Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeagiza Serikali kuimilikisha Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC), eneo linalojengwa kituo cha kujaza gesi kwenye magari ndani ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM).
Kwa mujibu wa TPDC kwa sasa eneo hilo wanalotumia kujenga kituo mama cha kujaza gesi asilia kwenye magari, wamekodi kwa makubaliano maalumu na chuo hicho.
Akijibu agizo hilo, Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amesema maagizo hayo yatafanyiwa kazi, kwani kamati hiyo imekuwa ikishauri mambo mengi yaliyosaidia kuboresha utendaji wa wizara hiyo.
Magizo hayo ya kamati ya Bunge yametolewa leo Januari 25, 2025 na mwenyekiti wake na David Mathayo baada ya kamati hiyo kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha kujaza gesi kwenye magari barabara ya Sam Nujoma.
“Kwa kuwa eneo linalojengwa kituo ni mali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na TPDC wamekodi na hawa wote wapo Serikali moja ni muhimu Serikali iangalie eneo hili limilikiwe moja kwa moja na TPDC badala ya ilivyo hivi sasa,” amesema.
Amesema ni muhimu chuo kikuu kuliachia eneo hilo lililojengwa kituo cha gesi ili TPDC iwe na eneo kubwa la kufanya shughuli zake huku akisisitiza maeneo ambayo mahitaji ya gesi ni makubwa hivyo miundombinu iharakishwe.
Mwenyekiti huyo amesema wataendelea kuishauri Serikali ili gesi inayopatikana nchini iwafikie wananchi wengi na kutatua kero ya kupanda kwa petroli na dizeli.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amesema: “Maagizo ya kamati tumeyapokea na wamekuwa wakitushauri lengo kuboresha utendaji wa Wizara,” amesema.
Naibu Waziri huyo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kujenga vituo vya kujaza gesi asilia kwenye magari pamoja na kuifikisha nishati hiyo majumbani.
Awali Kaimu Mkurugenzi wa TPDC Derick Moshi akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa kituo cha kujaza gesi kwenye magari amesema ujenzi umefikia asilia 90.
Amesema kituo hicho chenye uwezo wa kuhudumia magari nane kwa wakati mmoja kwa siku kina uwezo wa kuhudumia magari 1200 pamoja na uwepo wa eneo maalumu la kujaza gesi malori matatu kwa saa moja.
“Mradi huu ujenzi ulianza Mei,20204 na Kampuni ya Kimataifa ya Sinoma kwa gharama ya Sh18.9 bilioni ambazo zimegawanyika katika mikataba mitatu kituo mama Sh14.5 bilioni, kituo cha Muhimbili Sh1.99 bilioni na kituo cha Kairuki Sh2.39 bilioni na fedha zote ni za TPDC,” amesema.
Moshi amesema mradi huo ulipangwa kukamilika kwa miezi 18 yaani Desemba 2024 lakini changamoto ya mvua pamoja na kuchelewa kwa meli kuliathiri utekelezaji wa ujenzi wa kituo kwa wakati.
Hivi karibuni, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko alitembelea kituo hicho na kuahidi kukamilika mwanzo kwa Februari mwaka huu na kuanza kufanya kazi.