Mambo yanayomsubiri Lissu Chadema | Mwananchi

Dar es Salaam. Siku tatu tangu Tundu Lissu kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wadau wa siasa wametaja mambo manne anayopaswa kuyasimamia kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, ikiwemo upatikanaji wa Tume huru ya uchaguzi kabla ya kariba ambayo upatikanaji wake ni mlolongo mrefu.

Suala lingine wanaloshauri ni kuwaunganisha wanachama, kuvutia makundi mengi ya wafanyabiashara, wakulima na wafugaji ndani ya chama hicho kwa kupaza sauti ya kero zao.

Pia kuweka ukomo wa nafasi za viti maalumu pamoja na kusimamia vyema fedha za chama na kuzishusha kwa viongozi wa ngazi ya tawi zitumike kujijenga chama kuanzia ngazi ya shina kama alivyoahidi.

Lissu alishinda nafasi ya uenyekiti Chadema Januari 22, 2025 na baada ya kutangazwa kushika wadhifa huo amesisitiza hatokuwa na ndimi mbili kwenye utumishi wake.

“Tumelipata tulilokuwa tukilitafuta, sasa tufanye kazi na kazi inaanza leo. Kuanzia leo, kesho na siku zinazofuata tunafanya kazi ya kuhakikisha tunajenga chama chetu,” amesema Lissu baada ya kutangazwa mshindi.


Lissu mwenyekiti mpya Chadema

Katika hotuba hiyo, Lissu amesema moja ya kazi watakazoanza nazo kwa sasa ni kuangazia rufaa zilizokatwa na watia nia wa ujumbe wa kamati kuu majina yao yalikatwa kwa sababu mbalimbali.

“Tutaanza na maumivu ya chinja chinja ya wagombea, tutasikiliza rufaa zao kama zina hoja tutawarudisha,” amesema.

Kila mwenye haki ya kugombea uongozi ni lazima apate nafasi hiyo. Lazima tuhakikishe watu wote wanatendewa haki, hatuwezi kudai haki kwa CCM wakati sisi wenyewe ndani hatutendeani haki,” amesema.

Akizungumza na mwananchi kwa njia ya simu leo  Ijumaa Januari 24, 2025, Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa, Dk Stephen Kimondo amesema imani ya wananchi wengi kwa Lissu ni yale aliyoyanadi kwamba atakwenda kuyatekeleza.

Moja ya jukumu la Lissu alilolitaja Dk Kimondo ni kuweka ukomo wa nafasi za viti maalumu na usimamizi bora wa fedha za chama na upatikanaji wake.

“Akasimamie fedha za chama na viongozi wa chini nao wazipate wakijenge chama kuanzia ngazi ya tawi hadi shina,” amesema.

Dk Kimondo amesema ushindi wa Lissu si tu umeleta matumaini ndani ya chama, bali hata nje kwani watu walivutiwa na kauli zake hata alipokuwa mgombea wa urais.

Mtaalamu huyo wa sayansi ya siasa amesema kuchaguliwa kwa Lissu kumekoleza  hamasa ya uchaguzi mkuu akisisitiza msimamo wa Chadema wa ‘No reform no Election’ umewasukuma wanachama kumtafuta mtu ambaye anaweza kusimamia kaulimbiu hiyo bila kuyumba.

“Kazi nyingine aliyonayo ni kuunganisha wanachama wake wote ili chama kiwe imara, ieleweke ni kawaida kutofautiana wakati wa kampeni, hayo ndio majukumu aliyonayo Lissu kwenye uongozi wake,” amesema.

Kwa upande wake Mchambuzi wa masuala ya siasa Buberwa Kaiza amesema jukumu alilonalo Lissu katika uongozi wake ni kukiongoza Chadema kushiriki uchaguzi na kuongoza dola.

“Pia chama kiliongozwa na mtu mmoja kwa muda mrefu, sasa ana jukumu la kuitengeneza chama mpya na kuwaleta wanachama pamoja na watu kuelewa falsafa yake,” amesema.

Jukumu lingine ni kuunganisha chama chake na makundi mbalimbali ya watu wakiwemo wafanyabiashara, wakulima na wafugaji ambao wana changamoto nyingi ambazo hawana eneo la kuzisemea.

“Ana jukumu la kuyafuata makundi haya na kuhakikisha sauti zao zinasikika na agenda zao kwa pamoja zinafanyiwa kazi, pia makundi haya yapate uwakilishi bungeni,” amesema.

Kwa upande wake aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari amesema Chadema chini ya uongozi wa Lissu na vyama vingine vya upinzani vinapaswa kuwa na msimamo wa pamoja wa kutoshiriki uchaguzi mkuu kama hakuna Tume huru ya uchaguzi.

“Ni muhimu wasiende kwenye uchaguzi bila Tume huru ya uchaguzi na wasidai Katiba kwa sababu wataingia kwenye mtego wa CCM, mchakato wake ni mrefu, kinachohitajika ni kubadili eneo linalohusiana na tume huru,” amesema.

Profesa Safari amesema kudai Katiba mpya wakati huu ni kuingia kwenye mtego wa CCM.

Jambo lingine analoshauri Profesa Safari, Chadema inapaswa kushinikiza urejeshwaji wa nyumba za Serikali zilizohodhiwa na baadhi ya viongozi wa umma.

“Kuna agenda ya rushwa na nchi hii ina rushwa kwa kiwango kikubwa, lakini tuna agenda mpya, kuna watu wamegawana nyumba za Serikali,” amesema.

Related Posts