Kibaha. Mtoto mchanga mwenye umri wa miezi saba, Merysiana Melkzedeck, aliyeibwa Januari 15, 2025 katika eneo la Kwa Mfipa, Kibaha mkoani Pwani, amepatikana porini akiwa hai.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 24, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase amesema kupatikana kwa mtoto huyo kumetokana na ushirikiano wa pamoja na mamlaka zingine na taarifa kutoka maeneo mbalimbali.
Kamanda Morcase amesema baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza msako maeneo tofauti ndani na nje ya mkoa huo na leo Januari 24, 2025, saa 9 usiku, walifanikiwa kuwakamata watu watatu wakiwa na mtoto huyo ndani ya pori la Kimara Misare lililopo Mlandizi mkoa wa Pwani.
“Tumewakamata watuhumiwa watatu, mmoja ni mwanamke, wakiwa na mtoto huyo lakini pia tumekamata gari, simu moja na kompyuta mpakato, vyote mali za baba wa mtoto huyo,” amesema.
Amesema baada ya kumpata mtoto huyo, wamempeleka hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani (Tumbi) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kiafya.
Ameongeza kuwa wanaendelea na msako katika maeneo mbalimbali ili kumpata mtu mmoja ambaye alishirikiana na wenzake waliokamatwa kufanya tukio hilo.
“Hali ya mtoto ni nzuri baada ya kufanyiwa uchunguzi, tutamuunganisha kwa wazazi wake,” amesema.
Amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa jeshi hilo zitakazoongeza wepesi wa kupatikana kwa mtuhumiwa ambaye hajapatikana ili wahusika hao wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Watuhumiwa hao, wanadaiwa siku ya tukio wafika nyumbani kwa familia ya mtoto huyo, saa 12 asubuhi na kumvamia baba wa mtoto huyo na kumuamuru awape fedha.
Kwa mujibu wa baba huyo, Melkzedek Sostenes, watuhumiwa hao walimshambulia kisha wakawatumbukiza kwenye mashimo ya vyoo, yeye na mkewe, ambapo baadaye waliokolewa na majirani baada ya saa kadhaa, wakaondoka na mtoto, simu, kompyuta na gari.