Mserbia KenGold bado tatu za nguvu

KOCHA wa KenGold, Mserbia Vladislav Heric, amesema anahitaji zaidi ya michezo mitatu ya nguvu ya kirafiki ili kujiweka fiti na mzunguko wa pili, huku akiomba viongozi kufanyia kazi suala hilo haraka kabla ya Ligi Kuu Bara kurejea Februari Mosi.

Kauli ya kocha huyo inajiri baada ya kupata mchezo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Maafande wa Tanzania Prisons ulioisha kwa sare ya kufungana bao 1-1 wiki iliyopita huku akidai miongoni mwa nyota wa kikosi hicho wanahitaji pia muda.

“Ni kweli tumefanya usajili mkubwa na wa kuvutia, lakini baadhi ya wachezaji fitinesi zao ziko chini kwa sababu wengi walikuwa hawajacheza kwa muda mrefu. Tunaendelea kupambana na naamini kupitia michezo ya kirafiki itatusaidia kwa hilo,” alisema.

Kocha huyo aliyezifundisha Club Africain ya Tunisia, Chippa United, Maritzburg United, Ubuntu Cape Town, Bay United, Polokwane City, FC Cape Town zote za Afrika ya Kusini alisema kikosi hicho kinampa matumaini makubwa ya kufanya vizuri.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa KenGold, Benson Mkocha alisema wanaendelea kutafuta michezo mingine ya kirafiki kwa lengo la kukidhi matakwa ya benchi hilo jipya la ufundi, huku akijivunia zaidi uzoefu wa kocha huyo na wachezaji wapya.

“Jumatano ya Januari 29, tutakuwa na tamasha letu tulilolipa jina la ‘Makarasha Day’, lengo kubwa ni kutambulisha upya benchi la ufundi na wachezaji wapya, tutacheza pia mchezo wa kirafiki na tuko kwenye mazungumzo na timu za nje ya nchi.”

Mkocha alisema tamasha hilo lililopewa kaulimbiu ya ‘Saga Mwagia’ linalenga kutengeneza upya timu hiyo ikiwa ni ishara ya kujipanga tena na michezo ya mzunguko wa pili, huku wakipambana kukitoa kikosi hicho mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu.

Katika tamasha hilo watashuhudiwa mastaa wapya waliojiunga na timu hiyo ambao wamewahi kutamba na Yanga na Simba hapa nchini wakiwemo Bernard Morrison, Obrey Chirwa, Kelvin Yondani na Zawadi Mauya waliobeba matumaini ya kikosi hicho.

Kipimo cha kwanza cha Mserbia huyo katika Ligi Kuu Bara kitakuwa dhidi ya Yanga Februari 5, kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam, akiwa na kazi ya kukipambania kutoka mkiani baada ya kukusanya pointi sita tu katika michezo 16.

Related Posts