USAFIRI WA TRENI YA MWENDO KASI (SGR) UMEKUWA MKOMBOZI KWA WANANCHI WENGI- MSIGWA.

Na Janeth Raphael MichuziTv

Imeelezwa kuwa tangu kuanza kwa usafiri wa treni ya mwendo kasi (SGR) Imeonyesha mafanikio makubwa kwani safari ya treni kati ya Dar es Salaam na Dodoma, ambapo zaidi ya abiria milioni 1.5 wameshasafiri kwa usafiri huo wa kisasa tangu kuanza kwakwe mwaka jana 2024, mwezi wa sita ambao umekuwa mkombozi kwa Wananchi walio wengi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na michezo na Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa, ameyabainisha hayo leo Jijini Dodoma katika Stesheni ya Dodoma yenye jina la Samia Suluhu Hassani alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Hifadhi ya Taifa (TANAPA) Mkoani Morogoro.

Amesema kuwa wastani wa abiria laki tatu husafirishwa kila mwezi, huku huduma za treni zikihimili mahitaji kwa kuwa na miundombinu ya kutosha na inayoendelea kuboreshwa.

“Tunasafirisha wastani wa abiria laki tatu kwa mwezi. Treni zenyewe zinakwenda vizuri na tunazo treni za kutosha kukidhi mahitaji. Kwa sasa tuna vichwa vya treni 17 na mabehewa ya abiria zaidi ya 70, ambayo yanaongezeka hadi kufikia 80, na mengine zaidi yanatarajiwa kuwasili,” Msigwa.

Aliongeza kuwa hakuna upungufu wa treni, huku akisisitiza kuwa changamoto zinazojitokeza ni ndogo na hazihusiani moja kwa moja na mradi huo.

“Treni zinafanya kazi vizuri, na changamoto ndogo ndogo hazina uwezo wa kurudisha nyuma mradi huu. Kipande cha kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kisha Dodoma kinaendelea vizuri, na Watanzania wanafurahia huduma hii,” aliongeza.

Kuhusu usafirishaji wa mizigo, Msigwa alisema maandalizi yanaendelea, na tayari mabehewa 264 ya mizigo yameingia nchini, huku mengine 264 yakiwa bandarini, yakitarajiwa kuanza kazi muda si mrefu.

“Kazi ya ujenzi wa vipande vingine vya reli inaendelea, kuanzia kipande cha Dar es Salaam–Morogoro, Morogoro–Dodoma, hadi vipande vitakavyofuata. Mradi huu ni uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na tunakwenda vizuri,” alisema.

Hata hivyo Msigwa alihimiza Watanzania kufahamu kuwa mradi wa SGR ni wao, na Serikali imedhamiria kuhakikisha unakamilika kwa gharama ya zaidi ya dola bilioni 10 za Marekani (takriban shilingi trilioni 23).

“Mheshimiwa Rais amedhamiria kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa mafanikio makubwa,” alihitimisha.






Related Posts