Rukwa. Wavuvi 550 waliokuwa wanafanya shughuli za uvuvi katika Ziwa Rukwa wameokolewa na wengine 10 wakiendelea kutafutwa kufuatia upepo mkali uliotokea jana 23 Januari 2025 katika ziwa hilo lililopo Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Kufuatia tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amefika katika Kata ya Nankanga kuungana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji kujionea kazi ya uokozi, huku akiwa ameambatana na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga pamoja na askari wazamiaji.
Akitoa taarifa ya tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbwanga, Nyakia Chirukile ameeleza kuwa Januari 23, mwaka huu jumla ya wavuvi 550 kutoka Kata ya Nankanga na Mtowisa waliokuwa wanaendelea na shughuli za uvuvi ndani ya Ziwa Rukwa, walipatwa na dhoruba ya upepo mkali uliosababisha madhara kwao.
DC Chirukile amesema kuwa jitihada za uokozi zinazoendelea kufanywa na wananchi wakishirikiana na Jeshi la Zimamoto wa Uokoaji ambapo kufikia leo kufikia saa moja usiku, wavuvi 10 bado hawajapatikana
“Niwatake wananchi kuchukua tahadhari pindi wanapoona dalili za mvua ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza,” amesema DC Chirukile.
Akitoa salama za pole, Waziri Bashungwa amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kupata taarifa hizo, ametoa helkopta ya jeshi iliyoambatana na wazamiaji na vifaa maalum vya uokozi ili kuongeza nguvu za uokoaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvu, Dk Ashatu Kijaji ametoa pongezi kwa wananchi kwa kushiriki kikamilifu katika uokoaji pamoja na kutoa ushirikiano wa kuwatambua wavuvi wengine ambao walikuwa hawajasajiliwa katika vikundi na kampuni.
Mmoja wa wananchi, Edson Juakali, amesema amempoteza shemeji yake katika tukio hilo, huku akiliomba Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuongeza nguvu kuwatafuta wavuvi ambao bado hawajapatokana.
Jumla ya wavuvi waliokuwa katika ziwa hilo ni 550 ambapo 540 kati yao wameokolewa na wengine 10 wakiwa bado hawajapatika ambapo juhudi za kuwaokoa bado zinazoendelea.
Ikumbukwe Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitangaza kuwepo na mvua za chini ya wastani hadi juu ya wastani zitakazotarajiwa kuwa na matukio ya hali mbaya ya hewa, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
TMA ilisema vipindi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, yanayoweza kusababisha uharibifu wa miundombinu, mazingira, mlipuko wa magonjwa pamoja na upotevu wa mali na maisha.
Mvua hizo zinatarajia kunyesha msimu wa masika Machi- Mei 2025 za chini ya wastani hadi wastani ni maeneo ya mikoa ya Pwani, Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Morogoro, Tanga, Dar es Salaam na visiwa vya Unguja na Pemba.
Hata hivyo, mikoa inayopata mvua za wastani hadi juu ya wastani ni mashariki mwa mikoa ya Simiyu na Mara.
Endelea kufuatilia Mwananchi.