Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), limetangaza matokeo ya mithani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka 2024, yakiwa na sura ya furaha na vilio.
Ni furaha kwa watahiniwa 477,262 kati ya 516,695 waliopata daraja la kwanza hadi la nne sawa na asilimia 92, 37. Ufaulu huu ni sawa na ongezeko la asilimia 3.01 ikilinganishwa na wa mwaka 2023.
Hata hivyo, wapo wenye huzuni wakiwamo watahiniwa 39,433 waliopata sifuri. Kwa idadi hiyo ni sawa na kusema mwanafunzi mmoja kati ya 13 waliofanya mtihani wa kidato cha nne 2024 amepata daraja sifuri.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed, kati ya waliopata sifuri wasichana ni 22,477 sawa na asilimia 8.28 na wavulana ni 16,956 sawa na asilimia 6.92.
Hata hivyo idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na wanafunzi 56,149 mwaka 2023 na 63,583 mwaka 2022 waliopata daraja hilo.
Jambo hili linawaibua wadau wa elimu wakijadili sababu ya matokeo haya na hatma ya wanafunzi hao.
Mdau wa elimu, Ochola Wayoga amesema mwanafunzi kupata daraja sifuri kunachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo uhaba wa vifaa vya kufundishia na walimu, lakini akaongeza wanaopata daraja hilo, haimaanishi hawawezi kufanya vitu vingine.
“Hakuna mtu ‘reject’ (asiyeweza kufanya lolote), miongoni mwa hawa ndiyo tutawahitaji kuwa mafundi magari, mafundi friji, watengeneza bustani na kazi kama hizo,” amesema Ochola Wayoga.
Amesema kupata daraja sifuri hakumuondolei mtu uwezo wake binafsi, kwa sababu kunachangizwa na sababu mbalimbali.
“Yawezekena yale aliyofundishwa hakuyaelewa, hili kundi lina fursa ya kujikita kwenye mifumo isiyo rasmi, wengine wanaweza kurudia mitihani na wengine kujikita kwenye ufundi.
“Tunawategemea kwenye ufundi ujenzi, kuchomelea, kutengeneza magari, friji, kuwa wataalamu wa bustani na fani nyingine,” amesema.
Wasiwasi wa Ochola ni endapo kazi hizo nazo zitahitaji uwe na elimu ya kuanzia kidato cha nne, kundi hilo halitakuwa na uthibitisho chochote kwamba lilikaa darasani na kusoma elimu ya sekondari kwa miaka minne.
“Sijui kama itashusha elimu yetu, lakini kundi hili halina uthibitisho wowote kwamba mhusika aliwahi kusoma sekondari, atalindwa na cheti cha darasa la saba.
‘Kundi hili linalindwa na cheti cha darasa la saba, anapopata daraja sifuri maana yake hana uthibitisho mwingine unaoonyesha aliwahi kusoma sekondari na kuna shule ina zero (sifuri zaidi ya 40), hawa watu hawashindwi kufanya ufundi,”
“Sijui kama nitakuwa naishusha hadhi ya elimu yetu, lakini ningetamani iangaliwe tena, kusiwe na daraja sifuri, tuishie daraja la nne ili kuwapa uthibitisho kundi hili ambalo limefeli mitihani lakini lina ujuzi mwingine,” amesema.
Mdau mwingine wa elimu, Avemaria Semakafu anasema si ajabu mtu akapata daraja sifuri, lakini akaja kufanya vyema kimaisha.
“Kama kuna kitu kinatakiwa kupewa uzito ni huu mtalaa mpya, wapo watakaokwenda na hesabu, ufundi, sanaa na taaluma nyinginezo.Kila mmoja atashikilia kile anachokiweza, leo hii tunahesabu daraja sifuri, lakini tuupe nafasi kwanza mtalaa mpya tuone utatubebaje,” amesema Semakafu ambaye aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mdau mwingine, Zaida Mgalla amesema ufaulu wa asilimia 42.96 kwa daraja la kwanza hadi la tatu bado si wa kuridhisha.
“Waliosalia wameangukia daraja la nne na sifuri bado ni changamoto kwani inaonyesha zaidi ya nusu ya watahiniwa wameangukia kwenye daraja la nne na sifuri.
“Hii sio picha nzuri kwani hawa wa daraja la kwanza hadi la tatu ndiyo tunawafikiria wajiunge na kidato cha tano na kusoma kozi mbalimbali katika vyuo vya Serikali.
Zaida ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Uwezo Tanzania, amesema zaidi ya nusu wanarudi mtaaani, akihoji hilo kundi linarudi mtaani kufanya nini?.
“Bado elimu yetu sio bora inawavusha wachache na wengi wanafeli, tunataka kama umemamliza kidato cha nne umefunzwa vizuri na stadi za kazi uweze kujiajiri, pia kwa wanaofaulu huko ndipo tupate wataalamu.
“Lakini pamoja na matokeo kuonyesha kuna ongezeko la ufaulu, bado upo chini, nafikiri tuna haja ya kufanya utafiti wa kina, kuongea na watoto, walimu kujua changamoto ni nini?”
Kwenye masomo ya sayansi asilia, hisabati na teknolojia wanafunzi wengi wamefeli. Kwa mujibu wa takwimu za Necta somo la hisabati ufaulu wake wa alama A hadi C ni asilimia 11.71, ukiwa umeshuka kulinganisha na wa mwaka 2023 ambapo asilimia 12.75 walipata daraja A hadi C.
Hii inamaanisha zaidi ya robo tatu ya wanafunzi 516,520 walipata alama D au F. Kwenye somo la fizikia ufaulu wa alama A hadi C ni asilimia 32.59 ukishuka kulinganisha na mwaka jana ambao ulikuwa ni asilimia 32.82.
Wakati kwenye biolojia ufaulu wa alama A hadi C ni asilimia 40.04, licha ya kuwa chini ya 50, ufaulu huo umepanda kulinganisha na mwaka 2023 ambapo ufaulu wa daraja A hadi C ulikuwa ni asilimia 35.36.
Masomo ambayo wanafunzi wamepata alama A hadi C juu ya asilimia 50 ni kemia, uhandisi na kilimo.
Mengine yenye ufaulu wa zaidi ya asilimia 50 kwa alama A hadi C ni Tehama, hisabati ya ziada na chakula na lishe.
Ufaulu chini ya asilimia 50 kwenye masomo hayo unatajwa kuwa na athari katika harakati za Tanzania ya viwanda.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Ubunifu katika Elimu Tanzania (EIT), Benjamin Nkonya amesema changamoto ya masomo hayo ni kujifunza kwa nadharia tofauti na vitendo.
“Mfano ni fundi makochi, ukimpa kochi akutengenezee hawezi kukosea na vipimo, lakini mtu huyo huyo si ajabu alifeli darasani, au jiulize ni kwanini konda wa daladala hakosei kurudisha chenji, lakini huyo huyo shuleni somo la hesabu alifeli.
“Shida ipo kwenye ufundishaji, tunajifunza kwa nadharia zaidi kuliko vitendo, tukiweza kutoka huko, bila shaka ufaulu katika masomo haya utaongezeka,” amesema.
Naye, Wayoga amesema kama hatua zisipochukuliwa na ufaulu wa masomo hayo kuendelea kuwa chini ya asilimia 50, kuna uwezekano wa kupunguza upatikanaji wa wataalamu na kufifisha harakati za Tanzania ya viwanda.
“Tusipokuwa na wataalamu wa kutosha maana yake tutawatumia wataalamu kutoka nje, jambo ambalo ni gharama na huenda likapunguza wimbi la wawekezaji kuja kuwekeza kutokana na gharama hivyo kusababisha uchumi pia kushuka,” amesema.
Ameshauri Serikali kuwekeza kwa walimu wa masomo hayo na kuwatengenezea mazingira ambayo yatawashawishi vijana wengi kupenda kuyasoma masomo.
Semakafu amesema kufeli kwa somo la hisabati ni kutokana na ukweli kuwa linafanywa na wanafunzi wote.
“Kama nilivyosema awali, tuupe muda mtalaa mpya, hapo ndipo tutakuwa na haki ya kusema ule wa awali ulilega upande mmoja na kusahau upande mwingine, ndiyo tunaona matokeo ya ufaulu huu kwenye masomo haya,” amesema.
Mbali na masomo ya sayansi, kwenye masomo ya biashara ufaulu umeongezeka. Somo la commerce ufaulu wa kwa daraja A hadi C ni asilimia 50.58 ukipanda kutoka asilimia 37.81 mwaka 2023.
Kwenye somo la book-Keeping waliofaulu kwa daraja A hadi C ni asilimia 54.98 kutoka asilimia 38.83 ya mwaka 2023.
Jumla ya watahiniwa wa shule 477,262 kati ya 516,695 wenye matokeo sawa na asilimia 92.37 wamefaulu kwa daraja la kwanza hadi la nne. Ufaulu huu ni sawa na ongezeko la asilimia 3.01 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Katika matokeo hayo asilimia 42.96 walipata ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu kati ya watahiniwa 542,611 wasichana wakiwa 296,051 na wavulana 261,745.
Kwa watahiniwa waliopata daraja sifuri japo idadi imeshuka kutoka asilimia 10.64 mwaka 2023 hadi asilimia 7.63, bado nguvu ya ziada inatakiwa kufanyika ili kupunguza kundi hilo mtaani.
Kwa mujibu wa Necta, watahiniwa 39,433 wamepata daraja sifuri mwaka huu, wasichana wakiwa 22,477 sawa na asilimia 8.28 na wavulana ni 16,956 sawa na asilimia 6.92.
Idadi hiyo imepungua kulinganisha na mwaka jana ambapo watahiniwa 56,149 walipata daraja sifuri, wasichana wakiwa 33,764 sawa na asilimia 11.89 na wavulana walikuwa 22,385 sawa na asilimia 9.19.
Matokeo hayo yamewaibua wataalamu wa masuala ya elimu ambao baadhi wanatamani mifumo ya elimu ibadilike ili kusiwepo na daraja sifuri na wengine wakieleza kuwepo na fursa mpya kwa kundi hilo kwenye mtalaa mpya.
Kwa mujibu wa Necta, kwenye matokeo ya jumla, ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 89.36 mwaka jana hadi asilimia 92.37 mwaka huu kwa watahiniwa wa shule huku ufaulu huo kwa watahiniwa wa kujitegemea ukiwa ni asilimia 62.51 kutoka asilimia 52.44 mwaka jana.
Katika ufaulu huo, wasichana wamefaulu kwa asilimia 91.72 na wavulana ni asilimia 93.08 kwa watahiniwa wa shule na wale wa kujitegemea wasichana ni asilimia 62.06 na wavulana ni asilimia 62.51.
Necta limezuia matokeo ya wanafunzi 459. Hata hivyo, wanafunzi hao wamepewa fursa ya kurudia mitihani yao mwaka huu.
Katibu Mtendaji huyo amesema wanafunzi hao ni wale waliopata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mitihani yao kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo.
“Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mitihani mwaka huu kwa masomo ambayo hawakuyafanya kwa sababu ya ugonjwa,” amesema.
Baraza hilo limebainisha kukifungia kituo P6384 BSL Open School cha mkoani Shinyanga kuwa kituo cha mitihani ya taifa, kutokana na kuratibu mipango ya udanganyifu.
“Kinafungiwa kwa mujibu wa kifungu 4(8) cha kanuni za mitihani mwaka 2016 hadi hapo Baraza litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji wa mitihani ya taifa,” amesema.
Walioandika matusi kuadhibiwa
Necta limesema wanafunzi watano walioandika lugha ya matusi wataadhibiwa.Wanafunzi hao watano ni kati ya watahiniwa 72 waliofutiwa matokeo, wengine 65 wamefutiwa matokeo kwa udanganyifu.
Amesema, mbali na kufuta matokeo ya wanafunzi hao, pia wameziandikia shule walizosoma ili kutoa taarifa kwa wazazi wao wawachukulie hatua za kimaadili kwa kuandika matusi.
“Kuandika matusi kunaendana na maadili si kwenye mitihani tu, hadi kwingineko na matusi hayakubaliki kila mahali.
“Mwaka huu wametokea watano walioandika matusi kwenye matokeo ya kidato cha nne, katika matokeo ya kidato cha pili pia walitokea watano na mwaka 2023 kwenye matokeo ya kidato cha nne walitokea watano,” amesema.
Amesema iwapo Watanzania wataendelea kukemea jambo hili la kuandika matusi kwenye mitihani, huenda likakoma.