga mkono amri hiyo:
“Siwezi kuelewa jinsi mwanasheria mwenye uzoefu anaweza kusema amri hii ni ya kikatiba. Inashangaza akili yangu,” amesema.
“Nimekuwa jaji kwa zaidi ya miaka 40. Siwezi kukumbuka kesi nyingine yoyote ambayo masuala yake ni wazi kama hii. Hii ni amri iliyo wazi kuwa kinyume cha katiba,” ameongeza Jaji Coughenour.
Uamuzi wa Coughenour unazuia utekelezaji wa amri hiyo kwa siku 14, wakati Mahakama ikitarajiwa kusikiliza hoja za kuamua kama itaweka zuio la muda mrefu, Februari 6, mwaka huu.
Endelea kufuatilia Mwananchi.