Huduma za kisheria za Samia zawafikia zaidi ya  103,100 Mara

Musoma. Zaidi ya watu 103,100 wamefikiwa kupitia kampeni maalum ya huduma ya kisheria maarufu Mama samia Legal Aid, iliyofanyika mkoani Mara Desemba mwaka jana kwa muda wa siku 10.

Takwimu hizo zimetolewa mjini Musoma leo Jumamosi Januari 25, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi wakati akizindua wiki na siku ya sheria nchini kwa mkoa huo, ambapo amesema katika kipindi hicho jumla ya migogoro 1,303 ilipokelewa.

Mtambi amesema watu hao wamefikiwa kupitia kampeni hiyo iliyofanyika katika vijiji na mitaa 270 mkoani Mara, ambapo kati ya migogoro iliyofikishwa kwa wataalamu hao wa sheria jumla ya migogoro 224 ilipatiwa ufumbuzi papo hapo.

“Migogoro 1,079 inaendelea kupatiwa ufumbuzi na ni imani yangu  kuwa ufumbuzi utapatikana ndani ya muda mfupi,” amesema

Mtambi amesema mwitikio huo wa watu wengi kujitokeza kwaajili ya kupatiwa huduma za kisheria kwa muda huo mfupi, unaashiria kuwa huduma hiyo inahitajika kwa kiasi kikubwa kwa wananchi hasa wa kipato cha chini.

Amesema katika kipindi hicho pia wamebaini kuwa migogoro mingi inatokea kutokana na wananchi kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya masuala ya kisheria ambapo amewataka wakazi wa mkoa wa Mara kutumia maadhimisho ya wiki na siku ya sheria kufika katika maeneo yaliyotengwa, kwaajili ya kupata ushauri na elimu ya sheria juu ya masuala mbalimbali.

Mtambi pia amewaagiza watumishi wa umma hususan katika taasisi za kutoa haki kwa wananchi, kuhakikisha wanatoa haki kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, taratibu na weledi.

Awali Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Musoma, Fahmu Mtulya amesema katika maadhimisho hayo wanatarajia kutoa huduma za kisheria bila malipo katika maeneo mbalimbali ndani ya mkoa wa Mara ikiwemo katika Gereza la Musoma.

Jaji Mtulya amesema katika kipindi hicho pia watatoa elimu kwa wananchi ili kuelewa faida za kutatua migogoro kwa njia za usuluhishi badala ya kwenda mahakamani kama ambavyo imezoeleka.

“Utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi unatambulika kisheria lakini pia ni njia inayosaidia kupunguza milolongo mingi ikiwa ni pamoja na kutumia muda mfupi kumaliza mgogoro na hivyo kuruhusu wahusika kufanya shughuli zingine za kimaendeleo,” amesema

Baadhi ya wakazi wa Musoma wamesema ipo haja ya wadau kuunga mkono jitihada za Serikali kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinapatikana kwa watu wote,  bila kujali hali zao za kiuchumi kutokana na ukweli kuwa wengi wanashindwa kupata huduma hizo kwa  kutokuwa na uwezo kifedha.

“Umesikia hizo takwimu, hii inaonyesha watu wengi wana uhitaji wa huduma kisheria lakini hawana uwezo na ndio maana kwa muda mfupi watu waliojitokeza kwa wingi na hapo kuna baadhi ya maeneo hayakufikiwa. Nitoe wito kwa wadau waangalie namna ya kushirikiana na Serikali ili kuwafikia wananchi wengi,” amesema Paul Mgaya.

Ashura Masisa amesema gharama kubwa ya kupata huduma kutoka kwa wanasheria ni moja ya sababu zinazochangia watu wengi kukosa haki zao kisheria na hivyo kusababisha uwepo wa migogoro  katika jamii.

Related Posts