Ikanga Speed aachiwa Copco | Mwanaspoti

KIKOSI cha Yanga leo Jumamosi kinaanza rasmi harakati za kutetea ubingwa wa Kombe la Shirikisho la TFF wakati kitakapoikaribisha Copco ya Mwanza kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam, huku wachezaji wapya, Jonathan Ikangalombo na Israel Mwenda wakisubiriwa kuliamsha.

Ikangalombo maarufu kama Ikanga Speed na Mwenda wamesajiliwa na Yanga kupitia dirisha dogo lililofungwa Januari 15 mwaka huu wakitokea klabu za AS Vita ya DR Congo na Singida Black Stars ambapo mechi ya leo huenda wakaanza zikiwa ni za kwanza kwao tangu walipotambulishwa hivi karibuni.

Yanga inashuka uwanjani ikiwa ni siku kadhaa tangu ilipong’olewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiishia hatua ya makundi na namna pekee ya kuwafariji wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo ni kutwaa mataji mawili makubwa ya ligi ya ndani ambayo ni Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho inayoyatetea.

Uzoefu na ubora wa kikosi na mchezaji mmoja mmoja vinategemewa kuwa silaha kubwa kwa Yanga mbele ya Copco katika mchezo huo wa leo kulinganisha na wapinzani wao ambao wana kikosi kinachoundwa na kundi kubwa la wachezaji wasio na uzoefu wa kucheza mechi kubwa za ushindani.

Na mchezo huo sio muhimu kwa Yanga kama timu pekee bali hata wachezaji mmojammoja kama ilivyo kwa mshambuliaji Clement Mzize ambaye msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa mashindano hayo hivyo msimu huu atakuwa na kibarua cha kutetea tuzo yake. Mzize alibeba kwa kufunga mabao matano.

Huenda kikosi cha Yanga kikawa na mabadiliko kidogo katika mchezo wa leo ili kuwapa fursa baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa hawatumiki mara kwa mara kikosini

Yanga ina historia nzuri ya mechi za hatua ya 64 bora ya mashindano hayo ambapo katika misimu yote tisa ambayo mashindano hayo yamechezwa, haijawahi kupoteza mechi ya hatua hiyo.

Kwa upande wa Copco, haina historia nzuri katika hatua hiyo kwani mara zote ilizowahi kukutana na timu ya Ligi Kuu ilitupwa nje ya mashindano.

Kocha wa Copco, Lucas Mlingwa alisema wanatambua ubora wa Yanga na wanahisi mechi itakuwa ngumu kwa upande wao.

“Tumejiandaa vya kutosha kwa ajili ya hii mechi. Tumekuja kucheza tukiamini Yanga ni timu bora. Sisi tumekuja kukimbia uwanjani zaidi ya watakavyokimbia wao,” alisema Mlingwa.

Kocha wa Yanga, Sead Ramovic alisema kuwa kikosi chake kimejiandaa kupata ushindi katika mechi hiyo.

“Tutajaribu kushinda mechi kwa kile tulichonacho ili twende katika hatua inayofuata. Tuna wachezaji 25 ambao tunaweza kupanga 11 kati yao na wakacheza vizuri,” alisema Ramovic ambaye anasubiriwa kwa hamu na mashabiki na wapenzi kuona kama ataanza na Ikanga Speed na Mwenda ambao walisajiliwa dirisha dogo, mbali na mashine nyingine ambazo zimekuwa zikiishia benchini au jukwaani.

Yanga na watani wao Simba ndio timu pekee ambazo zilikuwa hazijacheza mechi za hatua hiyo ya 64 inayosaka timu mbili za kukamilisha timu 32 zitakazochuana hatua inayofuata. Tayari timu 30 zikiwamo za Ligi Kuu Bara, Ligi ya Championship, First League na Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) zimeshatingia hatua ya 32 Bora.

Droo ya mechi hizo zitapangwa hivi karibuni ili klabu hizo kuanza msako wa kutinga 16 Bora na hatua nyingine ikiwamo ya fainali itakayopigwa Mei 31.

Timu zilizofuzu 32 Bora ni; Stand United, Biashara United, Mbeya Kwanza, Transit Camp, Town Star, Polisi Tanzania, Songea United, Kiluvya, JKT Tanzania, Leo Tena, Kagera Sugar, Tabora United, Cosmopolitan, Bigman, Giraffe Academy na Geita Gold.

Nyingine ni Namungo, Coastal Union, Azam, Fountain Gate, TZ Prisons, Pamba Jiji, KMC, Mashujaa, Singida Black Stars, Mambali Ushirikiano, Mtibwa Sugar, TMA Stars, Green Warriors na Mbeya City.

Related Posts