Nne za Pamba Jiji zampa ujanja Minziro

KOCHA Mkuu wa Pamba Jiji, Fredy Felix ‘Minziro’ amesema mechi nne za kirafiki zitamsaidia kutengeneza muunganiko wa kikosi kati ya maingizo mapya na ya zamani na kuwa tayari kwa ushindani kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri na kubaki Ligi Kuu.

Pamba iliyosajili wachezaji tisa dirisha dogo lililofungwa Januari 15, mwaka huu wakiwemo sita wa kigeni, imepanga kucheza mechi nne za kirafiki dhidi ya Geita Gold, Stand United, Alliance FC na Copco FC uliopigwa juzi na timu hiyo kushinda mabao 3-0 katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Akizungumza baada ya ushindi dhidi ya Copco FC, Minziro alisema maandalizi yanakwenda vizuri huku kazi kubwa ikiwa ni kutengeneza muunganiko wa kikosi ambapo mechi za kirafiki zitakuwa na msaada mkubwa.

“Tumeanza na Copco, Alliance kisha Geita Gold na Stand United tunajaribu kutafuta mechi kutengeneza timu na kupata muunganiko wa kikosi, najaribu kuhakikisha kwamba kila wakati wachezaji wawe tayari mchezoni ili tupate matokeo mazuri,” alisema Minziro.

“Tumeingiza maingizo mapya ambayo yataleta ushindani ndani ya timu kwa sababu kila idara ina wachezaji wawili mpaka watatu. Makocha tutapata wakati mgumu kupanga wachezaji kwenye nafasi zao kutokana na ushindani ulivyo sasa.”

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji, Ezekiel Ntibikeha alisema japokuwa mzunguko wa kwanza hawakufanya vizuri lakini wamejipanga kuibakisha timu katika Ligi Kuu Bara.

Related Posts