Dar/Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa watendaji watatu katika halmashauri za wilaya tatu, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengera.
Wengine waliotenguliwa ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Meatu, Athuman Masasi na nafasi yake imechukuliwa na Zahara Michuzi aliyetokea Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
Stephano Kaliwa aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Nsimbo ametenguliwa na nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa Halmashauri ya Sengerema, Christina Bunini.
Utenguzi wa Mtahengera, unakuja miezi michache baada ya ugomvi wa mara kwa mara na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo kwa kile kinachoelezwa wanagombana katika masuala ya kazi.
Juni mwaka jana, Mtahengerwa alimtaja Gambo kuwa kikwazo cha kukamilika kwa miradi ya maendeleo kwa kuwa amekuwa akiingia katika migogoro na wataalamu wa halmashauri na madiwani.
Hata hivyo, Gambo alilikana hilo, akisema Mtahengerwa mwenyewe ameshindwa kuwasimamia watendaji wake.
Mtahengerwa pia, Aprili mwaka jana aliwahi kumtaka Gambo aache kile alichokiita siasa za maji taka, baada ya kulituhumu Jiji la Arusha kuhusika na ufisadi katika miradi ya maendeleo.
Kauli hiyo ya Mtahengerwa, ilitokana na hoja iliyoibuliwa bungeni na Gambo, akiutuhumu uongozi wa jiji hilo kuhusika na ufisadi katika miradi mbalimbali.
Pamoja na hayo, baadhi ya watendaji waliowahi kufanya kazi na Mtahengerwa wanasema ugomvi wake na Gambo si sababu za kutenguliwa kwake na kwamba wanachofahamu alifanya kila alivyoweza kutimiza wajibu wake.
Taarifa ya utenguzi wa watendaji hao, ilitolewa jana ikieleza nafasi ya Mtahengerwa imerithiwa na Joseph Mkude aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Kishapu.
Akizungumzia hatua hiyo leo Ijumaa Januari 24, 2025, Mkazi wa Arusha na kada wa CCM, Benard Henrico amesema anashawishika kuamini mamlaka ya uteuzi imefuatilia utendaji wake na kuamua kumtengua.
Amesema kutenguliwa huko hakupaswi kuhusishwa na mgogoro wake na Gambo.
“Nashawishika mamlaka ya utezi imefuatilia utendaji wa mtu ikaamua ilivyoamua,ila kuhusishwa na ugomvi baina yake na Gambo si sahihi,ninachokiona ni kwamba mamlaka ya uteuzi imeona inafaa kufanya mabadiliko hayo.
“Kimsingi malumbano yake na Gambo ni watu wameishi na kufanya kazi na Gambo muda mrefu,wanajuana vizuri hata wakati wanalumbana nilikuwa sioni jipya linaloweza kutokea kwa kila mtu kusema mwenzake ni dhaifu au ana makosa,” amesema.
Mwenyektii wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii ya Jiji la Arusha, Isaya Doita amesema amefanya kazi na Mtahengerwa kwa muda mrefu tangu alipokuwa Katibu Tarafa ya Themi, jijini Arusha.
Amesema anaamini Mtahengerwa amefanya kazi yake ikiwa ni uteuzi wake wa kwanza na kuwa alijitahidi kufanya kazi kadri ya uwezo wake licha ya Jiji la Arusha kuwa na mikiki mingi ikiwemo ya kisiasa.
Doita amesema Jiji la Arusha lina changamoto nyingi za kisiasa, wateule wa Rais dhidi ya wawakilishi wa wananchi.
“Kutokana na hilo kumpata mteule sahihi anayeweza kufanya kazi kwa mazingira ya aina hiyo anaweza kutawaliwa na nidhamu ya woga.
“Naamini hili ni jiji kubwa linahitaji mteule mwenye uzoefu, kuna mikiki mingi, tumekuwa tukishirikiana naye kwenye kazi na alikuwa mkuu wa wilaya wa kawaida anatoa ushirikiano.
“Ila Arusha hizi siasa tofauti za kisiasa kati yake na mbunge (Mrisho Gambo), wapo watakaosema inawezekana amefanikiwa kumtoa ila siamini hivyo.Naamini ni utaratibu wa kiutumishi tu, alijitahidi kufanya kazi tunashukuru kwani tumekuwa na utulivu na ushirkiano,” amesema.
Amesema kiongozi huyo alihitaji kulelewa, kuongzowa na kukanywa kwani alikuwa mchanga, labda angeanzia wilaya nyingine ndogo, kisha kwenda hapo.