Ushindi wa Lissu wawaweka maofisa Chadema matumbo joto

Dar es Salaam. Ushindi wa Tundu Lissu katika nafasi ya uenyekiti wa Chadema unatazamwa kufufua upya kishindo cha siasa za upinzani, huku ukiwaweka matumbo joto baadhi ya makada na maofisa katika kurugenzi za chama hicho.

Lissu alichaguliwa mwenyekiti wa Chadema Januari 21, mwaka huu akipata kura 513 dhidi ya mwenyekiti wa muda mrefu, Freeman Mbowe aliyepata kura 482, katika uchaguzi uliotanguliwa na kampeni zilizokuwa na kila aina ya ushindani.

Ingawa ushindi huo umetabiriwa kuwa mwanzo mzuri wa kushuhudia kishindo cha siasa za upinzani, wapo wanauona kuwa hatari kwa nafasi zao, hasa baadhi ya makada na maofisa katika kurugenzi cha chama hicho.

Hofu zilizopo zinachochewa na ukweli kwamba, katika uongozi wake, Lissu atapanga safu mpya katika kurugenzi za chama hicho na inaelezwa tayari anafikiria kuzifumua kisha kuteuwa watendaji wapya.

Maofisa, kurugenzi kusafishwa

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya uongozi wa sasa kimeweka wazi kuwa, baada ya uteuzi wa nafasi za juu katika sekretarieti ya chama hicho, kinachofuata ni usafi katika kurugenzi na maofisa wa chama.

Kurugenzi za Chadema ziko tano – Fedha, Uwekezaji na Utawala, Sheria na Haki za Binadamu na Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje.

Katika kurugenzi, chanzo hicho kimesema kitakachofanyika ni kuzifumua ili ziwe na muundo mpya, kisha watateuliwa viongozi wapya wa kuziongoza.

“Kwanza zitafumuliwa kurugenzi zilizopo na kuundwa mpya baada ya kujua zitakuwa ngapi, kisha watateuwa watu kwa ajili ya kuziongoza,” kilieleza chanzo hicho.

Chanzo hicho, kilidokeza katika ofisi ya makao makuu ya chama hicho, ukiachana na Katibu Mkuu, John Mnyika maofisa wengi wataondolewa.

Kujulikana nani ataongoza kurugenzi gani na muundo wa kurugenzi husika, chanzo hicho kimesema itakuwa Februari katika kikao cha Kamati Kuu.

Baadhi ya makada wanalalamikia ushindani uliokuwepo kabla na wakati wa uchaguzi, kuwa umegeuka uadui kati ya upande uliokuwa unamuunga mkono Lissu na ule wa Mbowe.

Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa viongozi wa chama hicho aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina akihofia nafasi yake, alisema kumekuwepo baadhi ya viongozi wanawatishia kufanya figisu za kuwaondoa wenzao kwa kuwa hawakuwa wanamuunga mkono Lissu wakati wa uchaguzi.

“Kuna kiongozi amemwambia mwenzake kabisa kwamba nitafanya kadri itakavyowezekana kuhakikisha nakuondoa kwenye nafasi ya uongozi, ukapumzike na Mbowe uliyekuwa unamuunga mkono,” alisema.

Yote hayo, alisema yamechochewa na lugha zilizokuwa zinatumika wakati wa kampeni na hata baada ya uchaguzi hakukuwa na maneno ya uponyaji, hivyo kumekuwa na vita vya timu mbili.

“Kuna harakati zimeanza chini kwa chini za kufukuza uanachama watu waliokuwa wanamuunga mkono Mbowe na sioni jitihada zinazofanyika kuhakikisha mambo yanakwenda kuwa sawa,” ameeleza kada huyo.

Iwapo mambo hayo yataachwa yaendelee, alisema utafika wakati itashindikana kuyadhibiti na huo ndio utakaokuwa mwelekeo mbaya kwa ustawi wa chama hicho, ameonya bila kutaja majina ya wahusika.

Ingawa hakutajwa jina, huenda aliyekuwa anatajwa na kada huyo John Mrema, mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, ambaye kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X juzi Alhamisi, alichapisha ujumbe akiahidi kuzungumza leo “kwa kinywa kipana”.

“Keshokutwa Mwenyezi Mungu akinijalia nitasema kwa kinywa kipana sana! Taasisi ni muhimu sana! Matusi na kejeli havijengi! Kuishi ughaibuni hakujengi!,” ameandika Mrema.

Ujumbe wake huo, ulifuatiwa na ujumbe mwingine alioandika kuwa amejulishwa kuhusu kuwepo nia ya kumfuta uanachama iwapo ataendelea na mpango wa kuzungumza na vyombo vya habari.

“Nimejulishwa na mwenyekiti wa tawi langu ameagizwa anifute uanachama kabla ya kesho, ili kama nitaendelea na nia yangu ya kuzungumza na vyombo vya habari basi niwe sio mwanachama,” amesema.

Kwa mujibu wa Mrema kupitia ujumbe huo, ameeleza kushangazwa na nia hiyo aliyodai inaratibiwa na viongozi.

“Wanademokrasia wameshinda uchaguzi, sasa hawataki wengine tuseme, wanataka kufukuza wengine uanachama ili wasisemwe,” ameandika Mrema.

Sambamba na hilo, ameandika demokrasia ni pamoja na uhuru wa mawazo na kutoa maoni, huku akisisitiza Chadema ndicho chama chake na hakuja kuwa mwanachama wa chama kingine chochote.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mrema amekiri ujumbe huo kwenye ukurasa wa mtandao wa X ni wa kwake.

Amefafanua taarifa zilitoka kwa Mwenyekiti wa Tawi anakoishi, Reuben Kagaruki aliyemwambia ameamrishwa na Mwenyekiti wa Kata ya Segerea kifanyike kikao cha kumfuta uanachama.

Ameeleza lengo la hatua hiyo ni nia yake ya kufanya mkutano na waandishi wa habari itimie wakati akiwa si mwanachama.

Mzizi wa mzozo huo ni kuendelea kwa kauli za kubeza dhidi ya Mbowe.

“Kauli hizo hazipaswi kuendelea kutolewa kwani ameshaondoka ofisini, uongozi mpya ujipange kukiunganisha chama na kuvunja makundi badala ya kuendelea kuwa na kauli ambazo hazijengi umoja na mshikamano,” alisema.

Hata hivyo, amesema yapo mengine aliyopanga kusema katika mkutano na waandishi wa habari lakini ameamua kutoyasema baada ya kushauriwa na watu mbalimbali atulie.

“Niliyopanga kusema bado nitayasema siku nyingine, nimepokea ushauri wa watu mbalimbali kuwa nitulie vumbi litulie kwanza, nami nimekubaliana na ushauri huo kwa masilahi mapana ya taasisi yetu,” amesema Mrema.

Alipotafutwa kuzungumzia madai hayo leo Ijumaa, Januari 24, 2025, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema hakuna ukweli katika yote yanayozungumzwa, ni maneno ya kutungwa.

“Kama kuna anayesema ametishiwa kufutwa uanachama, kwa mfano Mrema, muulize mwenyewe imekuwaje, amefutwa?

“Lakini kuhusu malalamiko ya watu wengine ni maneno ya kutungwa, ni uongo, hayana ukweli wowote,” amesema Mnyika.

Akizungumzia hali hiyo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo amesema ni muhimu kujiuliza aliyetishiwa ametishiwa na nani? Ametoa ushahidi wa hivyo vitisho na waliomtisha wana mamlaka hayo?

Pia, alisema ni vema kujiuliza upi utaratibu wa Chadema katika kumvua mtu uamachama, kuna mahali kikao chochote kimefanyika?

Dk Masabo ameeleza katika mazingira ya sasa baada ya uchaguzi, waliokuwa wanamuunga mkono Mbowe kuwa na wasiwasi ni jambo la kawaida kibinadamu, ingawa halipaswi kukuzwa kiasi hicho.

“Siamini kama Tindu Lissu anaweza kufanya siasa hizo, hata kama inalazimu kumfukuza, mtu yule ni mkurugenzi nadhani mamlaka yake ya kinidhamu hayapo kwenye tawi,” amesema alipozungumzia malalamiko ya Mrema.

Amefafana hata kungekuwa na haja ya kumfukuza Mrema, huu sio wakati mzuri kisiasa kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa Dk Masabo, kwa sasa kunaweza kuwa na mpango wa kubadili wakurugenzi tu na sio kufukuzwa uanachama.

Sambamba na hilo, mwanazuoni huyo amesema kwa hali ilivyo inaonekana kuna upande haukutarajia kushindwa uchaguzi.

“Mimi natamani kwanza tupate hoja za Mrema. Tukizipata tunaweza kudadavua kama zina mashiko ya kuweza kuharibu mambo au tunaweza kusema kwa msemo wa wazungu, kuwa “… is a kick of a dying horse (teke la farasi anayekufa)” au waswahili wasemavyo “… mfa maji haachi kutapatapa” alisema Dk Masabo.

Related Posts