Miti huongeza thamani ya jengo kwa asilimia 30

Dar es Salaam. Imeelezwa kwamba kuna faida nyingi za kupanda miti mbali na uhifadhi wa mazingira na kuwa hatua hiyo huongeza pia thamani ya jengo kwa asilimia 30.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Januari 24, 2025 na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma, Tafiti na Ushauri) wa Chuo Kikuu Ardhi, Profesa John Lupala, katika shughuli ya upandaji miti 400 katika maeneo mbalimbali chuoni hapo.

Profesa Lupala amesema kwa sasa watu wamekuwa na kampeni ya kupanda miti kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kutunza mazingira, lakini kuna faida nyingine nyingi ikiwemo kupandisha thamani ya jengo husika.

“Katika biashara ya nyumba na makazi, nyumba iliyo na miti huwa ina thamani kuliko isiyokuwa na miti. Hivyo, kama chuo tunavyozidi kupanda miti mingi zaidi katika eneo letu hili, ndivyo majengo na ardhi yetu inavyozidi kupanda thamani,” amesema profesa huyo.

Faida nyingine amezitaja kuwa ni pamoja na kuongeza mwonekano wa jengo, kusaidia kutambulika kwa kitu, na kuleta hali nzuri ya hewa.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Evaristo Liwa amesema kumekuwa na uendelezaji wa ujenzi katika maeneo hayo ya chuo, jambo linalosababisha ukataji wa miti mara kwa mara, ambayo inapaswa kurejeshwa.

“Kipindi cha nyuma tulikuwa tuna miti mingi sana eneo hilo, hadi ikafika mahali tukazuia kupandwa kwa miti mingine, lakini sasa tunaona ni wakati muafaka wa kufanya hivyo kutokana na baadhi kukatwa kwa ajili ya shughuli hizo za maendeleo ya ujenzi zinazofanyika,” amesema Profesa Liwa.

Wito wake kwa watumishi wa chuo hicho ni kuhakikisha wanaitunza miti hiyo ili ije ifae kwa vizazi vijavyo.

Pia ameongeza kuwa chuo hicho ndicho wabobezi wa kufundisha wataalamu wa mandhari ya kuishi binadamu, hivyo wanachofanya ni kwa vitendo wakiwashirikisha wanafunzi.

Ofisa Misitu Msaidizi wa Wilaya ya Ubungo, Kanuti Matasha amepongeza chuo kwa walichokifanya na kueleza kuwa wao katika kuhifadhi, kutunza na kuendeleza mazingira wamekuwa wakitoa miti ya bure kwa wananchi na kuwakaribisha watumishi wa chuo hicho kwenda kuchukua.

“Miti tunayotoa ni pamoja na ya kivuli, matunda na ya mbao. Unachotakiwa ni kuandika barua tu ya kuomba miti unayohitaji, nasi tutakupatia. Tuchangamkie fursa hiyo ili wote tuweze kutunza mazingira yetu,” amesema ofisa huyo.

Mwakilishi wa Taasisi ya Mabadiliko ya Tabianchi, Jophillene Bejumula amezungumzia miti na uoto wa asili baharini kuwa ina uwezo wa kunyonya hewa chafu kwa asilimia 30, lakini mpaka sasa ipo chini ya asilimia 22.

Related Posts