Kocha Bares macho yote yapo hapa

SIKU chache baada ya ratiba ya ligi kufanyiwa marekebisho, kocha wa Mashujaa, Abdallah Mohamed ‘Bares’ amesema tayari ameanza kukiweka sawa kikosi chake huku akizitaja timu tatu za Azam FC, Yanga na Singida Black Stars kuwa lazima awe nazo makini kutokana na kukutana nazo mapema zikiwa ndiyo washindani wakubwa nafasi tano za juu.

Mashujaa ipo nafasi ya saba kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi 19 katika michezo 16 iliyocheza huku malengo yao ni kumaliza nafasi za juu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bares alisema ana ratiba ya kukutana na timu hizo tatu mapema mzunguko wa kwanza huku moja pekee ikiwa nyumbani kitu ambacho lazima wawe makini ili kufikia malengo.

“Ratiba nimeiona na tayari nimeanza kuifanyia kazi, sasa timu imeanza mazoezi ya gym baada ya mchangani na Jumatatu tunaingia mazoezi ya uwanjani rasmi, hii ni baada ya kurejesha hali ya utimamu kwa wachezaji ambao walikuwa mapumzikoni,” alisema na kuongeza.

“Ukitaka kuwa bora shindana na unaofukuzana nao, ili nitoboe kumaliza nafasi tano za juu lazima kuhakikisha napata pointi tatu kwa wanaoniongoza na sio kuangalia timu ambazo tayari nimezizidi, huwezi kuwa bingwa au mshindi wa pili kama unagawa pointi kwa wanaokuongoza, ndiyo maana nimetaja hizo timu.”

Akizungumzia ratiba kwa jumla, Bares alisema ni ngumu lakini wanajiandaa kwa ajili ya ushindani kutokana na timu kufanya maboresho dirisha dogo.

“Sio rahisi na kuzitaja timu hizo haina maana wapinzani wengine sitarajii changamoto kutoka kwao, najiandaa kwa ajili ya kumaliza ligi na timu zote ambazo bado sijamalizana nazo. Kuhusu kuzitaja zaidi Yanga, Azam na Singida Black Stars ni kwa sababu ratiba ya kukabiliana nao ipo karibu na ndio washindani ninaotamani kuona napata matokeo mazuri kutoka kwao,” alisema.

Ratiba inaonyesha ligi ikirejea Februari Mosi mwaka huu, mwezi huo pekee Mashujaa itacheza mechi sita dhidi ya Tanzania Prisons (Februari 6), Coastal Union (Februari 11), Azam (Februari 15), Pamba Jiji (Februari 19), Yanga (Februari 23) na Singida Black Stars (Februari 26).

Related Posts