Kamati ya Bunge yaagiza uwanja wa ndege wa Msalato ukamilike Agosti

Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu ya Serikali (PAC), imeagiza Serikali kuhakikisha inakamilisha mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato jijini Dodoma ili uanze kutumika Agosti 2025.

Makamu Mwenyekiti wa PAC, Japhet Hasunga ameyasema hayo leo Januari 23, 2025 wakati kamati hiyo ilipotembea ujenzi wa uwanja huo.

Uwanja wa ndege wa Msalato, ni mradi mkubwa wa kimkakati unaolenga kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga nchini Tanzania.

Uwanja huu utakuwa wa kisasa, ukiwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa za kimataifa na za ndani, na utakuwa na vifaa vya kisasa vya usalama na huduma za abiria.

Eneo lake lipo kilomita 12 kaskazini mwa Dodoma, ukilenga kuchochea ukuaji wa kiuchumi, kibiashara na utalii katika mkoa huo na nchi nzima.

Hasunga amesema jukumu la PAC ni kuangalia fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya uwekezaji huo mkubwa, zinatumika ipasavyo na kuleta matunda ya yalikusudiwa.

“Tunaitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)  Ifikapo mwezi wa nane uwanja huu uwe umekamilika, tunataka Rais Samia Suluhu Hassan anapokuja kuapa na wale wanaokuja kushuhudia, wautumie uwanja huu,” amesema Hasunga ambaye ni mbunge wa Vwawa.

Wakala wa Ujenzi wa Barabara Tanzania (Tanroads) umeeleza kuwa eneo la uwanja huo lina ukubwa wa takribani hekta 4,500, ambalo litawezesha kuupanua uwanja huo itakapohitajika kufanya hivyo baadaye.

“Tulitaka kuona itakapofika Dodoma imepanuka imekuwa jiji kubwa, je, kuna nafasi ya kuongeza run way (njia ya kurukia) ya pili. Tayari wametuonyesha eneo lililotengwa kwa ajili hiyo na kuna phase (awamu) ya pili ambapo zinaweza kujengwa mbili na kuendelea,” amesema Hasunga.

Kwa mujibu wa Hasunga, Serikali pia imeweka mpango mkakati wa ujenzi, kuongeza eneo kwa ajili ya maduka makubwa, kumbi za mikutano na hoteli ambazo zitachagiza kuvua watalii na watu kutoka maeneo mbalimbali.

“Ambalo tunataka majibu ni kuwa baada ya Serikali imewekeza katika SGR, je, mpango ukoje baadaye kuhakikisha kuwa wanavuta line (njia) ya SGR kuja hadi katika uwanja huu, tunataka watu wawe na uhuru wa usafiri wanaotaka kutumia,” amesema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Matiko amesema kutokana na uwanja huo kuwa na eneo kubwa walitarajia kuona jengo la abiria lina ukubwa unaozidi wa lile la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

 “Lazima kama nchi kuhakikisha tunapanga bajeti kujenga kitu ambacho kinakaa muda mrefu pamoja na kwamba kuna viwanja duniani huwa wanaongeza kwa kadri ya muda, kwa jinsi tunavyotaka kuchechemua mji wa Dodoma lazima jengo liwe kubwa,” amesema.

Pia amesema wameona kuna barabara moja ya kuingilia katika uwanja huo, jambo ambalo litawafanya watu wengine wanaotaka kufika kwenye uwanja huo kuzunguka umbali mrefu kuufikia.

Hivyo, Matiko ameshauri Serikali iangalie namna wanavyoweza kuwa na njia mbili au tatu za kuingia kwenye uwanja huo, ili kuepusha yanayotokea JNIA.

“Kule Dar es Salaam ikitokea msafara wa kiongozi hata pikipiki huwezi kupita kufika Airport (uwanja wa ndege), hayo mambo hatuyataki kwa Dodoma. Tunapongeza kwa kazi inayoendelea, lakini tunawasihi umalizike kwa wakati,” ameongeza Matiko.

Mbunge wa Viti Maalumu Jacqueline Ngonyani amesema katika miradi mingi ambayo wameitembelea wamekutana na changamoto, lakini hali imekuwa tofauti kwenye mradi huo.

Mapema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta amesema mradi huo unatekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ya kiwanja kitajengwa kwa kiwango cha daraja la 4E.

Amesema kiwanja hicho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa aina ya Boeing 787-8 (Dreamliner) ambayo ina uwezo wa kubeba abiria 350.

Amesema Februari 2020 Serikali na Benki ya Afrika AfDB walitiliana saini mkataba wa mkopo kwa ajili ya ujenzi huo, wenye thamani ya Dola za Marekani 329.29 milioni.

“AfDB inachangia asilimia 100 kwenye malipo ya wakandarasi na mshauri mwelekezi huku Serikali ikilipa fidia na riba,” amesema.

Amesema sehemu ya kwanza ya mradi huo ambayo inahusisha ujenzi wa njia za kurukia ndege itakamilishwa Aprili 18, 2025 huku sehemu ya pili ya mradi huo inayohusisha majengo ikikamilika Julai, 2025.

Related Posts