Kobe 116 wa Tanzania waliokamtwa Thailand warudishwa

Dar es Salaam. Zaidi ya watoto mia moja wa kobe, wengi wao wakiwa wamekufa, wamerudishwa Tanzania kutoka Thailand, kama ushahidi katika kesi dhidi ya mtandao wa magendo ya wanyamapori.

Hayo yamebainishwa na Shirika la Polisi wa Kimataifa (Interpol) katika taarifa yake iliyotoka leo Ijumaa Januari 24, 2025 nchini Thailand.

Kobe hao 116 waligunduliwa wakiwa wamefichwa kwenye mizigo ya mwanamke raia wa Ukraine kwenye Uwanja wa Ndege wa Bangkok wa Suvarnabhumi zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Kati ya hao, 98 wamekufa lakini wote walikabidhiwa jana Alhamisi kwa ajili ya matumizi ya kesi za jinai, katika hafla iliyohudhuriwa na maofisa wa Thailand na Tanzania. Hakuna sababu zilizotolewa kuhusu vifo hivyo.

Wanyama hao wanajumuishwa kati ya spishi zilizo hatarini kutoweka duniani ikiwemo kobe aina ya pancake, kobe wenye miale na wale wakubwa aina ya aldabra. Aina zote zinalindwa chini ya Mkataba wa Biashara ya Kimataifa katika Viumbe vilivyo Hatarini Kutoweka (CITES).

Kwa kawaida kobe huondolewa porini kwa ajili ya kuuzwa kama wanyama ambao ni kivutio kwa watalii.

Kwa mujibu wa Interpol, jangili huyo alitoroka nchini Thailand lakini alifuatiliwa na kukamatwa nchini Bulgaria.

Kukamatwa kwake kulisaidia polisi kupata ramani ya mtandao mkubwa zaidi wa usafirishaji wa wanyamapori, na kusababisha kukamatwa kwa washukiwa wengine 14 katika operesheni iliyohusisha polisi wa Thailand, Tanzania na maofisa wa Interpol.

Kobe waliosalia watawekwa karantini na kutunzwa huku wataalamu wakitathmini kama wanaweza kurejeshwa katika makazi yao ya asili.

“Usafirishaji haramu wa wanyamapori ni tishio kubwa la kimataifa ambalo linavuruga mfumo wa ikolojia na kudhuru jamii, huku likitajirisha vikundi vya uhalifu vilivyopangwa,” amesema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Polisi wa Interpol, Cyril Gout.

Interpol ilikadiria mwaka 2023 kuwa soko haramu la bidhaa haramu za wanyamapori lina thamani ya hadi dola 20 bilioni (Sh50.9 trilioni) kwa mwaka.

“Uwindaji haramu na biashara haramu ya wanyamapori imekuwa eneo kubwa la shughuli za vikundi vya uhalifu uliopangwa na inahusishwa zaidi na vurugu za kutumia silaha na ufisadi na aina nyingine za uhalifu uliopangwa,” ilieleza Interpol.

Thailand inaendelea kuwa kitovu cha biashara hiyo. Mwezi Mei mwaka jana, takriban dazeni nne za kima na zaidi ya kobe 900 wanaotokea Madagasca walikamatwa katika jimbo la kusini la Chumporn baada ya kuvushwa kutoka Indonesia. Walirudishwa katika nchi yao mwishoni mwa mwaka jana.

Related Posts