Muhimbili yapatiwa vifaatiba vya kisasa kurahisisha upasuaji

Dar es Salaam. Wagonjwa watakaofanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, watanufaika na maboresho ya huduma hiyo baada ya Ubalozi wa China, kuipatia hospitali hiyo vifaatiba vya teknolojia ya kisasa, vinavyorahisisha huduma ya upasuaji vyenye thamani ya Sh125 milioni.

Upatikanaji wa vifaa hivyo, unaifanya hospitali ya Muhimbili kuingia katika dunia ya uvumbuzi na teknolojia ambayo sasa itakuwa na hadhi sawa na hospitali zinazofanya tiba utalii duniani.

Miongoni mwa vifaa hivyo vya kisasa ni pamoja na mashine inayomsaidia daktari wa upasuaji kuona kwa ufasaha mpaka vishipa vidogo vidogo na hivyo kupunguza madhara ya upasuaji kwa mgonjwa.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya msaada huo leo Ijumaa, Januari 24, 2025 Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Mohamed Janabi amesema mashine hizo zitaisaidia hospitali kuanza kutoa huduma za upasuaji kwa wagonjwa kwa njia za kisasa zaidi ikilinganishwa na hapo awali.

“Mashine hizo zina uwezo wa kumsaidia daktari kuona mishipa ya fahamu au ya damu kwa ufasaha hata ile mishipa midogo kabisa kwa sababu yote ipo kama darubini inavyotumika kukuza, hii ni teknolojia mpya inasaidia sana wakati wa upasuaji,” amesema.

Kwa mujibu wa Profesa Janabi, mashine nyingine inayotumika kuingiza mdomoni au puani kabla mgonjwa hajawekewa dawa ya usingizi, itasaidia kumwelekeza daktari na kusaidia kutoumiza tishu za mgonjwa wakati wa huduma hiyo.

“Hii mashine huwa tunapitisha kwenye njia ya hewa, inanionyesha kwenye kioo hapa kwamba inakwenda wapi, badala ya kuingiza bila kujua kama tulivyokuwa tunafanya mwanzo. Uwezekano wa mgonjwa kuumia unakua mdogo na hata kuumiza baadhi ya tishu za mgonjwa wakati wa utoaji huduma unaondoka.

“Hii tunaweza kuingiza mdomoni au puani. Hii ni teknolojia ambayo mimi kama daktari ninaweza kuionea nje, wapi inakokwenda kwa sababu yote inaingia kwenye mapafu. Inakwenda kwenye njia ya hewa, nimlaze mgonjwa kisha niendelee na upasuaji,” amesema Profesa Janabi.

Amesema mashine hiyo inasaidia kumuonyesha mtaalamu kama kuna kizingiti mahali, anabadilisha njia badala ya kuingiza mdomoni, anaingiza mashine hiyo kupitia pua.

Profesa Janabi ameitaja mashine nyingine ni ile inayosaidia kutoa dawa kwa mgonjwa kwa muda unaotakiwa, kazi ambayo hapo awali ilifanywa na muuguzi.

“Hii sihitaji kuwa na nesi, ninaweza nikaiweka pale nikaiseti kila baada ya dakika 10 nataka itoe dawa na vilevile zinasaidia sana wakati mgonjwa ametoka chumba cha upasuaji, unaagiza kila baada ya saa mbili mgonjwa apewe dawa, hauhitaji nesi kukaa pale, unaiseti ikifika muda wake inatoa dawa bila shida,” amesema.

Akipokea msaada huo, Waziri wa Afya Jenister Mhagama amesema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano kati ya Serikali hizi mbili.

“Msaada huu wenye thamani ya Sh125 milioni ni ushahidi mkubwa wa mshikamano imara na utayari wa pamoja katika kuimarisha huduma za afya nchini. Msaada huu ni mchango muhimu sana katika kukabiliana na mahitaji ya huduma za afya kwa jamii,” amesema.

Waziri Jenister amesema mashine hizo zitasaidia kuendelea kutoa huduma za tiba za kibingwa na kibobezi kuendana na teknolojia inayobadilika kila siku duniani, “Tunawashkuru China kutupatia nyenzo, mashine na vifaa vya teknolojia ya hali ya juu, inatufanya tuzidi kuwa imara katika tiba utalii.’

Balozi kutoka Timu ya Misaada ya Matibabu ya China kwa Tanzania, Chen Mingjian amesema huo ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Amesema tangu mwaka 1968, China ilianza kutuma timu za misaada ya matibabu katika Tanzania. Hadi sasa, vikosi 27 vya timu hizo vimekuwa vikitoa huduma za matibabu, wakihudumia zaidi ya wagonjwa milioni 20.

Related Posts