Dar es Salaam. Aliyekuwa mgombea uenyekiti wa Chadema katika uchaguzi wa Januari 21, 2025, Odero Charles Odero, amemshukuru mjumbe aliyempigia kura kwenye uchaguzi huo huku, akisema kura hiyo ina thamani kubwa kwake.
Katika uchaguzi huo, Odero alipata kura moja akishindana na vigogo wawili wa chama hicho, Freeman Mbowe, aliyepata kura 482 na Tundu Lissu aliyetangazwa mshindi kwa kupata kura 513 na hivyo kuwa mwenyekiti mpya wa Chadema akipokea kijiti kutoka kwa Mbowe.
Uchaguzi huo ulikuwa na mikikimikiki mingi hasa kati ya Mbowe na Lissu ambao timu zao zilikuwa zikitupiana maneno kwenye mitandao ya kijamii, huku kila upande ukijitapa kuibuka kidedea kwenye uchaguzi huo wa kihistoria.
Odero ambaye hakuwa na timu, alikuwa akipita katikati yao kwa kueleza kwanini yeye ndiyo anafaa huku akiwaaminisha wana-Chadema kwamba ametumwa na mbingu kuja kukiongoza chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Baada ya matokeo kutangazwa, Januari 22, 2025, na Mbowe kukubali matokeo, Mwananchi limefanya mahojiano na Odero kuzungumzia mchakato mzima wa uchaguzi huo hadi ulipokamilika na kazi iliyo mbele yao.
Akizungumzia kura moja aliyoipata, Odero amesema kura hiyo haikuwa yake kama wengi wanavyodhani kwa sababu yeye siyo mjumbe wa mkutano mkuu, hivyo siyo mpigakura kama walivyokuwa Mbowe na Lissu ambao ni wajumbe wa mkutano mkuu.
Amesisitiza kwamba kura hiyo ina thamani kubwa kwake kwa sababu mjumbe aliyepiga kura hiyo anathamini kitu alichonacho na kwamba anaweza kuleta mabadiliko ndani ya chama, kwenye jamii na taifa kwa ujumla.
“Kura ile moja maana yake huyo mtu (aliyempigia) alithamini nilichocho, aliona kwa hiyo kura yake moja ina uwezo wa kuleta mageuzi ndani ya chama, una uwezo wa kuleta mageuzi ndani ya nchi.
“Kwa hiyo ni kura ambayo ina thamani sana, watu wanaweza wakaihesabu, wakaona haina thamani kwa sababu haikufanyi ushinde kuwa mwenyekiti lakini kwangu mimi ni kura ya thamani kubwa sana na ninamshukuru huyo aliyepiga hiyo kura,” amesema.
Odero ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu, amesisitiza kwamba thamani ya kura hiyo ni kwamba mtu huyo amemwamini kwamba anaweza, ana kitu ambacho anaweza akakifanyia chama, jamii na umma wa Watanzania.
Alitolea mfano kwamba Mungu alipoumba dunia, aliumba mtu mmoja, mtu huyo amesababisha mabilioni ya watu duniani. Amesema mtu mmoja mmoja wamekuwa wakifanya mabadiliko makubwa katika ulimwengu huu.
“Tunatumia kamera, mtu mmoja tu alitengeneza kamera. Unaona umeme unawaka, ni mtu mmoja alivumbua. Leo tunafurahia kuwa na mawasiliano ya simu, mtu mmoja alivumbua simu, leo watu wanafurahi.
“Mtu mmoja ana thamani kubwa, mtu mmoja ana uwezo wa kuiangamiza dunia, mtu mmoja ana uwezo wa kuitengeneza dunia kuwa salama,” amesema kada huyo wa Chadema mwenye makazi yake jijini Arusha.
Odero amebainisha kwamba kupata kwake kura moja siyo kwamba alishindwa kufanya ushawishi kwa wajumbe, bali ushawishi wake ulikuwa mikononi mwa wajumbe kuamua. Amewashukuru kwa kufanya uamuzi na kutoa jukumu la uenyekiti kwa Lissu.
“Kwa (wajumbe) kufanya hivyo, siyo kwamba wametuadhibu mimi na Mbowe, kwa sababu tulikuwa hatushindani, tulikuwa tumefika mbele ya wapigakura kuomba majukumu, bahati nzuri wajumbe wengi wamesema jukumu hilo kwa mwaka 2025 – 2029 wamempa Lissu,” amesema.
Anaamini katika maridhiano
Odero amesema anaamini katika maridhiano kwa sababu jamii yoyote inahitaji maridhiano ili kujenga ustawi
Amesema maridhiano kati ya CCM na Chadema yalikuwa na nia njema, lakini namna walivyoyaendea, ubinafsi ulitawala kwenye vyama hivyo vikubwa, wakaona mazungumzo hayo yawe yao pekee.
“Kwa maoni yangu, mazungumzo yale yaliyoanzishwa na Chadema, yalipaswa yaongeze wigo kwa sababu kilichokuwa kinajadiliwa ilikuwa ni kupata mwafaka wa nchi; masuala ya Katiba, ulinzi wa haki za binadamu, na rasilimali.
“Jambo la msingi lilikuwa baada ya Chadema kuanzisha ule mchakato wa mazungumzo na CCM na Serikali, walipaswa sasa waalike na wadau wengine; vyama vya siasa, viongozi wa dini, wazee mashuhuri na makundi yote muhimu katika jamii ili tupate mwafaka wa pamoja,” amesema.
Amesisitiza kwamba mwafaka utakaopatikana usiishie tu kwenye mazungumzo, bali upelekwe bungeni upate baraka za wabunge, ili uwe ni sheria.
“Jamii yoyote inapaswa wakati wowote kuishi maridhiano, hata binadamu mwenyewe huwa ana maridhiano na nafsi yake. Unaamka asubuhi unataka kuvaa T-shirt, nafsi inakwambia hapana, vaa shati, mwishowe unafikia mwafaka,” amesema Odero.
Baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa ndani, sasa chama hicho kinajielekeza kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 ambapo Odero anasema ni mapema kwake kutangaza nia ya kugombea ubunge ama la, kwa sababu kazi kubwa iko mbele yake.
Amesema sasa wana jukumu la kwenda kuhakikisha kwamba mabadiliko makubwa yanafanyika katika Tume ya Uchaguzi ili kupata tume itakayosimamia uchaguzi huo kwa uhuru na haki na Watanzania wafurahie demokrasia.
“Baada ya kumaliza uchaguzi wetu, tuanze sasa kuushirikisha umma kwa nguvu zote kudai mageuzi kwenye mifumo ya uchaguzi. Kila mwana-Chadema aone kwamba kampeni za kwenye uchaguzi mkuu ni leo,” amebainisha kada huyo wa Chadema.
Odero amesema anatamani kufikia Februari 2025, mgombea urais wa chama hicho apatikane na kufikia Machi, angalau robo tatu ya wagombea wa ubunge wapatikane. Kufikia Aprili, Amesema chama hicho kiwe kimemalizana na mchakato wa kutafuta wagombea urais, ubunge na udiwani.
“Lengo ni kufikia Juni 2025, tutoe mafunzo kwa wagombea wetu wote na baada ya hapo tuanze sasa kutafuta rasilimali fedha na vifaa kama magari kwa ajili ya kampeni kwa sababu naona Oktoba kutakuwa na mtiti mkubwa sana,” amesema Odero.
Odero amesema sasa ni wakati wa kila mwanachama kutoa “mkono wa pole” wa maridhiano kwa wenzao ambao wamekwazana baada ya kampeni za uchaguzi wa ndani ili wawe pamoja kwenda kukabiliana na chama tawala.
Amesema kwa ujumla uchaguzi wa chama hicho umekwenda vizuri licha ya kuwepo kwa dosari ndogondogo za wakati wa kampeni kwani baadhi ya watu walijisahau kwamba wako kwenye uchaguzi wa ndani, hata kampeni walizopaswa kuziendesha ni tofauti na kampeni zingine.
“Tunaposhinda uchaguzi wa ndani, uchaguzi wa maneno ni muhimu sana kwa sababu wote mnaoshindana ni watoto wa mama mmoja, baba mmoja, wote wa chama hicho hicho, kwa hiyo wagombea wote ni wa kwenu, hakuna unayeweza kumtilia ngumu na kumshambulia.
“Hiyo ni changamoto katika uchaguzi wetu wa ndani, lazima uwe mtu unayechagua sana maneno, usimuumize mwenzako kwa sababu uchaguzi unaisha asubuhi, mchana unamhitaji, uchaguzi ukiisha usiku, kukikucha unamhitaji,” amesisitiza Odero.