PIRAMIDI YA AFYA: Umomonyokaji mfupa waliofikia ukomo wa hedhi

Kitabibu Osteoporosis ni hali ya umomonyokaji msongamano wa madini yanayounda mfupa, hatimaye kuwa myepesi na dhaifu. Ni tatizo hili linalowaathiri zaidi wanawake waliofikia ukomo wa hedhi.

Ni hali ya mifupa kupoteza ubora wake, hasa katika tungamo ya mfupa, hii ni mara baada ya kupungua kwa molekuli pamoja na kuzorota utendaji wa kujiimarisha uimara wake.

Hali hii ndiyo chanzo kikubwa kuwa dhaifu hatimaye kuvunjika kirahisi, hata pale panapotokea shinikizo dogo la ghafla. Vihatarishi vya kupata tatizo hili ni pamoja na umri mkubwa miaka zaidi ya 40, kukoma kwa hedhi, upungufu wa madini na kushuka kwa viwango vya homoni, lishe duni, magonjwa ya mfumo wa chakula na saratani.

Vilevile magonjwa yanayoathiri uchakataji vitamini D inayosaidia kuimarisha mifupa, matatizo ya tezi, unywaji pombe kupitiliza, dawa za matibabu za steroids na kupungua utendaji kwa misuli.

Tatizo hili linawapata zaidi wanawake ambao tayari wana umri mkubwa ambao hedhi imekoma. Hii ni kutokana na kiwango chao cha kichochezi cha estrogen kupungua, hatimaye kuleta athari katika mfumo wa kinga wa mifupa.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kwa mwaka pekee zaidi ya watu milioni 10 huvunjika kutokana na tatizo hili. Wanaume hupata tatizo hili kwa asilimia 25 ukilinganisha na asilimia 75 kwa wanawake.

Ni ugonjwa ambao hauonyeshi dalili na viashiria mapema katika hatua za awali. Maeneo ya mwili ambayo ndiyo yanaongoza kuathirika na tatizo hili huwa ni nyonga, pingili chini ya mgongo na mifupa ya paja.

Tatizo hili, linalokadiriwa kuathiri zaidi ya watu milioni 200 duniani kote linatokana na utaratibu wa mifupa kupitia mizunguko ya urekebishaji ili kuleta uimara wake. Katika hatua hizo za mizunguko, zile tishu za zamani zilizochakaa au kuharibika hutengana na kubadilishwa na zile zilozo mpya zenye ustahimilivu dhidi ya mambo yanayoathiri afya ya mifupa. Tatizo linakuja mara baada ya miaka mingi kusonga, mchakato huo wa kubadili tishu za zamani unakuwa dhaifu au unakosa ufanisi wa kiutendaji. Hali hiyo ndiyo inayoleta matokea hasi, kwani seli zinazohusika na malezi ya afya ya mfupa zinashindwa kuwa mbadala wa seli chakavu au zilizoharibika katika mfupa.

Matokeo yake mfupa hupoteza tungamo na ubora wa tishu ngumu za mfupa kama sehemu ya mchakato wa kiasili wa tishu za mfupa kuzeeka kutoka na kanuni ya kutumika na kulika na huku pia umri ukiwa umekwenda.

Madhara mabaya ya tatizo hili ni pale mfupa unapokuwa dhaifu na kuvunjika kirahisi hata kwa shinikizo la kawaida. Hapa mgonjwa anakuwa katika wakati mngumu, kwani anahamia katika matibabu ya mfupa ambayo pengine atahitajika kufanyiwa upasuaji.

Kichochezi cha estrogen kinaathiri tungamo ya mfupa (uzito wa mfupa) na hatimaye uimara wa mfupa kupungua hivyo kuwa katika hatari ya kuvunjika hata kwa shinikizo la kawaida.

Kwa upande wa kichochezi cha kiume kijulikanacho kama Androjeni kina faida kwa mwili, kwani chenyewe kinaongeza unene na uimara wa mifupa. Lakini kiwango chake hupungua katika umri wa miaka 40-50.

Hapa unaweza kupata picha kuwa kumbe kihatarishi kikubwa kwa wanaume ni kutokana na umri kusonga na huku kwa wanawake ni kutokana na kukoma kwa hedhi ambapo inatokea katika umri wa 45-50.

Matibabu ya tatizo hili yanahusisha utoaji virutubisho na kubadili mwenendo mbaya wa lishe. Kufanya mazoezi mepesi inasaidia kuzuia uimara wa mfupa kupotea.

Tatizo linaweza kuzuiwa kwa kuepuka vihatarishi vilivyotajwa hapo juu. Kuzingatia lishe bora na kuacha matumizi ya tumbaku, unywaji holela wa pombe na dawa za steroids.

Related Posts