Musoma. Raia wa Ukraine, Ihor Hladkyi (48) amekutwa amefariki dunia baada ya kudaiwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya manila kwa sababu ambazo hazijajulikana.
Mtu huyo ambaye alikuwa anafanya kazi katika mgodi wa dhahabu unaomilikiwa na kampuni ya Polygold, uliopo katika eneo la Kigera Etuma wilayani Musoma, anadaiwa kujinyonga Januari 23, 2025, saa 2 asubuhi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Ijumaa, Januari 24, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amesema mtu huyo alikutwa amejinyonga kwa kamba aliyoifunga kwenye nondo za dirisha la chumba chake.
Lutumo amesema tukio hilo limetokea katika kata ya Mwisenge, manispaa ya Musoma katika chumba alichokuwa akiishi enzi za uhai wake.
Amesema jeshi hilo lilipokea taarifa za mtu huyo kujinyonga na walipofika eneo hilo, waliukuta mwili wa marehemu ukining’inia.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara, kwa kushirikiana na vyombo vingine, limeanza uchunguzi wa kina unaolenga kubaini hali na sababu halisi za tukio hilo,” amesema Lutumo.
Amesema wakati taratibu zingine zikiendelea, mwili wa mtu huyo umehifadhiwa katika hospitali ya Manispaa ya Musoma.
Amesema matukio ya watu kujinyonga pamoja na mambo mengine pia yanasababishwa na msongo wa mawazo na kwamba wanapopatwa na hali kama hiyo ni vema wakakutana na wataalamu wa afya ya akili ili kupata msaada wa kitaalamu.