Samia mgeni rasmi Siku ya Wanawake Duniani

Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yatakayofanyika kitaifa Machi 8, 2025, mkoani Arusha.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Januari 24, 2025, na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, wakati wa hafla ya makabidhiano ya pikipiki zilizotolewa kwa Jeshi la Polisi ili kuimarisha usalama mkoani humo.

Amesema maadhimisho ya mwaka 2025 yatakuwa tofauti, yakihusisha shughuli za siku tatu hadi nne kama maonyesho ya biashara za wanawake, mechi za wanawake na burudani mbalimbali.

“Ninawaomba akina mama, hiyo siku ikitokea umebaki nyumbani, labda uwe unaumwa au umri wako ni mkubwa. Ukiwa mzima, njoo tuungane kusherehekea mafanikio ya wanawake tukiongozwa na Rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania,” amesema Makonda.

Aidha, ameongeza kuwa Mwenyekiti wa Leopard Foundation, chini ya kampuni ya utalii ya Leopard Tours, Mustapha Lalji, amejitolea kusaidia matibabu kwa wagonjwa wasiojiweza kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Huduma hizi zitatolewa kwa wagonjwa watakaojitokeza na kuthibitishwa na Katibu Tawala wa Mkoa na Mganga Mkuu wa Mkoa, ambapo kampuni hiyo itagharamia matibabu kwa asilimia 100.

“Sisi hiki ndiyo kitu tunatamani, mfanyabiashara kufanya biashara bila kubughudhiwa na michango. Tunashukuru kwa msaada huu kwani kuna watu wengi wenye hali ngumu,” amesema Makonda.

Related Posts