Tanga. Serikali ya Mkoa wa Tanga imeanza kuchukua hatua kuangalia namna ya kuvifufua viwanda vikubwa vitatu vya Mbolea, Mbao na Chuma hatua ambayo inaweza kurejesha matumaini ya wananchi kwa kuongeza kipato, ajira na uchumi wa mkoa kuimarika.
Tayari mazungumzo yameanza kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na mwekezaji wa kiwanda cha Chuma ‘Steel Rolling Mills’ ambacho baada ya ubinafsishaji wa awali, kilifahamika kwa jina la Unique Steell Rolling Mill.
Ofisa Biashara, Viwanda na Uwekezaji wa Mkoa wa Tanga, Peter Lyoko anasema Serikali inakutanana na mwekezaji huyo ili kujua changamoto za ukosefu malighafi na huduma ya uzalishaji na usafirishaji chuma kwenda nchi jirani, ambazo zilitajwa kuwa ni kikwazo.
Pia lilionekana tatizo la ukosefu wa malighafi lakini sasa miundombinu imeimarishwa, ikiwano uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye Bandari ya Tanga.
“Kutokana na hali hiyo, changamoto hiyo kwa kiwanda cha chuma hivi sasa imetoweka, hivyo mwekezaji anapaswa kurejea kwenye uzalishaji wa bidhaa husika, suala ambalo pia litaiwezesha Serikali kukusanya mapato yake kama awali na kuleta tija kwa wananchi,” anasema Lyoko.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian akizumgumza katika hafla ya kuombea Taifa iliyofanyika Tanga Desemba 31, 2024, alisisitza kuwa ofisi yake inaendelea na mkakati wa kufufua viwanda ambavyo vilibinafsihwa na ambavyo vimekufa.
Aliwataka wawekezaji walioshindwa kuviendeleza wavirejeshe ili mkoa uweze kuchukua hatua stahiki kupata wengine wa kuvifufua na kuviendeleza.
Kuhusu Kiwanda cha kuzalisha mbao cha Sikh Saw Mills, Lyoko anasema Serikali imefanya juhudi kadhaa ikiwamo kukipeleka kwa Msajili wa Hazina na kwamba taratibu za kukitafutia mwekezaji mwingine zimeshafanyika.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa KItengo cha Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano katika Ofisi ya Msajii wa Hazina, Sabato Kosuri kiwanda hicho kimerejeshwa kwa mmiliki wake.
Wakati hayo yakielezwa kuhusu kufufuka viwanda hivyo vilivyowahi kuiing’arisha Tanga, inaonekana hakuna matumaini kabisa kwa iwanda cha mbolea kurejea katika hali yake ya awali ya kuweza kufanya uzalishaji kutokana na eneo lake kubadilishwa kabisa matumizi.
Hata hivyo, aliyewahi kuwa mfanyakazi wa kiwandha hicho kabla ya ubinafsishaji, Seif Abdallah (68), mahitaji ya mbolea bado ni makubwa kwa maana ya bidhaa hiyo kuhitajika kwa wakulima na wakazi wa Jiji la Tanga kupata ajira.
Katika kipindi ambacho kiwanda cha mbolea kilikuwa kikifanya kazi, wakulima hususani wale wa Mkoa wa Tanga waliweza kupata bidhaa husika kwa karibu na maeneo yao na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji.
Akizungumizia kiwanda cha Mbolea, Mwaimu anasema bidhaa hiyo mbali na kuwa na umuhimu mkubwa kwa wazi wa Mkoa wa Tanga lakini pia ilikuwa ikisafirishwa kwenda mikoa jirani kutokana na umuhimu wake kwenye sekta ya Kilimo, kwa mujibu wa Kiama Mwaimu,. mdau wa maendeleo na mchambuzi wa masuala ya uchumi mkoani Tanga.
Licha ya Serikali kuanza mikakati ya baadhi ya kufufua baadhi ya viwanda, bado wananchi wanaliona suala hilo kama lenye mtazamo wa kisiasa zaidi wakiamini hakuna mikakati madhubuti ya kurekebisha hali hiyo.
Mwaimu anasema viwanda vya mbolea, chuma na mbao bado ni muhimu kwa wkazi wa Tanga na wananchi wa Tanzania kwa ujumla.
Moja ya changamoto zilizokumba viwanda mkoani Tanga ni ukosefu wa fedha za kigeni kwa ajili ya kununua malighafi, jambo ambalo lilichagizwa na vita vya Tanzania na Uganda.
Salimu Hassan, mkazi wa Jiji la Tanga anasema kama kweli Serikali imekusudia kufufua viwanda vya chuma na kile cha mbao, ni lazima kuwe na mikakati madhubuti yenye usimamizi makini, tofauti na ilivyofanyika kwenye nyakati za kwanza za uwekezaji huku akisisitiza upatikanaji wa wawekezaji makini.
Anasema ipo haja kwa Serikali kuangalia namna ya kuwapata wawekezaji ambao wana uwezo wa kuendesha viwanda hivyo kwa maana ya wale wenye taaluma husika, badala ya kuvigawa kwa watu wenye fedha tu hata kama hawana uwezo wa kuviendesha.
Tathmini ya Serikali inaeleza kuwa, viwanda vilivyokuwa vimekufa vilikuwa vikikumbwa na changamoto mbalimbali, ukiwemo ukosefu wa malighafi za kutosha, gharama kubwa za uendeshaji, mabadiliko ya teknolojia na ushindani mkali sokoni.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo anasema wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji – Msajili wa Hazina watapanga utaratibu bora wa kuhakikisha viwanda vilivyobinafsishwa na havifanyi kazi vinaendelezwa na kufanya kazi ili kuongeza ajira, pato la Taifa na kukuza uchumi kwa ujumla.
Alisema hayo wakati wa ziara yake mkoani Tanga Agosti 22, 2024 ambapo alitembelea viwanda na kuongea na wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda kujionea utendaji kazi, kusikiliza changamoto zao na kuona njia bora ya kuzitatua kwa kushirikiana na taasisi nyingine husika.
Akizungumzia hatua ambazo Serikali inachukua, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania, Juma Mwampamba anaungana na ofisi ya mkuu wa mkoa kuwa mazungumzo yamefanyika na wamiliki wa viwanda vya chuma na mbao kutafuta njia za kuvifufua.
Wale watakaosa uwezo wa kuviendesha viwanda hivyo virejeshwa serikalini vitafutiwe wawekezaji wapya kupitia zabuni za wazi.
Pia amezungumzia kiwanda cha Mkata Saw Mill kilichoko Mkata, wilaya ya Handeni, kuwa kimekabidhiwa kwa Mamlaka ya Uzalishaji wa Mauzo Nje (EPZA), ambayo inatafuta wawekezaji wenye nia ya kufufua uzalishaji wa mbao.
Amesema Serikali, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkoa wa Tanga, imeandaa Mwongozo wa Uwekezaji 2023 unaolenga kuvutia wawekezaji wa ndani na nje na kuwa makongamano ya uwekezaji yamefanyika kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vilivyokufa ikiwa ni pamoja na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda vipya.
Mwongozo huo unataja sehemu mbalimbali za fursa za uwekezaji katika kila sekta na kila wilaya na kuelezea kwa ufasaha kila eneo.
Kuna maeneo kuu sita ya fursa za uwekezaji katika mkoa ikiwemo uanzishwaji wa maeneo maalumu ya uwekezaji wa viwandani na kilimo. Hii itahusisha serikali kushirikiana na sekta binafsi kutambua ardhi na uanzishwaji wa mbuga za uwekezaji wa kawaida kwa viwanda au kusajiliwa zaidi kama maeneo maalumu ya uchumi (SEZs) na maeneo ya usindikaji wa nje (EPZs).
Hii inachukuliwa kama chaguo bora kwa wawekezaji ikilinganishwa na kujadili na kulipa fidia wamiliki wa ardhi ambayo kawaida inakosa vifaa vya miundombinu ya msingi
Eneo lingine ni usindikaji wa kilimo ikiwemo uongezaji thamani haswa kwenye bidhaa za msingi zinazozalishwa ndani ya mkoa kama vile nafaka, katani, chai, kahawa, korosho, soya, viungo, nyama, ngozi na bidhaa za misitu
Pia mwongozo unazumgumzia kilimo cha kibiashara. Ili wakulima na wachakatajii wa mazao ya kilimo kustawi, itakuwa muhimu kuwekeza katika kuongeza tija ili kuongeza idadi na ubora wa mazao (malighafi) inayohitajika na tasnia ya usindikaji wa kilimo na watendaji wa mnyororo wa juu
Pia mwongozo unazungumzia raslimali za maliasili ambapo unataja kuongeza thamani kwa madini na mbao kuwa ni fursa ambayo inaungwa mkono na maagizo ya serikali ya hivi karibuni kuongeza thamani kwa madini na bidhaa za misitu kabla ya usafirishaji
Sekta ya huduma pia imetajwa ambapo mwongozo fursa katika huduma za hoteli na utalii, benki, masoko ya kisasa na maduka makubwa, ghala, maendeleo ya mali isiyohamishika na uchunguzi wa ardhi na ramani
Eneo la lingine ni kujenga uwezo. Hii ni pamoja na uwekezaji katika sekta ya elimu, sekta ya afya, na vituo vya mafunzo ya ufundi.
Kupitia taasisi kama TIC, EPZA, NDC, na ofisi za Balozi nje ya nchi, Serikali inaendelea kutafuta wawekezaji wa kimkakati. Mazingira bora ya uwekezaji yameelezwa ili kuhakikisha viwanda vilivyokufa vinapata wawekezaji wenye uwezo wa kuviendeleza na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, hususan katika Mkoa wa Tanga.
Juhudi za kuzungumza na wawekezaji ili kutafuta suluhu ya kufufua viwanda zinaungwa mkono na Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda, na Kilimo mkoani Tanga, Rashid Mwanyoka.
“Tunataka kuhakikisha viwanda hivi vinaanza kufanya kazi tena. Kama wawekezaji waliopo watashindwa, tutatafuta wengine wenye nia ya dhati,” alisema.
Alidai kuwa tatizo ni kuwa walionunua kwa ajili ya kuwekeza hawajafanya hivyo na badala yake wamevifunga na kuondoka.
“Tunatafuta jukwaa maalumu la kuzungumza na wafanyabiashara kujua hatua gani wachukue, itakayosaidia kuvifufua viwanda hivyo na wataoshindwa, chemba ifuatilie kuona itafanya nini, ili vifufuliwe na vianze kufanya kazi,” alisema.
Hata hivyo, Rais wa TCCIA, Vicente Minja, ametoa wito wa ushirikiano kati ya Serikali ya mkoa na wawekezaji wapya ili kurejesha hadhi ya Tanga kama mkoa wa viwanda.
“Viwanda vingi Tanga vimepewa wawekezaji wanatakiwa kuanza kuvifanyia kazi, ili kuvifufua ila hawajafanya hivyo kwa muda mrefu kama walivyokubaliana,” amesema Minja.