Mkongomani azitaka tatu za Simba

WAKATI Tabora United ikijifua kwa mchezo wa kiporo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba, kocha Anicet Kiazayidi amesema hana presha huku akisifu kiwango cha wapinzani wao.

Timu hizo zitakutana kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora utakaopigwa Februari 2 kwani katika mechi ya kwanza zilipokutana Uwanja wa KMC Complex, Simba ilishinda mabao 3-0, Agosti 18, mwaka jana.

“Licha ya kukaa kwa muda mrefu bila michezo ya ushindani ila mwelekeo wetu sio mbaya na maboresho ambayo tumeyafanya katika dirisha dogo. Utakuwa ni mchezo mgumu ila tunaendelea kujipanga ili kutumia vyema uwanja wetu,” alisema.

Kocha huyo aliongeza wana kazi kubwa ya kuendeleza walichokifanya msunguko wa kwanza akiipongeza Simba kwa kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Anicet aliyezifundisha AS Vita Club, FC Simba Kolwezi, FC Les Aigles du Congo na Maniema Union za kwao DR Congo, tangu ajiunge na kikosi hicho Novemba 2 hajapoteza mchezo wa Ligi Kuu.

Chini yake timu hiyo imecheza mechi sita bila kupoteza ikiifunga Mashujaa bao 1-0, Yanga (3-1), KMC (2-0), Azam (2-1), huku sare zikiwa na Singida Black Stars ya mabao 2-2 na 1-1 ilipokutana na Coastal Union.

Sare ya bao 1-1 iliyoipata Tabora dhidi ya Coastal Desemba 17, mwaka jana iliifanya timu hiyo kufikisha michezo saba mfululizo bila ya kupoteza tangu Oktoba 18.

Related Posts