Mvua ya mawe yaharibu ekari 120 za tumbaku Chunya

Mbeya. Mashamba ya tumbaku yenye ukubwa wa ekari 120 yameathiriwa na mvua ya mawe iliyoambatana na upepo Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Mvua hiyo ilinyesha Januari 20, 2025 katika baadhi ya maeneo na kusababisha majani ya zao hilo kuharibika.

Mashamba yaliyoathirika yanamilikiwa na wakulima 31 ambao ni wanachama wa Amcos za Magunga na Ifuma zilizopo wilayani humo.

Kufuatia athari hizo, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga ameagiza kuanzishwa mfuko maalumu wa majanga ili uwe msaada pindi yanapojitokeza majanga kama hayo.

Batenga amewataka maofisa kilimo katika halmashauri na kutoka kwenye kampuni za ununuzi wa zao la tumbaku kuongeza usimamizi na ushauri wa kitaalamu kwa wakulima ili kuona njia ya kunusuru miche michache ilibaki mashambani.

“Niwaombe wakulima kukubaliana na mapendekezo ya kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa majanga ili kuwapunguzia hasara pindi yanapojitokeza matukio ambayo hayawezi kuzuilika,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Januari 24, 2025, Batenga amesema baada ya kutokea tukio hilo alikwenda na kamati ya ulinzi na usalama kuona madhara yaliyojitokeza.

“Nimejirishisha, nimetoa maelekezo kwa vyama vya msingi vya wakulima kuanzisha mifuko ya majanga ili wakulima wanaopata maafa waweze kusaidiwa na punguziwa makali ya hasara zinazojitokeza,” amesema Batenga.

Pia, amewataka wakulima kuzingatia elimu ya wataalamu wa kilimo na kufuatilia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) katika kipindi hiki cha mvua za juu na chini ya wastani.

Mkulima Jema Jaluo ambaye ni miongoni mwa waathirika amesema hali ni mbaya lakini anamshukuru Mungu kwa sababu alikuwa na vibarua 30, lakini kwa uwezo wake, wote wako salama.

“Mimi ni miongoni mwa wakulima tuliopata changamoto lakini kwa sasa ni mapema mno kujua madhara yaliyojitokeza kufuatia mvua hiyo,” amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Magunga, David Siwakwi amesema athari kubwa imeyojitokeza kwenye mashamba ya tumbaku, hivyo wanaiomba Serikali iwashike mkono wakulima hao katika kipindi hiki.

Ofisa katika Bodi ya Tumbaku Wilaya ya Chunya, Loysuhaki Kimiri amesema tathmini ya awali inaonyesha kwamba zaidi ya ekari 128 zinazolimwa na wakulima 31, zimeathiriwa.

Related Posts