Moshi. Shirika la Tmeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Kilimanjaro limekuja na mikakati minne itakayochochea upatikanaji wa huduma bora na kuondoa mitazamo hasi iliyojengeka kwa wananchi juu ya shirika hilo.
Mikakati hiyo ni pamoja na kubadilisha nguzo za umeme zilizooza na kuweka nyingine za zege, ili kuondoa changamoto ya ukatikaji wa umeme mara kwa mara, hasa kipindi cha mvua pamoja na kutatua matatizo ya wananchi ndani ya saa mbili tangu kuripotiwa.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kilimanjaro, Dotto Chacha wakati akizungumza na Mwananchi digital ofisini kwake, kuhusiana na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, hasa wakati wa mvua, ambapo amesema kwa sasa tatizo hilo litabaki kuwa historia.
Chacha ametaja mikakati mingine kuwa ni kutoa huduma za kuunganisha umeme ndani ya siku mbili kuanzia mteja alipoomba huduma na kulipia pamoja na kuhakikisha wanaoomba wanafanyika ukaguzi na wanapata huduma hiyo ndani ya siku moja bure.
“Tanesco Mkoa wa Kilimanjaro moja ya malengo yake makuu ni kubadilisha mitazamo hasi iliyojengeka kwa wateja wetu, kwa kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa sasa zinakuwa bora na kwa wakati,” amesema Chacha.
Ameongeza kuwa “Hii tumeichukua kama fursa kuweza kufanya kitu zaidi na kuondoa hayo malalamiko ya wananchi kwa kutengeneza malengo mahususi ya mkoa.
“Lakini la pili tumesema wale wateja wetu wote wanaohitaji umeme kwa maombi ya awali na wamekwishalipia huduma zao, ndani ya siku mbili tuhakikishe wote wameunganishiwa umeme, na wale wanaofika kwenye ofisi zetu au kupitia mifumo na mitandao kuomba kufanyiwa survey (ukaguzi) ndani ya Mkoa tumehakikisha inafanyika ndani ya siku moja na ni bure. Tunataka wananchi watambue Tanesco tupo kazini na kuondoa ile katika ya umeme,” amesema Chacha
Aidha amesema kuanzia Februari mosi mwaka huu, wamejipanga kuanza matengenezo makubwa ya miundombinu ya umeme ili kuepusha changamoto za kukatika kwa umeme wakati wa mvua za masika.
Amesema “Pia tumekuja na kaulimbiu ya fahari kwa mteja, kwani moja ya changamoto ambayo ilikuwa ikisababisha umeme kukatika mara kwa mara ni nguzo kuoza hivyo tukafikiri tutakapoanza kutumia nguzo za zege ambazo zinakaa muda mrefu tutaondokana na changamoto hii,” amesema.
Akizungumzia wizi wa miundombinu ya umeme, Chacha amesema imekuwa ni changamoto kubwa na sasa wameanzisha operesheni kubwa na wale watakaobainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Kumekuwa na changamoto ya wizi wa miundombinu ya umeme, kuna hujuma zinafanywa na baadhi ya watu wasio wazalendo, wanaiba miundombinu ya umeme kama transfoma, mita na nguzo na hili lipo maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro ambao tunahudumia wilaya nane za Kitanesco,” amesema Chacha
Wakizungumzia mikakati hiyo, baadhi ya wananchi mjini Moshi, wamesema mitazamo hasi juu ya Tanesco ilitokana na utolewaji wa huduma zisizoridhisha na kwamba huduma zikiboreshwa itafutika na kila mmoja kufurahia huduma.
“Kila mmoja anahitaji huduma bora, hivyo mtu ukienda Tanesco ukahudumiwa kwa haraka na kuondoka huwezi kulalamika utafurahia,” amesema Rose Mongi.
Naye Raheli Moiso amesema, “ukatikaji wa umeme umekuwa ni changamoto hapo kipindi cha nyuma, lakini tatizo hilo tumeona limepungua kwa sasa, tunahitaji waendelee kuboresha upatikanaji wa huduma na kuhakikisha zinapotokea changamoto za dharura na mwananchi kuripoti, utatuzi uwe wa haraka ili kurejesha huduma.”