Marekani yaanza kuwafukuza wahamiaji, ndege za kijeshi zatumika

Washington. Ameanza! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Jeshi la Marekani kuanza utekelezaji wa amri iliyotolewa na Rais Donald Trump ya kuwarejesha kwao (deportation) wahamiaji haramu wanaoishi nchini.

Televisheni ya ABC news imeripoti leo Jumamosi Januari 25, 2025, kuwa mamia ya wahamiaji wameonakena wakipandishwa kwenye ndege za kijeshi huku wakiwa wamefungwa pingu na minyororo tayari kurejeshwa katika mataifa yao.

Miongoni mwa ndege hizo inadaiwa kuwabeba raia zaidi ya 80 wa Guatemala Alhamisi jioni, huku maelfu ya wanajeshi wakimwagwa kwenye mpaka wa Kusini mwa Marekani, Guatemala na Mexico.

Ikulu ya Marekani na `makao makuu ya jeshi la Marekani (Pentagon), imesema kipaumbele chao kwa sasa ni kuwarejesha wahamiaji katika mataifa yao.

Kwa mujibu wa ABC news, takriban wanajeshi 1,500 walipelekwa eneo la San Diego ambalo ni mpaka wa Marekani na Mexico, huku vikosi vya wanajeshi nchini Mexico wakiendelea na Ujenzi wa mahema kwa ajili ya wahamiaji hao.

Miongoni mwa ndege zilizoonekana zikiwabeba wahamiaji hao ni pamoja na ndege mbili aina ya Air Force C-17 iliyokuwa ikiwabeba kutokea Uwanja wa Kijeshi wa Davis-Monthan uliopo Tucson, Arizona, na Uwanja wa Biggs uliopo El Paso, Texas, nchini humo.

Takriban wahamiaji 80 walisafirishwa usiku wa kuamkia leo kupitia viwanja hivyo kwenda Guatemala.

ABC news pia imeripoti kuwa maofisa zaidi ya 1,000 kutoka Jeshi la taifa hilo, Polisi na vikosi vya ulinzi wa mpakani wanasafirishwa kuelekea maeneo yanayopakana na mataifa ya Kusini ili kutekeleza amri hiyo.

Taarifa ya kwanza kuchapishwa kuhusu kurejeshwa kwa wahamiaji hao kwao ilichapishwa kwenye akaunti ya Ikulu ya Marekani kupitia mtandao wa X (zamani Twitter) ikiwaonyesha wanajeshi wakijenga uzio eneo la San Diego na kuwafukuza wahamiaji waliokuwa wakipambana kupenya nchini humo.

“Kama alivyoahidi, Rais Trump ameanza kutuma ujumbe kwa Ulimwengu kuwa wanaoingia nchini Marekani bila kibali watachukuliwa hatua kali za kisheria,” imesema taarifa hiyo ya Ikulu ya Marekani.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Idara ya Ulinzi nchini humo, Joe Kasper, ametoa taarifa kwa Umma kuwa Serikali nchini humo inazuia usambazaji wa video za aina yoyote kuhusiana na Operesheni hiyo.

Kasper amesema uamuzi huo ulichukuliwa kwa lengo la kutoleta sintofahamu na kuongeza umakini kwa maofisa wanaoendelea na utekelezaji wa amri ya Rais Trump maeneo mbalimbali nchini humo.

“Tunataka kuwapatia mwanya maofisa wetu waendelee kutekeleza amri ya Rais Trump yenye lengo la kuifanya Marekani kuwa mahala salama kwa raia wa Marekani hususan ni usalama wa ndani na kwenye medani za kimataifa,” alisema Ofisa huyo.

Ndege hizo (mbili) zinatajwa kutumiwa kwa Mara ya kwanza kuwarejesha kwao wahamiaji hao tangu kuanzishwa kwa Kitengo cha USTRANSCOM kinachosimamia ndege hizo mwaka 1982.

Shirika la Ulinzi nchini humo, lilitoa taarifa kwa Umma kuwa litakuwa tayari kutoa usaidizi hususan ni kwenye shughuli za udhibiti wa mipaka nchini humo ambapo maofisa wake 2,500 watapelekwa watakapohitajika.

“Huu ni mwanzo tu, na ni hatua za awali kabisa za utekelezaji wa Operesheni yetu,” Msimamizi Mkuu wa Ulinzi wa mipaka nchini humo (Border Czar), Tom Homan aliieleza Televisheni ya ABC news.

Kwa mujibu wa Homan, Operesheni hiyo inalenga kuwarejesha kwao wahamiaji zaidi ya milioni 12 wanaoishi nchini Marekani kinyume na utaratibu na itafikia lengo hilo ndani ya kipindi cha miezi sita.

Wakati Homan akitoa kauli hiyo, Serikali nchini Mexico imeukosoa utawala wa Rais Trump kwa kile ilichodai utekelezaji wa sera ya kuwarejesha kwao wahamiaji kutoka nchini Marekani unalenga kuvunja ushirikiano kati ya mataifa hayo.

Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum amekuwa akisisitiza Trump kusitisha amri yake ya utekelezaji wa Sera ya Uhamiaji na kusema kuwa utekezaji wake utaharibu mahusiano ya muda mrefu kati ya mataifa hayo.

Wengi wa wahamiaji hao wanaonekana kuficha sura zao kwa kutumia barakoa huku wengine wakitokwa machozi kufuatia uamuzi huo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts