Mikoa, wananchi wanavyojiandaa kuepuka maafa utabiri wa TMA

Mikoani. Wananchi katika mikoa iliyotajwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) kuwa itakabiliwa na mvua za masika za juu ya wastani kati ya Machi hadi Mei, mwaka huu, wameeleza namna walivyojiandaa kuchukua tahadhari ili kuepuka madhara ya mvua hizo.

Pia, Serikali katika maeneo hayo zimeeleza hatua zitakazochukua kuwaepusha wananchi na madhara ya mvua za masika zilizotabiriwa na TMA ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kuhusu namna ya kuepuka na majanga.

Wananchi wameeleza hayo zikiwa zimepita siku mbili tangu TMA ilipotoa utabiri huo wa msimu wa mvua za masika,  ambapo mikoa 14 imetajwa kuwa na mvua za masika za chini ya wastani, wastani na juu ya wastani.

Mikoa iliyotajwa kupata mvua hizo ni Pwani, Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Morogoro, Tanga, Dar es Salaam na visiwa vya Unguja na Pemba. Mikoa inayopata mvua za wastani hadi juu ya wastani ni mashariki mwa mikoa ya Simiyu na Mara.

Wananchi katika Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wamejipanga kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya makazi yao ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mkazi wa Sengerema, Julius John ambaye anajishughulisha na uvuvi, amesema wao wakiwa wavuvi wamejipanga kuhakikisha  wanapokuwa ziwani, hawaathiriki na majanga yao kwa kutoa vifaa vya uokovu.

Mkoa wa Simiyu unachukua hatua mbalimbali kukabiliana na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha kama ilivyotolewa na TMA.

Katika hatua za kukabiliana na athari za mvua hizi, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Faiza Salim, ameeleza kuwa tayari serikali ya wilaya kupitia kamati ya maafa imeanza kuchukua hatua, hususan kwa wananchi ambao makazi yao yako kandokando ya Ziwa Victoria.

Amewahimiza wananchi kuondoka mara moja katika maeneo hatarishi ambayo katika msimu uliopita wa mvua katika mji wa Lamadi, yalizingirwa na maji ili kujiepusha na madhara yanayoweza kujitokeza iwapo mvua hizo zitanyesha kwa mujibu wa TMA.

Pia, amewahimiza wadau wa sekta mbalimbali kama vile kilimo, mifugo, afya na usafirishaji, kuchukua tahadhari kutokana na mvua zinazotarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika mkoa huo na mikoa mingine ya kanda ya Ziwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amewataka wadau wa maafa kutoa elimu kwa wananchi kuchukua tahadhari, lengo likiwa ni kuwajengea uelewa wananchi namna ya kujilinda pindi mvua hizo zitakapoanza.

“Kama watendaji wa umma, tuna kila sababu ya kuchukua na kuwatahadharisha wananchi kuhusu jambo hilo, na kama maafa yakiwakuta, tuna kila sababu ya kuchukua hatua kuhakikisha tunanusuru uhai na mali zao. Tuna kila sababu ya kunusuru miundombinu mbalimbali itakayoathirika na jambo hilo,” amesema.

Mohamed Said, mkazi wa mji wa Lamadi Wilaya ya Busega, amesema elimu kwa wananchi kuhusu maafa, inatakiwa kutolewa ili kuwajengea uelewa wananchi kuhusu tahadhari kuchukua pindi yanapotokea.

“Wadau wa maafa nawahimiza waweze kutoa elimu ya kutujengea kuelewa sisi wananchi kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa pindi maafa yanapojitokeza,” amesema.

Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mara wamesema ili kuepuka athari zinazoweza kutokea ni vema hatua zikachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwahamiaha watu wanaoishi katika maeneo hatarishi.

“Hakuna haja ya kubembelezana, kama mtu anaishi kwenye eneo hatari mfano kwenye kingo za mto au kwenye mabonde hatua zichukuliwe, waondolewe hata kwa nguvu ili kuepuka majanga,” amesema Yohana Kitebe.

Kwa upande wake, Makongoro Emmanuel amesema jitihada zaidi zinatakiwa kuwekwa kwenye miundombinu ya barabara hasa maeneo vijijini ili kurahisisha mawasiliano nyakati za mvua.

“Mara nyingi nyakati za mvua barabara zinakuwa hazipitiki na hii inakuwa ni hatari sana kwani wananchi wanakosa huduma muhimu, kwa hiyo napendekeza barabara ziboreshwe ili kuhakikiha wananchi wanapata huduma muhimu ikiwepo matibabu pale wanapohitaji,” amesema Emmanuel.

Serikali mkoani Mara imeziagiza kamati za ulinzi pamoja na za maafa katika wilaya zote za mkoa huo kufanya tathmini ya haraka na kuwaondoa watu wote wanaoishi katika maeneo hatarishi ikiwemo kwenye vyanzo vya mito na mabondeni ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua za masika.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amesema mkoa umejipanga ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza endapo kutakuwa na mvua zitakazozidi kiwango.

Amesema mbali na tathmini hiyo, pia, ameelekeza vyombo hivyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo ikiwepo magonjwa ya mlipuko.

Baadhi ya wananchi hasa wanaoishi kwenye maeneo yenye hatari ya kukumbwa na mafuriko wameiomba Serikali kurekebisha miundombinu kwa kufukua mifereji, makaravati na madaraja yaliyojaa mchanga, magogo na taka ngumu.

Katika Manispaa ya Morogoro, maeneo yenye hatari ya kukumbwa na mafuriko ni pamoja na Kihonda, Lukobe, Mkundi, Mafisa, Kichangangani, Mji mpya, Mwembesongo na Bigwa.

Mmoja wa wakazi wa kata ya Lukobe, Mgeni Matajili amesema pamoja na wakazi wa kata huyo kuchukua tahadhari na lakini bado haitaweza kusaidia kukabiliana na mafuriko hayo isipokuwa Serikali inapaswa kuwasaidia kwa kuboresha miundombinu hasa mifereji ama makorongo ya kupitishia maji ya mvua.

“Hata mafuriko ya mwaka jana kwa kiasi kikubwa yametokana na hii mifereji na makorongo kujaa na kuwa finyu kiasi cha kushindwa kubeba na kusafirisha maji kwenda kwenye mito mikubwa na hivyo kusababisha mafuriko kwa wananchi,” amesema Matajili.

Naye Aziz Habib amesema tangu mwaka jana aliamua kuihama nyumba yake na kwenda kutafuta makazi mengine ya muda na ameamua kufanya hivyo kwa sababu ya kuepuka madhara ya mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara.

“Januari, mwaka jana, nililazimika kuihama nyumba yangu niliyojenga kwa gharama kubwa maana niliona hakuna kitu chenye thamani kwenye maisha yangu zaidi ya uhai wangu na uhai wa familia yangu.

Related Posts