YANGA leo ilikula kiporo cha mechi za Kombe la Shirikisho kiulaini baada ya kuifumua Copco ya Mwanza kwa mabao 5-0, huku nyota mpya wa kikosi hicho, Jonathan Ikangalombo ‘Ikanga Speed’ akishindwa kuanza kuitumikia timu hiyo baada ya kuanzishwa jukwaani na Kocha Sead Ramovic.
Wakati Ikanga Speed akianzia jukwaani, beki wa kulia Israel Mwenda aliyesajiliwa katika dirisha dogo kama ilivyo kwa winga huyo Mkongoman alianza pambano hilo na ‘kumwaga’ maji ya kutosha yaliyosaidia Yanga kutoka na ushindi huo wa kishindo mbele ya timu hiyo ya First League.
Katika pambano hilo la hatua ya 64 Bora lililopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam, kocha Ramovic alimwanzisha Mwenda aliyetua kutoka Singida Black Stars, sambamba na nyota wanaoanzia benchi akiwamo Jonas Mkude aliyecheza kama beki wa kati sambamba na nahodha Bakar Mwamnyeto. Wengine walioanza mchezo huo kabla ya baadhi ya kutolewa kipindi cha pili ni kipa Abuutwalib Mshery, Nickson Kibabage, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Duke Abuya na Farid Mussa, huku Stephane Aziz Ki na Prince Dube wakiwa nyota pekee wa kikosi cha kwanza walioanza mchezo wa leo.
Dakika 45 za kwanza Copco inayoshika nafasi ya saba katika Kundi B la First League ikiwa na pointi tano tu katika mechi saba iliyocheza ikifunga mabao matano na kufungwa 10, ilicheza kwa kujiamini na kuifanya Yanga isitembeze lile boli la Gusa Achia Twende Kwao.
Licha ya kwamba wachezaji wa timu hiyo hawakupata nafasi ya kulifikia lango la Yanga na kumpa likizo ya muda mrefu kipa Mshery, lakini katika eneo lao la ulinzi na katikati waliibana Yanga iliyokuwa ikitegemea mashambulizi ya mabeki wa Kibabage na Mwenda sambamba na Aziz KI.
Hata hivyo, kona iliyopigwa na Farid Mussa dakika ya 35 ilitua kichwani mwa Shekhan na kuandika bao la kwanza lililodumu hadi wakati wa mapumziko.
Kabla ya kuanza kipindi cha pili, Kocha Ramovic alifanya mabadiliko ya wachezaji wawili akiwatoa viungo Stephane Aziz Ki na Shekhan Khamis, wakaingia mabeki Dickson Job na Kibwana Shomari.
Mabadiliko hayo yalilenga kubadilisha aina ya uchezaji baada ya kuonekana kipindi cha kwanza Copco kujazana zaidi kati kuinyima Yanga kutawala eneo hilo. Kuingia kwa wachezaji Kibwana aliyekwenda kucheza beki wa kulia, kulimfanya Israel Mwenda kuhamia winga ya upande huo, huku Jonas Mkude akienda kiungo mkabaji kutoka beki wa kati akimuachia Dickson Job.
Dakika 15 za kipindi cha pili, Yanga ilikuwa ikianzisha mashambulizi yake maeneo yote, kati na pembeni hali iliyowafanya Copco muda mwingi kucheza eneo lao na kujikuta dakika ya 58 wakiruhusu bao lililofungwa na Prince Dube aliyetumia udhaifu wa walinzi kushindwa kujipanga vizuri kutokana na krosi iliyopigwa na Israel Mwenda.
Baada ya hapo, Yanga ikaendeleza mashambulizi langoni mwa Copco na kuandika bao la tatu kwa penalti dakika ya 68 mfungaji akiwa Maxi Nzengeli na mkwaju huo wa penalti ulitokana na yeye mwenyewe kufanyiwa faulo na nahodha wa Copco, Yusuph Amos Mgeta.
Kadiri muda ulivyokuwa unakwenda, Copco ilionekana kuchoka na kuiruhusu Yanga kuzidisha mashambulizi ambayo yalizaa bao la nne dakika ya 77 lililofungwa kwa kichwa na Duke Abuya aliyeunganisha krosi ya Nickson Kibabage.
Mudathir Yahya alikamilisha ushindi huo dakika ya 84 kwa bao la kichwa kupitia krosi ya Israel Mwenda.
Usajili mpya ndani ya Yanga, Israel Mwenda, huu ulikuwa mchezo wake wa kwanza wa kimashindano tangu ajiunge na kikosi hicho na ametoa asisti mbili kati ya mabao matano yaliyofungwa.
YANGA: Aboutwalib Mshery, Israel Mwenda, Nickson Kibabage, Jonas Mkude, Bakari Mwamnyeto, Salum Abubakar/John Misheto, Shekhan Khamis/Dickson Job, Duke Abuya, Prince Dube/Maxi Nzengeli, Aziz Ki/Kibwana Shomari na Farid Mussa/Mudathir Yahya.
COPCO: Joseph Adam, Berkhhof Ahab William, Mohamed January Alex, Andrew Frank Mahende, Yusuph Amos Mgeta, Ally Athuman Ekwabi, Simon Bulemo Bazili/Dickson Charles Mwizarubi, Rajab Rashid Rajab/Ibrahim Hashim Njohole, Rajesh Biku Kotecha/John Elias Masanzu, Joseph Moshi Samson/Bahati Posso na Jagadi Sola Gushaha/ Said Juma Manoni.