Dar es Salaam. Uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump wa kuzuia misaada ya maendeleo kwa siku 90, umeanza kuleta maumivu katika maeneo kadhaa, hususan ajira na utekelezaji wa miradi kama elimu na kilimo nchini.
Mbali na hiyo Trump pia ameeleza nia yake ya kuitoa Marekani kwenye Shirika la Afya Duniani (WHO), hatua hii itaathiri baadhi ya asasi za kiraia na mashirika ya misaada ambayo yamekuwa tegemeo kwa utekelezaji wa miradi ya kijamii.
Uamuzi huo unaleta changamoto kwa baadhi ya Watanzania, lakini pia unatoa fursa ya kujifunza na kuimarisha uwezo wa kujitegemea.
Akizungumzia na Mwananchi kuhusu hofu ya kukosa ajira kutokana na uamuzi huo wa Trump, Esther Jackson (sio jina lake halisi), mmoja wa mameneja wa mradi wa elimu ya afya ya uzazi jijini Dar es Salaam, amesema hatua hiyo imewaacha wafanyakazi wengi katika hali ya sintofahamu.
“Baada ya maagizo yale, tulitangaziwa ofisini kuwa miradi tuliyokuwa tunaitekeleza itasimama kwa muda. Kwa sasa tumeambiwa hatuna haja ya kwenda kazini mpaka pale tutakapofahamishwa vinginevyo,” amesema Jackson.
Amesema tayari hali hiyo imesababisha wasiwasi kwa wafanyakazi kuhusu malipo yao ya mshahara na mustakabali wa miradi.
Jackson amesema kuna matumaini madogo ya kupokea mshahara wa mwezi huu na pengine ujao, lakini hofu yake kuu ni kuhusu uendelevu wa mradi huo.
“Sera za Trump hazionekani kuipa kipaumbele sekta yetu, hivyo tunasubiri kwa wasiwasi kuona hali itakavyokuwa,” ameongeza.
Mwingine aliyeathirika ni mfanyakazi wa asasi inayosimamia miradi ya uzazi wa mpango jijini Mwanza, ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Amesema ingawa bado wanaendelea kwenda ofisini, ila tayari utekelezaji wa miradi umesimama.
“Hatuendi field (maeneo ya utekelezaji wa miradi) kwa sasa. Shughuli zetu zimejikita zaidi vijijini, lakini kwa sasa tumesimamisha shughuli hizo,” amesema.
Kuhusu kuathirika kwa sekta ya kilimo, Mkurugenzi Mtendaji wa Malembo Farm, Lucas Malembo akizungumza na Mwananchi amesema Tanzania itakumbwa na changamoto kubwa hasa kwenye tafiti za kilimo, zinazofadhiliwa kwa kiasi kikubwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).
“Fedha nyingi kutoka USAID zilienda kwenye tafiti. Bado tunatakiwa kukua zaidi katika sekta ya kilimo kupitia tafiti, lakini sasa tupo hatarini kurudi nyuma. Pia, masoko ya kimataifa tuliyokuwa tumeanza kuyafikia yanaweza kuathirika pia,” amesema Malembo.
Kwa mujibu wa Malembo, mashirika mengi yanategemea misaada kutoka Marekani, hususan kwa miradi ya kilimo inayowalenga wanawake na vijana.
“Mashirika kama SUA (Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine) yamekuwa yakifanya kazi kubwa kuboresha kilimo nchini kupitia msaada huu. “Sasa ni wakati wa kujifunza kujitegemea zaidi katika sekta hii,” amesisitiza.
Pia, Serikali na wadau wa maendeleo wametakiwa kuona umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza utegemezi kwa msaada wa kigeni na kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea kutolewa bila kukwama.
Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Dk Luka Mkonongwa ameonya kuwa lazima Tanzania ijifunze kujitegemea.
“Tupunguze matumizi yasiyo ya lazima serikalini ili fedha hizo ziweze kusaidia sekta ya elimu. Tukitegemea misaada pekee, tutayumba pale mfadhili anapoyumba,” amesema Dk Mkonongwa.
Amesema ni wakati sahihi kwa Tanzania kujitafakari na kuweka mikakati ya kujitegemea, akitolea mfano wa nchi ya Burkina Faso ambayo imejiondoa kwenye utegemezi wa misaada na mikopo ya kigeni.
Kwa upande wake, Muhanyi Nkoronko, ambaye ni mdau wa elimu nchini, amesema miradi mingi inaweza kusuasua au kusimama kabisa endapo tathmini itafanyika na ikabainika kuwa haina faida kwa Marekani.
“Programu zilizokuwa zikiendelea zinaweza kushindwa kufanyika na athari kubwa itakuwa kwa wananchi wa maeneo husika watakaozidi kukosa huduma na ajira,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inapaswa kuja na mpango wa dharura kuhakikisha huduma zenye umuhimu mkubwa zinaendelea kutolewa.