Mikakati ushindi Yanga hii hapa

Katika kuhakikisha inafanya vizuri kwenye mashindano ya ndani baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga imepanga kufanya mambo mawili ikiamini yatakuwa na tija kwa mechi ilizobakiza msimu huu.

Jambo la kwanza ambalo imeamua kulifanya ni kufanya maboresho ya kamati yake ya mashindano ambapo kuna baadhi ya watu itawapunguzwa na wengine kuongezwa ili kuipa nguvu zaidi.

“Ni maboresho ya kawaida ambayo yamekuwa yakifanyika mara kadhaa pindi msimu unapomalizika au pale ambapo uongozi unaona kuna sehemu inayumba hivyo wala sio jambo la ajabu au la kushangaza kwa vile lengo ni timu ifanye vizuri,” kilisema chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga.

Timu hiyo pia imeamua kurudisha utaratibu wa kambi kwa wachezaji wake ambayo itaanza rasmi leo huko Avic Town Kigamboni.

“Wachezaji wataingia kambini kesho (leo) na itakuwa endelevu tofauti na zamani ambapo walikuwa wakitokea majumbani na kisha kukutana siku chache kabla ya mechi,” kilisema chanzo hicho.

Kibarua cha kwanza kwa nyota wa Yanga baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika ni mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB ambayo itakabiliana na Copco ya Mwanza, Jumamosi, Januari 25.

Baada ya hapo itakuwa na mechi tano za Ligi Kuu ambazo inahitajika kupata ushindi ili ijiweke katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wake.

Katika Ligi Kuu, kibarua cha Yanga kitaanza Februari Mosi kwenye Uwanja wa KMC Complex dhidi ya Kagera Sugar na Februari 5 itacheza na KenGold katika Uwanja huohuo.

Siku tano baadaye itakuwa hapahapa Dar es Salaam kucheza ugenini na JKT Tanzania katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na Februari 14 itakuwa ugenini dhidi ya KMC katika Uwanja wa KMC Complex ambao itautumia kucheza na Singida Black Stars, Februari 17.

Kwa sasa, Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 39 huku Simba ikiongoza na pointi 40.

Related Posts