Jeshi la Polisi Arusha lapewa pikipiki nyingine 20

Arusha. Kampuni ya Utalii ya Leopard Tours imetoa pikipiki 20 kwa Jeshi la Polisi ili kuimarisha usalama na kukuza sekta ya utalii mkoani Arusha.

Pikipiki hizo zimekabidhiwa leo Ijumaa Januari 24, 2025 kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ambaye amewashukuru wadau hao kwa kuendelea kulisaidia jeshi hilo.

Hii ni awamu ya pili kwa Kampuni hiyo ya utalii kutoa pikipiki kwa jeshi hilo, awamu ya kwanza walitoa pikipiki nyingine 20, Desemba 18, 2024. Pikipiki hizo zimefanya jeshi hilo mkoani humo kufikisha zaidi 100 zilizotolewa na mashirika mbalimbali ndani yam waka mmoja.

Makonda amelitaka Jeshi la Polisi kihakikisha linatumia pikipiki hizo katika kuimarisha ulinzi na usalama wa mkoa huo ili wananchi wafanye shughuli za kiuchumi bila kuwa na hofu.

“Kwa niaba ya wananchi na Serikali tunashukuru kwa msaada huu kwani licha ya kuwa kampuni ya utalii iliyoajiri vijana wetu wengi, umeona utoe sehemu ya faida kulisaidia jeshi letu la polisi, tutahakikisha mnafanya kazi za utalii usiku na mchana,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Zuher Fazal, amesema wametoa pikipiki hizo kusaidia Jeshi la Polisi kuimarisha usalama hasa ikizingatiwa mkoa wa Arusha ni kitovu cha utalii.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alishukuru kampuni hiyo kwa kulisaidia  jeshi hilo kwa vitendea kazi hivyo na kuwa vitawaongeza nguvu katika utekelezaji wa majukumu yake.

 “Kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, tunashukuru kwa msaada huu na niwahakikishie tutaishi kwenye ndoto za kuhakikisha mkoa unatengeneza fedha na atakayejitokeza katikati akitaka kuharibu, tutashughulika naye ili Arusha iendelee kuwa na amani,” amesema.

Related Posts