TRA ENDELEENI KUPAMBANA NA WAKWEPAKODI.: RAIS SAMIA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha wanaendelea kupambana na watu wanaokwepa Kodi kwa kuwasaka wanaoghushi risiti za EFD na VFD pamoja na wanaotumia Stempu bandia kwenye vinywaji.

Pia amewataka Walipakodi nchini kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kuachana na vitendo vya kukwepa Kodi ambavyo vinaondoa usawa wa ushindani sokoni.

Rais Samiah amesema hayo Januari 23, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utolewaji wa Tuzo za Mlipakodi kwa mwaka 2023/2024.

Amesema Tuzo hizo zinaongeza chachu ya ulipaji wa Kodi kwa hiari na kuwataka wenye tabia za kukwepa kodi kuacha mara moja kwani wanadhoofisha Uchumi wa nchi na kuwavunja moyo walipakodi waaminifu kwa kuweka ushindani usiokuwa sawa sokoni.

Dkt. Samia amesema mwelekeo wa Serikali ni kuongeza idadi ya walipakodi na siyo kuwatumia wachache waliopo na hilo litafanikiwa kwa kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iwe rasmi na kulipa Kodi kikamilifu.

Amesema inajulikana kuwa dhuruma siyo kitu kizuri, wale wote wanaokwepa Kodi wajue kuwa wanafanya dhuruma na hata watumishi wa TRA wanaofanya makadirio yasiyokuwa sahihi nao pia wanafanya dhuruma hivyo amewaasa kuacha mara moja kufanya hivyo na kuwataka kwenda kutenda haki kwa kila mmoja.

Amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM inaitaka nchi ipunguze utegemezi na utegemezi huo utapungua kwa kusimamia kwa usahihi ukusanyaji wa Kodi jambo ambalo litaifanya Tanzania ijiamini.

“Bajeti ya Serikali ni Sh. Trilion 49.34 miongoni mwa fedha hizo Sh. Trilion 30.4 sawa na asilimia 61.6 inatokana na makusanyo ya Kodi kutoka kwa TRA hiyo ndiyo inaonyesha tunavyoundea kujitegemea hivyo ongezeni juhudi katika kukusanya Kodi.” Amesema Rais Samiah

Rais Samia ameongeza kuwa Mwaka ujao 2025/2026 hakutakuwa na Tuzo za Mlipakodi za TRA bali kutakuwa na Tuzo za Rais ili kuonyesha umuhimu wa kulipa Kodi na zitakuwa na hadhi ya Rais na zitaandaliwa na ofisi ya Rais

“Kwenye masuala ya Kodi hakuna mzaha, mtu asijifanye kwamba ana maelekezo kutoka juu asilipe Kodi, napenda kuwaambia hakuna mtu yoyote niliyemruhusu asilipe Kodi na Mimi ndiyo ngazi ya juu ya mwisho, kama nitamruhusu mtu yoyote nitatoa maagizo kwa maandishi ” Rais Samia

Akizungumzia kesi za kikodi, Rais ameitaka Bodi ya rufani kuharakisha usikilizaji wa kesi hizo ili Kila mmoja apate haki yake.

Rais Samia ametoa rai kwa watumishi wa TRA kufanya kazi kwa uaminifu, kudumisha nidhamu kwa kuwa na mienendo mizuri kazini ili kuwajengea Imani Walipakodi.
 

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepewa tuzo ya kumshukuru kwa kuunga mkono uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa hiari na kurahisisha ukusanyaji wa mapato kwa mwaka 2023/2024.
Tuzo hiyo imetolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Januari 23,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa Hafla ya utolewaji wa Tuzo kwa Walipa kodi iliyofanyika katika ukumbi wa The Super Dome- Masaki


Related Posts