Gaza. Israel imethibitisha kuwapokea wanajeshi wake wanne waliokuwa wakishikiliwa mateka na kundi la Hamas eneo la Gaza kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Katika makubaliano hayo, raia 200 wa Palestina waliofungwa kwenye magereza mbalimbali nchini Israel pia wameachiwa huru kutoka katika magereza hayo.
Wafungwa hao wameachiwa kufuatia makubaliano ya kusitishwa mapigano hayo kutamka kuwa Israel itawaachia wafungwa 20 kwa kila mwanajeshi mmoja wa IDF atakayeachiwa kutoka Gaza.
Al Jazeera imeripoti kuachiwa kwa mateka hao, leo Jumamosi Januari 25, 2025 ambako kumeshuhudiwa na maelfu ya raia wa Gaza waliokusanyika eneo la Palestine Square nchini humo na kushuhudia mateka hao wakipandishwa kwenye magari ya Msalaba Mwekundu.
Majina ya wanajeshi hao wanawake walioachiwa leo kama yalivyotangazwa na Hamas, ni pamoja na Liri Albag, Karina Ariev, Danielle Gilboa na Naama.
Msemaji wa Kundi la Hamas, Abu Obeida alitangaza majina hayo jana na kusisitiza kuwa wanajeshi hao wataachiwa kabla ya kufika jioni ya leo Jumamosi.
Wakati wakiachiwa, familia zao zilikuwa zikifuatilia mubashara kutokea Israel na tayari wanajeshi hao wamewasili jijini Tel Aviv kwa ajili ya uchunguzi wa kina wa afya zao kabla ya kujumuika na wapendwa wao.
Mmoja wa mateka hao, Albag alitimiza miaka 19 akiwa mateka huku wenzake wakitimiza miaka 20 wakiwa mafichoni katika maeneo ya wapiganaji wa kundi hilo.
Kwa mujibu wa Al Jazeera, wanajeshi hao walichukuliwa mateka eneo la kambi ya kijeshi ya Nahal Oz, iliyopo takriban kilometa moja kutoka ulipo mpaka wa Gaza na Israel. Walitekwa kwenye shambulizi la kushtukiza la Oktoba 7, 2023.
Mabadilishano hayo ni sehemu ya utetekelezaji wa makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano kati ya IDF na wapiganaji wa kundi la Hamas yaliyodumu kwa zaidi ya siku 450.
Katika mabadilishano ya kwanza mateka watatu wa Israel waliachiwa huku raia 90 wa Palestina wakiachiwa huru.
Katika wiki sita za utekelezaji wa makubaliano hayo ya kusitishwa kwa vita yaliyofikiwa Doha nchini Qatar, Israel iliridhia kuwaachia Wapalestina 50 kwa kila mateka (mmoja) atakayekuwa anaachiwa na Hamas.
Hivyo, Wapalestina 200 wataachiwa kutoka gerezani baada ya kuachiwa kwa mateka (wanajeshi) wanne wanaoshikiliwa eneo la Gaza na wapiganaji hao wa Hamas.
Hata hivyo, vyombo vya habari nchini Israel vimeripoti kuwa majina yaliyotangazwa na Hamas hayaendani na matakwa ya makubaliano kwa kile kinachodaiwa kuwa matarajio ilikuwa kwamba kati ya wanne wanaochiwa leo, alipaswa kuwemo raia.
“Israel ilikuwa inataka raia ndiyo waachiwe kwanza, ndipo wanajeshi wafuatie kisha wafuatie wale ambao wanadhaniwa kuwa wanaumwa sana kutokana na kukaa kizuizini kwa muda mrefu ikiwa ni sehemu ya awamu ya kwanza ya makubaliano,” amesema mwandishi wa Al Jazeera, Hamduh Salut akiripoti kutokea Amman, Jordan.
Tangu kuachiwa kwa mateka watatu Jumapili iliyopita na kurejeshwa kwa mabaki ya mwili wa mwanajeshi wa Israel aliyotoweka mwongo mmoja uliopita, Israel ilitoa taarifa kuwa raia wake 94 walikuwa wanaendelea kushikiliwa eneo la Gaza.
Makubaliano ya kusitisha mapigano hayo yalifikiwa baada ya majadiliano ya muda mrefu kati ya pande hizo na kuratibiwa na mataifa kama vile Qatar, Misri na Marekani.
Katika awamu ya kwanza ya makubaliano hayo, Hamas iliridhia kuwaachia mateka 33 katika mabadilishano na maelfu ya wafungwa ambao ni raia wa Palestina walioko kizuizini nchini Israel.
Katika awamu inayofuata, pande hizo zilikubaliana kuachilia mateka na wafungwa wa kila upande sambamba na Israel kuondoa vikosi vyake eneo la Gaza baada ya mapigano yaliyodumu kwa zaidi ya miezi 15.
CNN imeripoti kuwa wakati wa kuachiwa, mateka hao watafanyiwa uchunguzi wa papo kwa papo wa hali ya afya zao kabla ya kukabidhiwa kwa maofisa wa Msalaba Mwekundu kwa ajili ya kurejeshwa nchini Israel.
Baada ya kuvuka mpaka na kuingia Israel, mateka hao watapelekwa hospitalini jijini Tel Aviv kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina iwapo hawana changamoto za kiafya zilizotokana na kuwa kizuizini eneo la Gaza kisha kukutanishwa na wazazi wao.
Wakati hayo yakiendelea, Gaza inapambana kuanza kurejesha miundombinu na makazi ambayo yameharibiwa vibaya kutokana na mashambulizi ya IDF yaliyolenga maeneo ya makazi kwa kisijgizio cha kuwatafuta wapiganaji wa Hamas.
Pia, raia wengine wa Gaza wamekuwa wakisita kurejea nyumbani kwao kwa hofu ya kurejea kwa mapigano kati ya pande hizo. Hata hivyo maelfu wanatajwa kurejea katika eneo hilo na kuanza upya ujenzi wa makazi yao.
Hadi sasa, Vita ya Israel na Hamas imesababisha vifo vya raia wa Palestina zaidi ya 47,283 huku 111,472 wakijeruhiwa tangu Oktoba 7, 2023. Pia raia 1,139 wa Israel waliuawa nchini Israel wakati wa uvamizi wa Hamas na kusababisha watu zaidi ya 200 kuchukuliwa mateka wakiwemo wanajeshi wa IDF.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.