Maswali 10 uraia nyota Singida BS

HATUA ya wachezaji watatu wa Singida Black Stars kutangazwa kupewa uraia wa Tanzania na kuthibitishwa na Idara ya Uhamiaji, imeibua mijadala kuanzia mtaani hadi katika mitandao ya kijamii, huku kukiwa na maswali 10 magumu kutokana na taratibu zilizotumika kuwapa uraia huo.

Kabla ya Idara ya Uhamiaji kutoa taarifa hiyo juzi Alhamisi kupitia msemaji wake, SSI Paul J Mselle, tayari katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari ilishaanza kuhoji juu ya suala hilo na hasa baada ya ufafanuzi wa idara hiyo unaodaiwa uliongeza utata zaidi kulingana na sheria zilizopo.

Wachezaji hao watatu waliotangazwa kupewa uraia na kutambulika kama Watanzania kwa mujibu wa uraia kwa Tajnisi (uraia wa kujiandikisha) ni Emmanuel Keyekeh (Ghana), Josephat Arthur Bada (Ivory Coast) na Mohamed Damaro Camara (Guinea) wanaodaiwa waliomba kubadili uraia kwa mujibu wa vifungu vya 9 na 23 vya Sheria ya Uraia ya Tanzania, Sura ya 357.

Hata hivyo, baada ya taarifa hiyo kumeibuka utata na maswali magumu juu ya mchakato mzima wa kubadili uraia wachezaji hao kuwa Watanzania, huku Simba nayo ikithibitisha kuwasilisha maombi wachezaji tisa kati ya 12 ilionao kwa sasa walioomba kubadilisha uraia saa chache baada ya wenzao wa Singida Black Stars kupewa.

Utata juu ya uraia wa nyota hao wa watatu ambao walisajiliwa mwanzoni mwa msimu huu unatokana na masharti ya mtu anayetaka uraia wa Tajnisi na taarifa hizo kuibuka ghafla wakati dirisha la usajili la Ligi Kuu Bara likiwa limefungwa, huku wachezaji wao wakitumika duru la kwanza kama wageni.

Kwa mujibu wa masharti sita ya muombaji wa uraia wa kuasili zinazopatikana katika tovuti ya Idara ya Uhamiaji kati ya hayo matatu yanakinzana na sifa za wachezaji hao watatu kiasi cha kuzuka kwa mjadala mkubwa na kuzua maswali mengi.

Sharti la kwanza linamtaka (muombaji) awe ameishi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi chote cha miezi kumi na mbili (12) kabla ya tarehe ya maombi.

Wachezaji hao watatu wanajikuta wako nje ya sharti hilo kwa kuwa wana miezi kati ya mitano na sita tangu walipotangazwa kusajiliwa na Singida kuwa miongoni mwa nyota wa kigeni waliotumikia timu hiyo katika duru la kwanza la Ligi Kuu Bara kupitia dirisha kubwa la usajili lililofungwa Agosti, mwaka jana.

Sharti la pili linasema kwamba muombaji katika kipindi cha miaka 10 iliyotangulia kipindi tajwa cha miezi 12 aliishi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda wa jumla ya miaka isiyopungua saba eneo ambalo nalo linawanyima uhalali wa kifungu hicho wote wakiwa na chini ya miezi sita.

Sharti la tatu linawataka waombaji kuwa na ujuzi wa kutosha wa Lugha ya Kiswahili au Kiingereza ambapo hapa ni Keyekeh pekee anayejua Kiingereza (lugha ambayo pia inatumika pia nchini kwao, Ghana), lakini wengine wawili wanazungumza Kifaransa na pia hawajui sio kuongea tu, bali hata kuandika Kiswahili.

Mbali na masharti hayo pia wachezaji hao mchakato wao unakutana na wingu zito kwa mujibu wa taratibu za maombi kipengele cha nne kinachotaka waombaji kuchapisha katika matoleo mawili mfululizo ya magazeti ya kila siku yaliyosajiliwa Tanzania Bara na Zanzibar notisi ya nia ya kuomba uraia, hatua ambayo bado haijathibitishwa kama ilifanyika, mbali na kutakiwa wenyewe kuomba kubadili uraia walionao.

Ndani ya sakata hilo hakuna kiongozi wa TFF aliyekuwa tayari kulizungumzia ambapo vigogo wengi wameonekana kukimbia kuliongelea huku mmoja wao akisema hakuna anayejua kwa undani mzizi wa mabadiliko hayo.

“Kiukweli ukituuliza hakuna anayefahamu wapi mchakato huu umeanzia. Kama mnavyoona ni mambo ambayo yapo nje ya mfumo wa utawala wa TFF kwa ukubwa wake linaonekana lipo kwenye ngazi ya kiserikali zaidi na sio mamlaka ya soka,” alisema bosi mmoja wa shirikisho hilo ambaye aligoma kuandikwa jina lake gazetini.

Hali hiyo ya TFF kuuruka mpira huo ni kuwepo kwa taarifa kwamba tayari Singida BS ilishakuwa na wachezaji wa kigeni zaidi ya 12 wanaotakiwa kikanuni, kwa mujibu wa chanzo kutoka ndani ya timu hiyo wakiwamo nyota wapya wanne waliotambulishwa hivi karibuni akiwamo beki Mghana Frank Assink, kipa Amas Obasogie (Nigeria) na washambuliaji Serge Pokou (Ivory Coast) na Jonathan Sowah (Ghana).

Mbali na nyota hao wapya, Singida BS tayari ilikuwa na Marouf Tchakei, Elvis Rupia, Andy Koffi, Anthony Tra Bi, Mohammed Damaro, Ibrahim Imoro, Emmanuel Keyekeh, Josephat Bada, Victorien Adebayor mbali na wale waliokuwa kwa mkopo Tabora United kina Morice Chukwu na Faria Ondongo waliorudishwa.

1. Kama mchakato huo ulifanyika ilikuwa ni lini na waliomba wenyewe au waliombewa na walihojiwa na Kamati ya Usalama ya Wilaya na taarifa kupelekwa mkoani kama sheria inavyotaka?

2. Kama wameishi kwa muda mfupi nchini na hawajui Kiswahili na miongoni mwao Kiingereza, vigezo gani vilitumika kwa Idara ya Uhamiaji kuwakubalia ombi hilo wakati inakinzana na sheria ya uraia wa Tajnisi?

3. Kwanini mabadiliko hayo ya uraia yamekuja wakati dirisha la usajili likiwa limefungwa, kuna siri gani nyuma yake?

4. Je wachezaji wengine wa kigeni kutoka klabu zingine wakiamua nao kuomba kubadilishiwa uraia kama ilivyofanyika kwa wachezaji hao watatu nao watapata?

5. Wachezaji tajwa waliitumikia Ligi Kuu msimu huu duru la kwanza wakitambulika kama nyota wa kigeni wakipewa vibali vya kuishi nchini kama wageni, watasomekaje ndani ya mfumo kwa sasa?

6. Sheria za Fifa zinawabana juu ya kuhamisha uraia wao, hatma yao itakuwaje kwenye kuitumikia Taifa Stars wakiwa Watanzania?

7. Endapo mchakato huu utaendelea kuleta shaka na hata kukwama TFF, itakuwa nini hatma ya wachezaji hao kuitumikia Singida na itakuwaje kwa mechi zilizobakia msimu huu?

8. Inawezekana maombi ya kubadilisha uraia yalianzia kwa wachezaji wenyewe kama inavyoelezwa, ukomavu wa uongozi wa klabu au hata TFF ulikuwa na nafasi gani katika kuondoa utata unaoendelea na utakaoendelea?

9. Kanuni inasema kila klabu itakuwa na haki ya kusajili wachezaji 12 wa kigeni, kupitia uamuzi huu idadi ya wachezaji wa kigeni itabaki hivyo hivyo au itaongezeka kupitia fursa kama hii ya kubadili uraia kwa haraka?

10. Moja ya sharti linalotakiwa kubadili uraia wa muombaji anatakiwa mara atakapoidhinishwa kuendelea kuishi ndani ya nchi kwa kudumu, lakini mmoja wa wachezaji hao aliondoka hivi karibuni kwenda kuona na familia yake ikabaki huko atawezaje kuishi hapa kwa sharti hilo?

Mara baada ya Idara ya Uhamiaji kutangaza wachezaji watatu wa Singida BS kupewa uraia, klabu ya Simba nayo imetangaza kuwaombea wachezaji tisa kati ya 12 wa kigeni ilionao, bila kuweka hewani majina husika.

Awali, ilisambaa barua mtandaoni ikionyesha kusainiwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu, bila kuthibitishwa kama ilikuwa ni halali au la, lakini Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alikiri jana kwamba ni kweli wamewasilisha maombi ya wachezaji tisa wanaoomba uraia.

“Ni kweli Simba imewasilisha maombi ya wachezaji hao wanaotaka kubadilisha uraia waliokuwa nao na tunasubiri kuona watajibiwaje,” alisema Ahmed kwa ufupi.

Mwanaspoti leo liliwasiliana kwa njia ya simu na maofisa wa Idara ya Uhamiaji ili kutaka ufafanuzi wa maswali hayo na taarifa za Simba kuwasilisha maombi yao, lakini simu hazikupowa kwa muda mrefu hadi tunaingia mitamboni.

Related Posts