Nguvu zaidi zinahitajika ulinzi ghuba ya Chwaka

Unguja. Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud amesema umefika wakati sasa kuongeza nguvu ya ulinzi katika Ghuba ya Chwaka, kutokana na kuwepo kwa baadhi ya wavuvi kuendelea na uharibifu wa hifadhi za bahari na rasilimali zake.

Ameyasema hayo leo Ijumaa Januari 24, 2025 wakati akizindua na kukabidhi boti ya doria kwa ajili ya kamati ya usimamizi wa doria ya Ghuba ya Chwaka. 

Ayoub amesema Serikali imefanya uamuzi wa kuzuia eneo hilo lisitumike kwa uvuvi wa nyavu na matumizi mengine ya uvuvi kutokana na jiografia ilivyo ya ghuba hiyo. 

 Hata hivyo, amesema kutokana na ukubwa wa historia ya hifadhi ya Ghuba ya Chwaka chimbuko lake ni changamoto za kiuvuvi na upatikanaji wa mazao ya bahari katika ukanda huo, hivyo limekuwa jicho la Serikali.

‘’Sisi tutatimiza wajibu wetu ndani ya wiki hii, hakuna mtu aliyeruhusiwa kuvua uvuvi haramu au eneo la hifadhi la Serikali hii mpaka sasa, kwahiyo tutakuwa makini na wakali kulinda,” amesema.

Ameeleza azma ya Serikali  ni kutatua changamoto za wavuvi wadogowadogo na ndio maana zinatolewa boti za kisasa katika uvuvi ambapo kwa ukanda wa Kusini wamepewa boti 100 ili kuepusha uvuvi haramu.

 “Kutokana na umuhimu wa kuhifadhi bahari na ni jambo la kisheria hivyo wadau hao kutoa boti hiyo ni kuiunga mkono Serikali kupitia ushirikiano uliopo na ni chachu ya mafanikio kwa serikali kwani mashirikiano hayo ya wadau yanasaidia kubadili fikra za baadhi ya wananchi na mienendo yao,” amesema.

Wakati huohuo, ametoa agizo kwa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi kukamilisha taratibu za eneo la Chamakangu kufungiwa kwa shughuli za uvuvi na kutumika kwa shughuli za utalii kwa ajili ya maslahi ya jamii na taifa kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi Idara ya Uhifadhi wa Bahari, Dk Makame Omar Makame amesema kamati ya usimamizi wa pamoja ya Ghuba Chwaka (CMG), imesaidia kuimarika kwa rasilimali za bahari jambo ambalo limesaidia kuinua uchumi wa buluu kupitia sekta ya uvuvi na utalii.

“Kamati hiyo ni muhimu sana katika kufikia malengo ya Serikali. Tunahitaji kamati kushirikiana na kupata fursa ya kukaa pamoja na kujadiliana namna bora ya kutumia bahari ipasavyo,” amesema.

Amesema Wizara ya uchumi wa Buluu na Uvuvi imepewa jukumu la kusimamia uvuvi na kuimarisha mazingira ya bahari kwa ajili ya maslahi ya wavuvi na watalii wanaoingia katika ghuba hiyo.

“Ili tuweze kuwa na uchumi wa buluu lazima tuwe na usimamizi madhubuti wa kulinda rasilimali za bahari na uvuvi endelevu unaofuata sheria na kanuni za uvuvi za hapa nchini,” amesema.

 Ametoa wito kwa kamati ya usimamizi baada ya makabidhiano ya boti hiyo,  kushirikiana na wananchi kupitia kamati za uvuvi, wadau wa maendeleo na vyombo vya ulinzi na usalama ili kufikia lengo lililowekwa na Serikali. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa MCCC, Dk Said Khalid amesema MCCC kwa  kushirikiana na idara ya maendeleo ya uvuvi na wanajamii,  wanafanya tathmini ya maeneo yaliowazunguuka jamii husika kwa lengo la kuweka utaratibu wa matumizi mazuri katika hifadhi za bahari.

Dk Said amesema elimu zaidi itaendelea kutolewa kwa wanajamii ili kuleta faida kwa wavuvi katika kujiongezea kipato kupitia uhifadhi wa bahari.Amesema vikundi 15 tayari vimepatiwa mafunzo ya uhifadhi wa bahari.

Akizungumza kwa niaba ya wanakamati ya usimamizi shirikishi (CMG) Mwenyekiti katika Ghuba Chwaka, Muhsini Moh’d ameziomba taasisi husika,  kuwapatia bajeti ya kutosha ili kuweza kufanya kazi ya doria kwa ajili ya kupambana na wavuvi wanaokiuka utaratibu uliowekwa na Serikali.

Related Posts