Dar es Salaam. Barabara tisa jijini Dar es Salaam, zimefungwa kwa siku sita kuanzia leo Januari 25 hadi Januari 30, 2025 ili kupisha misafara ya viongozi wanaokuja kutoka nchi mbalimbali kuhudhuria mkutano wa Nishati Afrika.
Pia, bajaji na bodaboba hazitaruhusiwa kuingia katikati ya jiji katika kipindi chote ambacho mkutano huo utakuwa ukifanyika.
Mkutano huo utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Januari 27 hadi Januari 28, 2025, unatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya marais 25 na mawaziri 60 kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Taarifa ya Polisi iliyotolewa leo Jumamosi Januari 25,2025 na Kamanda Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Jumanne Muliro, imesema kutokana na ugeni huo, barabara hizo zitafungwa kuanzia leo.
Amezitaja barabara zitakazofungwa kuwa ni Nyerere kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwenda katikati ya Jiji.
Nyingine ni Barabara ya Sokoine, Kivukoni na Lithuli kuanzia taa za Gerezani kwenda Hoteli ya Johari Rotana, Hyatt Regency hadi Ikulu.
Pia ipo Barabara ya Ohio kutokea Kivukoni kwenda Hoteli ya Serena na ile ya Ghana kutokea barabara ya Ohio kwenda Hoteli ya Onomo
Vilevile Barabara ya Bibi Titi kutokea makutano ya Barabara za Ohio na Ally Hassan Mwinyi kwenda Hoteli ya Crowne na Barabara ya Azikiwe kwenda Hoteli ya Four Points, Hoteli ya Golden Tulip City Center na Hoteli ya Holiday Inn.
Pia, ipo Barabara ya Morogoro kutokea Sokoine kwenda Hoteli ya Tiffany No. 1 na ile ya Makunganya kutokea Azikiwe kwenda Hoteli ya Tiffany No. 2.
Aidha Barabara ya Garden kutokea Barabara ya Lithuli kwenda Hoteli ya Southern Sun pamoja na Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa JNICC nayo itafungwa kutokana na ugeni huo.
“Katika kipindi chote cha Mkutano huu watumiaji wengine wa barabara mnashauriwa kutumia Barabara za Uhuru, Kawawa kupitia Magomeni, Kigogo kuelekea Temeke, Barabara ya Morogoro na Msimbazi, Morogoro na Lumumba.
“Kwa wale wanaotokea maeneo ya Chanika wanashauriwa kutumia njia mbadala ya mradi ya SGR ili waje kutokea barabara ya Mandela na Uhuru,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa: “kwa sababu za kiusalama wale wanaotumia vyombo vya moto kama pikipiki za magurudumu mawili (bodaboda) na magurudumu matatu (bajaji) vyombo hivyo havitaruhusiwa kuingia katikati ya jiji kwa muda ambao umetajwa wakati wageni hao wakiwa bado wapo.”
Badala yake wameshauriwa na kuelekezwa kuishia daraja la Salender kwa kwa barabara ya Ally Hassani Mwinyi wataishia
Huku kwa wale wanaotumia Barabara ya Morogoro wataishia Jangwani na kwa wa Barabara ya Kawawa kutokea Magomeni wataishia Kigogo sambusa.
Kwa wale wa Barabara ya Uhuru kutokea Buguruni wataishia Ilala Boma na kwa Barabara ya Nyerere kutokea Airport na Veta wataishia taa za Veta. Wakati wa barabara ya Kilwa wataishia Mivinjeni.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam linatoa wito kwa wananchi kufuata utaratibu huu na Jeshi la Polisi litajitahidi kuzisimamia hizo njia mbadala ili kupunguza msongamano kwa kadri itakavyowezekana.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam linawatakia Wananchi wote mapokezi mazuri kwa wageni hao,”imesema sehemu ya taarifa hiyo.