BARABARA ZA BRT KURAHISISHA USAFIRI WA MISAFARA YA VIONGOZI WA MKUTANO WA NISHATI AFRIKA

 

Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, leo Jumamosi, Januari 25, 2024, amekagua miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Tatu, ambayo inayoanzia katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Gongolamboto kupitia Barabara ya Nyerere. Barabara hiyo imepewa kipaumbele maalum kwa maandalizi ya kuwakaribisha viongozi wa nchi mbalimbali watakaoshiriki Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika, unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam.

Katika ziara yake, Waziri Ulega ametoa maelekezo mahususi ya kuhakikisha usafiri wa misafara ya viongozi, wakiwemo marais, unakuwa rahisi na wa haraka. 

Waziri Ulega ametangaza kuwa, barabara ya mabasi yaendayo haraka kuanzia Airport hadi Katikati ya Jiji itatumiwa kwa misafara hiyo, huku wananchi wakitumia barabara za pembeni kuendeleza shughuli zao bila usumbufu.

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imetekeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara za Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kwa awamu nne hadi sasa huku awamu nyingine mbili zikiwa njiani kuanza kutekelezwa. 

Hadi sasa, ujenzi wa awamu ya tatu ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) umekamilika kwa zaidi ya asilimia 70, na unatarajiwa kupunguza msongamano wa magari jijini. 

Waziri Ulega amepongeza jitihada za TANROADS na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila, kwa kusimamia mradi huo kikamilifu na kujipanga vyema wakati wote wa mapokezi kwa kurahisisha usafiri kupitia miundombinu hiyo. 

Aidha, Waziri amesisitiza matumizi ya taa za barabarani zinazotumia nishati ya jua ili kuokoa umeme kwa matumizi mengine muhimu kama viwandani.

 Hatua hiyo inathibitisha dhamira ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha miundombinu inaboresha uchumi wa nchi na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema katika kuimarisha mazingira ya kibiashara,  zoezi la uwekaji wa taa za barabarani kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hadi katikati ya Jiji linaendelea kwa kasi na kwamba taa hizo siyo tu zitatumika wakati wa misafara ya viongozi wanaokuja katika mkutano bali pia ni sehemu ya maandalizi ya mpango wa kuzindua masoko yanayofanya kazi kwa saa 24. 

Hatua hiyo, pamoja na mifumo ya kamera za usalama, inalenga kuboresha usalama na kuwezesha biashara kustawi zaidi katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi za Afrika, unaotarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 3,000, unaleta fursa za kiuchumi, utalii, na kuimarisha sifa ya Tanzania kama taifa la amani na utulivu.

Related Posts